Tetemeko la ardhi laua watu 129
Muktasari:
- Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 5.6 limesababisha vifo vya watu zaidi ya 129 Magharibi mwa Nepal jana Ijumaa.
Nepal. Zaidi ya watu 129 wamepoteza maisha baada ya tetemeko la ardhi kupiga eneo la Magharibi mwa Nepal jana Ijumaa na kusababisha pia uharibifu wa mali na miundombinu.
Vikosi vya usalama vimetumwa kusaidia juhudi za uokoaji katika wilaya za Jajarkot na Rukum Magharibi, kilomita 500 Magharibi mwa Kathmandu.
Kwa mujibu wa CNN tetemeko kali lilisikika katika Mji Mkuu wa Nepali na miji ya nchi jirani ya India, ikiwemo New Delhi.
Matetemeko mengine matatu yalisikika ndani ya saa moja baada ya tetemeko hilo, na watu wengi wakilala sehemu za wazi usiku mzima kwa sababu ya kuhofia matetemeko zaidi na uharibifu wa nyumba zao.
Kanda za video kwenye vyombo vya habari vya ndani zilionyesha nyumba nyingi zilivyoharibiwa huku watu wakichimba vifusi gizani ili kuvuta manusura kutoka kwenye mabaki ya majengo yaliyoporomoka.
Waziri Mkuu wa Nepal, Pushpa Dahal amewasili katika eneo lililoathiriwa leo Jumamosi, na kueleza huzuni yake ya watu kupoteza maisha na mali zilizoharibiwa na tetemeko hilo.
Pia alisema ameviagiza vyombo vya usalama kuanza mara moja zoezi la uokoaji na shughuli za misaada.
Hata hivyo shughuli hizo za utafutaji na uokoaji zinatatizwa na barabara kuzibwa na maporomoko ya ardhi ambayo yalisababishwa na tetemeko hilo.
Mkuu wa polisi wa wilaya ya Jajarkot, Suresh Sunar ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa ilikuwa vigumu kupata picha kamili ya nini kilichotokea.
“Tunakusanya maelezo lakini kutokana na baridi na usiku ni vigumu kupata taarifa kutoka maeneo ya mbali," alisema Sunar.
Tetemeko hilo lilirekodiwa saa 5:47 usiku saa za ndani kulingana na Kituo cha Ufuatiliaji na Utafiti cha Nepal.
Wakala wa Jiolojia wa Marekani walipima tetemeko hilo la ukubwa wa 5.6 na kusema kuwa ni tetemeko la ardhi lenye kina kirefu, kumaanisha kwamba lilitokea karibu na uso wa dunia.
Mnamo 2015, nchi ilikumbwa na matetemeko mawili mabaya ya ardhi ambapo watu 9,000 walipoteza maisha na 22,309 kujeruhiwa.
Tetemeko la kwanza la Aprili 25, 2015 lilikuwa la kipimo cha 7.8 ambalo lilisababisha uharibifu mkubwa na kupoteza maisha. Idadi kubwa ya mitetemeko ilifuata mwezi wa Mei mwaka huo.
Matetemeko hayo yaliharibu zaidi ya nyumba 800,000 hasa katika wilaya za Magharibi na kati, kulingana na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu.
Imeandaliwa na Victor Tullo kwa msaada wa mashirika.