Spika Bunge la Afrika Kusini ajiuzulu kwa madai ya rushwa

Muktasari:


  • Spika Nosiviwe Mapisa-Nqakula amekanusha tuhuma hizo, lakini amechukua hatua hiyo, ili kupisha uchunguzi.

Afrika Kusini. Spika wa Bunge la Afrika Kusini, Nosiviwe Mapisa-Nqakula amejiuzulu nafasi hiyo jana Jumatano Aprili 3, 2024 baada ya kuenea kwa tuhuma za kupokea rushwa kati ya mwaka 2016 hadi 2019.

Hatua hiyo ameichukua baada ya kupeleka ombi mahakamani la kuzuia kukamatwa kutokana na tuhuma hizo.

Waendesha mashtaka wiki iliyopita walisema wanakusudia kumfungulia mashtaka Spika Nosiviwe Mapisa-Nqakula ya madai ya rushwa, wakimtuhumu kupokea takriban Dola 135,000 za Marekani (Sh348.3 milioni) za rushwa akiwa waziri wa ulinzi.

Inadaiwa alipokea fedha hizo kati ya Desemba 2016 na Julai 2019.

Mapisa-Nqakula alitangaza katika taarifa yake kwamba amewasilisha kujiuzulu kwake, lakini akasisitiza kuwa hana hatia kutokana na tuhuma zinazomkabili.

"Nimefanya uamuzi huu makini, ili kujitolea muda na umakini wangu kushughulikia uchunguzi uliotangazwa hivi karibuni dhidi yangu na vyombo vya sheria vya nchi yetu," alisema. "Kujiuzulu kwangu sio dalili au kukiri kuwa na hatia kuhusu tuhuma zinazotolewa dhidi yangu."

Ripoti za vyombo vya habari nchini Afrika Kusini zinadai kuwa katika tukio moja Februari 2019, alipokea zaidi ya dola 15,000 na wigi kwenye mkutano kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa nchi hiyo.