Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Traore aifungia virago ofisi ya haki za binadamu UN nchini Burkina Faso

Muktasari:

  • Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa utaifunga ofisi yake ya haki za binadamu nchini Burkina Faso ifikapo Novemba 30, 2026, kufuatia kusitishwa kwa shughuli zake na mamlaka ya kijeshi, hatua iliyozua mjadala mkali kuhusu demokrasia, haki za binadamu na uhusiano wa nchi hiyo na ulimwengu ya Magharibi.



Dar es Salaam. Umoja wa Mataifa (UN) umetangaza utaifunga rasmi ofisi yake ya Haki za Binadamu nchini Burkina Faso ifikapo Novemba 30, 2026.

Ni baada ya serikali ya kijeshi ya nchi hiyo kusitisha kwa muda usiojulikana shughuli za ofisi hiyo, hatua iliyosababisha taasisi hiyo kukosa uwezo wa kuendelea na kazi zake za ufuatiliaji, uchambuzi na ulinzi wa haki za binadamu.

Katika taarifa yake, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa imesema uamuzi huo si hiari, bali ni matokeo ya mazingira yaliyowekwa na mamlaka ya Burkina Faso, yaliyofanya operesheni za ofisi hiyo kushindikana.

Kamishna Mkuu wa taasisi hiyo, Volker Turk amesema hatua ya kusitishwa kwa shughuli hizo imeifanya ofisi kushindwa kutimiza jukumu lake la msingi la kulinda haki za binadamu nchini humo.

Ofisi hiyo ilianzishwa Oktoba 2021 ikiwa na jukumu la kufuatilia hali ya haki za binadamu, kutoa ripoti za uchambuzi na kusaidia kujenga uwezo wa taasisi za Serikali, hususan vikosi vya usalama na ulinzi.

Kabla ya kusitishwa kwa shughuli zake, ilishatoa mafunzo ya sheria za kimataifa kwa takribani maofisa 4,000, hatua iliyolenga kuimarisha uwajibikaji katika sekta ya usalama.

Hali hii inatokea katika mazingira ya kisiasa yenye historia ya misukosuko nchini Burkina Faso, taifa ambalo kwa miaka mingi limekabiliwa na changamoto za kiusalama, mashambulizi ya makundi ya wanamgambo na udhaifu wa taasisi za dola.


Alivyoingia madarakani

Kabla ya mapinduzi ya 2022, serikali ya kiraia ilikuwa ikikumbwa na shinikizo kubwa la kushindwa kudhibiti hali ya usalama, hali iliyosababisha kukua kwa hasira ya wananchi na jeshi.

Ndani ya mazingira hayo ndipo alipoingia madarakani Kapteni Ibrahim Traore, Septemba 2022 kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyoundoa uongozi wa kiraia.

Traore, kijana mwenye umri mdogo kulinganisha na viongozi wengi wa Afrika, aliingia madarakani akiahidi kurejesha usalama, kupigania uhuru wa kiuchumi, na kupunguza utegemezi wa nchi yake kwa mataifa ya magharibi, ambayo kwa muda mrefu yamekuwa na ushawishi mkubwa katika Afrika Magharibi.

Mara baada ya kuchukua madaraka, utawala wake ulijikita katika mkakati wa kujenga upya usalama wa ndani kupitia operesheni za kijeshi dhidi ya makundi ya wanamgambo, sambamba na mabadiliko ya kimfumo ndani ya taasisi za dola.

Hata hivyo, hatua zake zilianza kuambatana na ukosoaji kutoka kwa mashirika ya kimataifa na baadhi ya mataifa ya Magharibi, yakisema kuna dalili za kupungua kwa uhuru wa kiraia, vyombo vya habari na nafasi ya asasi za kiraia.


Mvutano ulipoanzia

Mvutano kati ya utawala wa Traore na taasisi za kimataifa ulianza kujidhihirisha wazi pale serikali yake iliposimamisha shughuli za kisiasa, ikiwemo kufuta vyama vya siasa na kuimarisha itawala wa kijeshi.

Tangu wakati huo, Traole amekuwa akituhumiwa kutawala kwa mabavu na kukanyaga haki za kiraia nchini humo, akiibuka kuwa kiongozi wa Afrika wa kizazi cha leo anayekosoa waziwazi sera za mataifa ya magharibi.

Aidha, hatua ya kuitaka Ofisi ya Haki za Binadamu ya UN nchini humo kusitisha shughuli zake, Umoja wa Mataifa umeitafsiri kama kikwazo katika utekelezaji wa majukumu ya haki za binadamu.

Hapo ndipo mchakato wa kufungwa kwa ofisi hiyo ulipoanza rasmi, na sasa umetangazwa kukamilika ifikapo Novemba 2026.


Wadau wagawanyika

Hatua hiyo imewagawa wachambuzi wa siasa za Afrika, wengine wakimtuhumu Rais Traole kukanyaga misingi ya utawala bora huku wengine wakisema utendaji wa ofisi hiyo ndiyo sababu kuu kukomeshwa kwake.

Wakili na mchambuzi wa siasa, Dk Onesmo Kyauke, amesema hatua ya kufungwa kwa ofisi hiyo ni ishara ya kurudi nyuma kwa misingi ya demokrasia na utawala bora nchini Burkina Faso.

"Haki za binadamu, haki za kujieleza na uhuru wa raia ni haki za kuzaliwa. Hakuna mwenye mamlaka ya kuzikanyaga. Traoré hata kama anafanya vizuri kwenye mambo mengine, matendo haya yanapunguza uhalali wa utawala bora," amesema.

Ameongeza kuwa mwenendo wa utawala wa kijeshi kukandamiza sauti mbadala unapaswa kuibua wasiwasi mkubwa ndani na nje ya Afrika.

"Kunyanyasa upinzani na kuzima harakati za haki za binadamu ni kuonyesha dalili za kurudi nyuma kwa demokrasia. Afrika hatupaswi kushangilia mwenendo huo," ameongeza.

Kwa upande mwingine, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Conrad Masabo anaona mgogoro huu unatokana na tofauti ya msingi ya vipaumbele kati ya Afrika na mataifa ya Magharibi kuhusu dhana ya haki.

"Unapozungumzia haki, zipo haki za kisiasa na za kiuchumi. Mataifa ya Magharibi yamekuwa yakisisitiza zaidi haki za kisiasa, wakati viongozi wa Afrika wanasisitiza zaidi haki za kiuchumi na usalama," amesema.

Amefafanua kuwa katika mtazamo huo, Traoré anaonekana kama kiongozi anayejenga msimamo wa kujitegemea, hasa katika mazingira ya usalama na rasilimali za taifa.

"Hili linatengeneza mgongano wa moja kwa moja kati ya taasisi za kimataifa na viongozi wa Afrika wanaotaka mabadiliko ya mfumo," ameongeza.

Mtaalamu wa Sayansi ya Siasa, Dk Paul Loisulie, anaona sakata hili kama sehemu ya mvutano mpana wa kiitikadi duniani, kati ya mifumo ya ubepari na mitazamo ya kijamii ya utawala.

"Afrika kiasili ina mwelekeo wa kijamii, lakini imeingizwa katika mfumo wa kibepari unaoambatana na masharti ya demokrasia ya Magharibi," amesema.

Ameeleza kuwa viongozi wanaopinga mfumo huo hujikuta wakikabiliwa na shinikizo la kimataifa na wakati mwingine kutengwa kisiasa.

"Anayepingana na mfumo huo huanza kuonekana kama tishio la kimataifa, na hatimaye hutengwa au kushinikizwa kubadili mwelekeo wake," amesema.