Tisa wauawa Senegal wakipinga hukumu ya kiongozi wa upinzani

Polisi wakiwarushia mabomu ya machozi wafuasi wa kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko huko Dakar, Senegal, wakati wa machafuko kufuatia hukumu yake ya miaka miwili jela.

Muktasari:

  • Watu tisa wameuawa nchini Senegal ikiwa ni katika hatua za kupinga hukumu iliyotolewa na mahakama nchini humo dhidi ya kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko akitiwa hatiani kwa makosa ya unyanyasaji wa kijinsia.

Senegal. Takribani watu tisa wameuawa nchini Senegal katika mapigano kati ya polisi na wafuasi wa kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko kufuatia mahakama nchini humo kumhukumu kifungo cha miaka miwili jela, wizara ya mambo ya ndani ya nchi hiyo imesema.

Kwa mujibu wa Al Jazeera, mapigano yalizuka baada ya uamuzi huo wa Mahakama uliotolewa jana Alhamisi, ambao huenda ukamzuia Sonko, mpinzani mkubwa wa Rais Macky Sall, kuwania uchaguzi wa urais mwaka ujao.

Magari na mabasi yalichomwa moto katika mji mkuu wa Dakar na ghasia ziliripotiwa mkatika maeneo mengine ya nchi ikiwa ni pamoja na jiji la Ziguinchor, ambako Sonko amekuwa meya tangu 2022.

"Tumeona ghasia ambazo zimesababisha uharibifu wa mali na kwa bahati mbaya kumetokea vifo tisa Dakar na Ziguinchor," Waziri wa Mambo ya Ndani Antoine Diome amesema kwenye televisheni ya taifa leo Ijumaa.

Sonko (48) hakuhudhuria wakati wa kusikilizwa kwa madai yanayomkabili ya unyanyasaji wa kijinsia ambapo alishtakiwa kwa kumbaka mwanamke ambaye alifanya kazi katika chumba cha masaji mnamo 2021, huku akidaiwa kutishia kumuua mwanamke huyo japo Sonko amekanusha na kusema mashtaka hayo yalichochewa kisiasa.

Mahakama ilimuondolea Sonko kosa la ubakaji lakini ikamtia hatiani kwa kosa la lingine lililoelezwa kwamba ni tabia mbaya dhidi ya watu walio na umri wa chini ya miaka 21.

Wizara ya sheria ilisema kiongozi huyo wa upinzani sasa anaweza kupelekwa gerezani wakati wowote.

Polisi walisalia kuzunguka nyumba yake huko Dakar huku machafuko yakipamba moto katika mji mkuu na maeneo mengini nchini humo kufuatia hukumu hiyo.

"Kwa hukumu hii, Sonko hawezi kuwa mgombea," alisema mmoja wa mawakili wa kiongozi wa upinzani, Bamba Ciss, akinukuu sheria ya uchaguzi ya Senegal.

Chama cha Sonko cha PASTEF kilisema uamuzi huo ni sehemu ya njama ya kisiasa na kuwataka raia katika taarifa yake, kusimamisha shughuli zote za uzalishaji na kuingia barabarani kwa maandamano kupinga hukumu hiyo.

Siku ya Alhamisi, moshi mzito ulifuka kutoka katika Chuo Kikuu Cha Dakar, ambapo waandamanaji walichoma mabasi kadhaa mchana na kuwarushia mawe Polisi wa kutuliza ghasia ambao walijibu kwa kurusha mabomu ya machozi.

Msemaji wa Serikali Abdou Karim Fofana alisema vikosi vya usalama vinadhibiti hali katika mji mkuu.

Mitandao kadhaa ya kijamii na majukwaa ya kutumiana ujumbe yamezuiwa nchini Senegal hatua ambayo imetajwa kuathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wa umma kuwasiliana, kitengo cha uchunguzi cha mtandao cha NetBlocks kilisema.

Profesa wa sheria wa chuo kikuu Ndiack Fall alisema Sonko anaweza kutaka kesi isikilizwe upya ikiwa atajisalimisha kwa mamlaka. Lakini wafuasi wa Sonko wamekashifu mashtaka hayo kama njama ya kumzuia kushiriki katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari.