Rais mstaafu Donald Trump kuchunguzwa

Donald Trump

Muktasari:

  • Wizara ya Sheria ya Marekani juzi ilimtaja mpelelezi wa zamani wa uhalifu wa kivita kama wakili maalumu wa kusimamia uchunguzi wa uhalifu dhidi ya Donald Trump, siku tatu baada ya rais huyo wa zamani kutangaza kuwa atagombea tena uchaguzi wa rais wa mwaka 2024.

Washington, Marekani. Wizara ya Sheria ya Marekani juzi ilimtaja mpelelezi wa zamani wa uhalifu wa kivita kama wakili maalumu wa kusimamia uchunguzi wa uhalifu dhidi ya Donald Trump, siku tatu baada ya rais huyo wa zamani kutangaza kuwa atagombea tena uchaguzi wa rais wa mwaka 2024.

Trump, ambaye anadai kuwa ‘anawindwa na wachawi’, alikashifu hatua hiyo akisema isiyo ya haki na siasa chafu katika nchi yao.

Ikulu ilikanusha vikali uingiliaji wowote wa kisiasa, lakini uchunguzi wa mawakili maalumu ambao haujawahi kushuhudiwa wa Rais wa zamani na mgombea wa sasa wa urais unaweka mazingira ya vita vya kisheria.

Katika mkutano na waandishi wa habari, Mwanasheria Mkuu Merrick Garland alitangaza uteuzi wa Jack Smith, ambaye alikuwa mwendesha mashtaka mkuu huko The Hague, akichunguza uhalifu wa kivita wa Kosovo, kuchukua jukumu la chunguzi mbili zinazoendeshwa dhidi ya Trump.

Uchunguzi mmoja unaangazia juhudi za Rais huyo wa zamani za kutengua matokeo ya uchaguzi wa 2020 na shambulio la Januari 6, 2021 dhidi ya Ikulu ya Marekani lililofanywa na wafuasi wake.

Nyingine ni uchunguzi wa hifadhi ya nyaraka za siri za Serikali zilizonaswa wakati Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) lilipovamia kwenye makazi ya Trump ya Mar-a-Lago huko Florida Agosti mwaka huu.

Mwanasheria Garland alisema kumtaja wakili maalumu ni kwa manufaa ya umma kwa sababu Trump wa chama cha Republican na mrithi wake wa Chama cha Democratic, Joe Biden wameeleza nia yao ya kugombea 2024, ingawa ni Trump pekee ndiye ametangaza rasmi kwa sasa.

“Kuteua wakili maalumu kwa wakati huu ni jambo sahihi,” Garland alisema. “Hali za ajabu zilizowasilishwa hapa zinahitaji jambo kama hilo.”

Katika Ikulu, Katibu wa Habari wa White House, Karine Jean-Pierre alisema Biden hakuwa na taarifa ya mapema ya mipango ya Garland ya kutaja wakili maalumu.

‘Si haki’

Katika mahojiano na Fox News Digital, Trump alidai alikuwa akilengwa na utawala wa Biden ili kumzuia kushinda tena urais katika uchaguzi ujao.

“Hii ni aibu na inatokea tu kwa sababu ninaongoza katika kila kura katika vyama vyote viwili,” alisema. “Haikubaliki. Si haki. Ni ya kisiasa sana.”

“Huu hautakuwa uchunguzi wa haki,” Trump aliwaambia wageni baadaye nyumbani kwake Mar-a-Lago.

“Matumizi mabaya ya nguvu ya kutisha ya hivi sasa ni katika msururu mrefu wa ‘mawindo ya wachawi’,” alisema, huku akishangiliwa.

Katika taarifa yake, Smith, ambaye hapo awali aliongoza Idara ya Haki na Uadilifu wa Umma, alisema “kasi ya uchunguzi haitasitishwa au kupunguzwa kasi.”

“Nitatoa uamuzi huru na nitasogeza uchunguzi mbele kwa haraka na kwa kina kwa matokeo yoyote kwa kadiri ukweli na sheria itakavyoamuru,” alisema.

Kuingia kwa Trump katika kinyang’anyiro cha White House Jumanne iliyopita kunafanya kumshtaki kuwe jambo gumu zaidi.

Uteuzi wa mwendesha mashtaka huru kusimamia uchunguzi huo pacha unaweza kusaidia kumzuia Garland, mteule wa Biden, kutokana na mashtaka kwamba uchunguzi huo unachochewa kisiasa.

Wakili huyo maalumu ndiye atakayeamua iwapo Rais huyo wa zamani atakabiliwa na mashtaka yoyote, lakini Mwanasheria Mkuu ndiye atakuwa na uamuzi wa mwisho kuhusu iwapo mashtaka yanafaa kufunguliwa.

Hata kama atashtakiwa, Trump, mwenye umri wa miaka 76, bado anaweza kugombea urais, hakuna chochote katika sheria za Marekani kinachomzuia mtu anayeshtakiwa au aliyepatikana na hatia ya uhalifu kufanya hivyo.

Akiwa madarakani, Trump alichunguzwa na wakili maalumu, Robert Mueller kuhusu kuzuia haki na uwezekano wa kula njama na Russia katika uchaguzi wa mwaka 2016, lakini hakuna mashtaka yaliyofunguliwa dhidi yake.


Shida nyingine za kisheria

Mbali na uchunguzi, Trump anakabiliwa na matatizo mengine ya kisheria.

Mwanasheria Mkuu wa Jimbo la New York, Letitia James, amefungua kesi ya madai dhidi ya Trump na watoto wake watatu, akiwatuhumu kwa udanganyifu wa biashara.

Na Trump anachunguzwa kwa kushinikiza maofisa katika Jimbo la Kusini mwa Georgia kutengua ushindi wa Biden wa mwaka 2020, ikiwa ni pamoja na simu iliyorekodiwa ambayo sasa ni maarufu ambapo alimtaka waziri wa mambo ya nje ‘atafute’ kura za kutosha za kutengua matokeo.

Tangazo la mapema lisilo la kawaida la Trump kwamba anagombea urais mwaka 2024 lilionekana na baadhi ya wachambuzi mjini Washington kama jaribio la kuepusha mashtaka ya uhalifu yanayoweza kufunguliwa.

Mwanzoni mwa wiki, Trump alitangaza azma yake ya kuwania urais kwa mara ya tatu, katika jaribio nadra sana la kiongozi wa zamani wa Marekani kutaka kuingia tena Ikulu baada ya kushindwa katika uchaguzi.

Ikiwa atashinda urais, Trump atakuwa na umri wa miaka 78 atakapoapishwa. Na ingawa huo ni umri wa Biden alipoingia Ikulu, kutamfanya kuwa Rais wa pili kuwa na umri mkubwa katika historia ya Marekani.

Muda unakuwa na athari zake kwa njia tofauti kwa watu tofauti, lakini mizigo inayoongezeka kutokana na umri haiwezi kuepukika.

Hakuna uhakika kwamba Trump anaweza kustahimili aina ya kampeni kali zinazohitajika ili kushinda uteuzi wa Chama cha Republican iwapo atashindana na wagombeaji wachanga zaidi.