Trump akutwa na kesi ya unyanyasaji kingono

Muktasari:
- Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump amekutwa na kesi ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya mwandishi Jean Carrol, Mahakama ya Manhattan imesema.
New York. Jinamizi bado linamtafuna Rais wa zamani wa Marekani Dornald Trump baada ya mahakama mjini Manhattan kumkuta na kosa la kumnyanyasa kingono mwandishi wa jarida Jean Carrol (79). Shirika la Habari la BBC limeripoti.
Inadaiwa Trump alitenda kosa hilo miaka ya 1990 kwa mwanamke huyo katika duka moja kuu la jijini New York.
Carrol alifungua kesi katika mahakama ya Shirikisho ya Manhattan mwaka jana akidai Trump alimbaka katika chumba cha kubadilishia nguo cha duka kuu la Bergdorf Goodman karibu na nyumba yake ya Fifth Avenue.
Jana Mei 9, 2023 Jopo la majaji tisa kwa mara ya kwanza lilimpata Trump na hatia ya unyanyasaji wa kingono na kosa la kumtamkia maneno ambayo hayakuwa sahihi kumwita mwandishi huyo muongo.
Akizungumza na waandishi wa habari Carrol amesema alifungua kesi kwa ajili ya kusafisha jina lake na kurejesha amani ya maisha yake pia ulimwengu ujue ukweli juu yake na Trump.
“Nilifungua kesi dhidi ya Trump ili kusafisha jina langu na kurejesha amani ya maisha yangu na leo hatimaye ulimwengu umejua ukweli juu yangu,” amesema Carrol.
Mathalan, majaji hao wamesema hawakupata ushahidi wa kutosha kuwa Trump alimbaka mwandishi huyo kama ilivyokuwa ikidaiwa.
Kiongozi huyo ambaye ametangaza nia ya kuwania tena Urais mwaka 2024 amewashutumu wapinzani wake wa Chama cha Democratic kuwa wanatumia kesi hiyo kumchafua kisiasa.
Hata hivyo mahakama hiyo iliamuru Trump kumlipa Carrol fidia ya dola milioni tano ambayo ni sawa na Sh11.5 bilioni.
Mbali na hayo wakili wa Trump amesema kiongozi huyo anapanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Imeandaliwa na Dorcas Hhando