Tisa wafariki dunia, 1,000 wajeruhiwa tetemeko likiipiga Taiwan

Muktasari:

  • Tetemeko hilo lenye ukubwa wa 7.4 ni baya zaidi tangu mwaka 1999.

Taiwan. Takribani watu tisa wamefariki dunia, huku wengine 1,000 wamejeruhiwa baada ya tetemeko la ardhi kuipiga Taiwan jana Jumatano na kuharibu pia makumi ya majengo.
Shirika la Habari la AFP limesema kufuatia tetemeko hilo lenye ukubwa wa 7.4 katika kipimo cha Richa, limesababisha tahadhari za tsunami hadi katika mataifa ya Japan na Ufilipino.
Maofisa wa nchi hiyo wamesema tetemeko hilo ndilo lenye nguvu zaidi kutikisa kisiwa hicho katika kipindi cha miaka 25, huku wakionya kuhusu tetemeko zaidi katika siku zijazo.


Wu Chien-fu, mkurugenzi wa Kituo cha Taipei cha Central Weather Administration's Seismology Center, amesema tetemeko lilikuwa kubwa zaidi tangu lilipotokea lile la ukubwa wa 7.6, Septemba, mwaka 1999, na kuua karibu watu 2,400.
Aidha, imeelezwa moja ya tukio baya ni lile la watu watatu waliokuwa wakitembea jijini Taipei kukandamizwa hadi kufa na mawe yaliyoteremka kutokana na tetemeko hilo.
Pia, Shirika la Kitaifa la Zimamoto limesema vifo vyote vimetokea katika kaunti ya Hualien na kuongeza kuwa watu 1,011 kote Taiwan wamepata majeraha.
Hadi  jana usiku, inaelezwa eneo hilo bado lilikuwa likikumbwa na mitetemeko midogo midogo, huku waokoaji wakiendelea na kazi ikiwemo ya kuondoa vifusi vilivyotapakaa barabarani.