Burkina Faso yaja na kombati mpya za kijeshi za asili
Muktasari:
- Kombati hizo zimetengenezwa kwa kutumia kitambaa cha asili ikiwa ni sehemu ya kudumisha uzalendo.
Burkina Faso. Nchi ya Burkina Faso imezindua sare mpya za kijeshi kwa wanafunzi wa Chuo cha Kijeshi cha Prytanée Militaire de Kadiogo (PMK), hatua inayotajwa kuwa sehemu ya mkakati wa kuimarisha uzalendo, kukuza viwanda vya ndani na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Tofauti na sare za awali, mavazi hayo yametengenezwa kwa asilimia 100 kwa kutumia Faso Dan Fani, kitambaa cha asili kinachosokotwa kwa mikono na kutambulika kama moja ya alama muhimu za utamaduni na utambulisho wa taifa hilo la Afrika Magharibi.
Sare hizo zimezinduliwa katika mahafali ya maofisa wapya wa kijeshi Julai 25, 2026 na Rais wa nchi hiyo Kapteni Ibrahim Traore.
Hatua hiyo imepokelewa kama mwendelezo wa sera za Burkina Faso zinazolenga kuhimiza matumizi ya bidhaa zinazozalishwa nchini humo, sambamba na juhudi za kujenga uchumi unaojitegemea kupitia sekta za viwanda na nguo.
Kwa mujibu wa tovuti ya Africalix na TRT Afrika, Chuo cha Prytanée Militaire de Kadiogo, kinachosimamiwa na Wizara ya Ulinzi ya Burkina Faso, kina jukumu la kuwaandaa vijana kuwa viongozi wa baadaye katika sekta za kijeshi na kiraia kwa kuwajengea maadili, taaluma na uwezo wa uongozi.
Taasisi hiyo imekuwepo tangu mwaka 1951 na imezalisha baadhi ya viongozi mashuhuri wa kijeshi nchini humo.
Faso Dan Fani ni kitambaa kinachosokotwa kwa kutumia pamba ya ndani na kwa miongo kadhaa kimekuwa ishara ya utaifa wa Burkina Faso.
Umaarufu wake uliongezeka wakati wa utawala wa hayati Thomas Sankara katika miaka ya 1980, ambapo matumizi ya bidhaa za ndani yalihimizwa ili kukuza uchumi wa taifa na kupunguza utegemezi wa bidhaa za nje.
Katika miaka ya karibuni, serikali ya Burkina Faso imeendelea kusisitiza matumizi ya kitambaa hicho katika mavazi rasmi na hata sare za shule, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuendeleza viwanda vya ndani na kuhifadhi urithi wa kitamaduni.
Hata hivyo, taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa sare hizo mpya zinawahusu wanafunzi wa Chuo cha Kijeshi cha PMK pekee, na si kwamba zimechukua nafasi ya sare za operesheni zinazovaliwa na wanajeshi wote wa Jeshi la Burkina Faso.
Hadi sasa hakuna tangazo rasmi linaloonyesha kuwa jeshi lote limeanza kutumia sare hizo katika shughuli za kivita au operesheni nyingine.