Traore aibuka na jingine kwa wasomi Burkina Faso
Rais wa Burkina Faso, Ibrahim Traore
Muktasari:
- Rais Ibrahim Traore ametaka wanafunzi wa PhD wazalishe ubunifu wa vitendo badala ya tafiti za nadharia pekee ili kutunukiwa Shahada hiyo.
Dar es Salaam. Rais wa Burkina Faso, Ibrahim Traore ameibua mjadala mpya kuhusu mwelekeo wa elimu nchini humo baada ya kutaka vyuo vikuu kubadili mfumo wa kutoa Shahada za Uzamivu (PhD), akiwataka wahitimu kuonyesha uwezo wao kwa kutengeneza suluhisho la vitendo badala ya uandishi wa tasnifu pekee.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari nchini Burkina Faso, Traore amesema wanafunzi wanaosomea fani za teknolojia na uhandisi wanapaswa kuhitimu wakiwa na uwezo wa kutengeneza bidhaa, mashine au ubunifu unaoweza kusaidia kutatua changamoto za maendeleo ya nchi hiyo.
Akizungumza na vijana katika eneo la Yaadga, kaskazini mwa Burkina Faso, leo Jumanne Julai 28, 2026, Traore amesema elimu haipaswi kuzalisha wataalamu wanaobaki na maarifa ya vitabu pekee bila kuyatumia katika kutatua matatizo yanayoikabili jamii.
Amesema wanafunzi wanapaswa kutumia teknolojia na vyanzo mbalimbali vya maarifa kujifunza na kubuni vitu vinavyoweza kuleta mabadiliko.
“Vijana, tumieni intaneti kutafuta maarifa. Nakilini kila kitu mnachoweza kunakili isipokuwa nadharia. Tunaweka mazingira yote muhimu ili muweze kufanikiwa,” amesema Traore.
Amesema katika vyuo vya teknolojia vinavyoanzishwa nchini humo, mwanafunzi wa uhandisi hatakiwi kumaliza masomo yake kwa karatasi pekee, bali anatakiwa kuonesha uwezo wa kutengeneza kitu.
“Kama wewe ni mhandisi, kwa tasnifu yako unatakiwa kutengeneza, kunakili au kujenga kitu. Vinginevyo hatutaendelea kuunga mkono uandishi wa karatasi ndefu,” amesema.
Mbali na vyuo vikuu, Traore amesema mfumo huo unatakiwa kuanza pia katika shule za ufundi, ambako wanafunzi wanapaswa kupimwa zaidi kwa uwezo wao wa vitendo kuliko nadharia pekee.
Kauli hiyo ni sehemu ya msisitizo mpana wa Traoré kuhusu kujenga Burkina Faso inayojitegemea kupitia uzalishaji wa ndani, teknolojia na ubunifu.
Si mjadala wa kwanza
kwenye elimu
Tangu kuingia madarakani mwaka 2022, Traore amekuwa akichukua hatua mbalimbali zinazolenga kubadili mwelekeo wa nchi hiyo katika sekta ya elimu, hatua ambazo zimekuwa zikizua mijadala ndani ya nchi hiyo.
Kauli yake hii imeja baada ya kutoa kauli nyingine iliyoibua mjadala alipotangaza wanaokwenda nje kusoma masomo ya dini kuzingatia elimu ya ujuzi wa Sayansi na Teknolojia ili kuja kuisaidia nchi yao.
Katika msimamo wake huo kuhusu elimu ya dini, mamlaka zinatajwa kuwa zimekuwa zikisisitiza usimamizi zaidi wa taasisi za elimu zinazohusiana na masuala ya dini, hasa katika mazingira ya changamoto za usalama zinazoikabili nchi hiyo.
Katika mjadala huo, wafuasi wa Traore wamekuwa wakiona sera zake kama jitihada za kujenga kizazi chenye uwezo wa kujitegemea na kuzalisha suluhisho la ndani, huku wakosoaji wakitaka tathmini zaidi kuhusu namna utekelezaji wa mageuzi hayo unavyofanyika.