Tetesi za kuzima intaneti kwenye maandamano ya kesho nchini Kenya
Nairobi. Rais wa Chama Cha Wahariri Kenya (KEG), Churchill Otieno amesema wamepata tetesi juu ya mpango wa Serikali kutaka kuzima intaneti na vituo vyote vya utangazaji siku ya kesho kwa sababu ya maandamano.
Kauli hiyo ameitoa Otieno Leo, Jumapili Aprili 2, 2023 ikiwa nchi hiyo chini ya kiongozi wa umoja wa upinzani wa Azimio la Umoja, Raila Odinga ikifanya maandamano ya kupinga kupanda kwa bei za vyakula kila siku ya jumatatu.
"Endapo tetesi hizi zitakuwa na ukweli, hili litakuwa tukio baya zaidi kuwahi kutokea nchini kwa sababu linanyima haki ya kupata taarifa ya wananchi," amesema Otieno katika taarifa yake.
Pia, Otieno amesema tukio hilo endapo likitokea kwa upande wa vyombo vya habari litarudisha nyuma uhuru wa habari.
Kenya ambayo inaongozwa na Rais William Ruto wa umoja wa Kenya Kwanza imekuwa katika msuguano wa kisiasa na upande wa upinzani unaoongoza na Waziri Mkuu msataafu wa nchi hiyo Odinga, baada ya Ruto kukataa maridhiano na upinzani Mara tu baada ya kutangazwa mshindi wa Uchaguzi ulipofanyika Agosti 2022.