Mahakama yamwachia huru aliyefungwa miaka 30 kwa wizi, ubakaji

Muktasari:
- Ilielezwa siku ya tukio mrufani huyo akiwa eneo lake la kazi, alipita wakala wa kusajili laini za simu (mwathirika wa tukio hilo) na kutaka asajiliwe laini ila hakuwa na kitambulisho, hivyo kumuomba wakala huyo aende naye hadi nyumbani kwake ili akachukue kitambulisho, ila wakiwa njiani alimbaka kando ya mto.
Arusha. Mahakama ya Rufani imefuta hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela dhidi ya Kenedy Andrew, aliyekuwa amehukumiwa kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha na ubakaji.
Uamuzi huo umetolewa baada ya Mahakama kujiridhisha kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka haukuthibitisha makosa hayo bila kuacha shaka.
Mahakama hiyo imeamuru Kenedy aachiliwe huru kutoka gerezani ambapo awali alishtakiwa kwa kutenda makosa hayo kwa wakala wa kusajili wa laini za simu.
Mahakama hiyo ya rufani iliyoketi Mbeya imetoa hukumu hiyo Julai 3, 2025 na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.
Rufaa hiyo ya jinai ilikuwa ikisikilizwa na majaji watatu wa Mahakama hiyo ya juu nchini ambao ni Ferdinand Wambali, Gerson Mdemu na Latifa Alhinai Mansoor, rufaa iliyokuwa imetokana na uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.
Jaji Mdemu amesema baada ya kupitia mwenendo wa kesi ya msingi na kumbukumbu za rufaa hiyo wamejiridhisha kuwa makosa hayo dhidi ya mrufani hayakuthibitishwa kama sheria inavyoelekeza.
Msingi wa rufaa
Awali Kenedy alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Momba kwa makosa mawili.
Shitaka la kwanza lilikuwa ni wizi wa kutumia silaha kinyume na kifungu cha 287A na la pili ni ubakaji kinyume na kifungu cha 130 (1) (2) (e), vyote vya Kanuni ya Adhabu.
Kwa mujibu wa upande wa mashitaka, mrufani anadaiwa kuiba simu mbili za mkononi aina ya tecno F1 na halotel, mali ya mwathirika wa tukio hilo ambaye katika kesi hiyo alidaiwa alimtishia kwa kisu wakati anaiba vitu hivyo, kisha akambaka.
Tukio hilo lilitokea Oktoba 11, 2018 katika eneo la Mpande, wilayani Tunduma ambapo ilielezwa kuwa shahidi huyo wa pili alikutana na Kenedy eneo lake la kazi ambapo mrufani huyo alitaka kusajili laini ya mtandao wa Halotel.
Ilielezwa kuwa kwa kuwa hakuwa na kitambulisho chochote, alimuomba wakala huyo (mwathirika wa tukio hilo), kwenda naye nyumbani kwake ili akachukue kitambulisho amsajilie laini hiyo.
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa ilichukua karibu saa mbili kufika nyumbani kwa Kenedy na kuwa licha ya wasiwasi aliokuwa nao wakala huyo, mrufani alimtia moyo.
Ushahidi uliendelea kuwa walipofika kando ya mto, Kenedy alimshika wakala hiyo akamnyang’anya simu zake mbili alizokuwa nazo, akamvuta hadi kwenye jiwe kubwa lililokuwa karibu, kisha akamvua nguo na kumbaka ambapo alimtishia na kisu alichokuwa nacho.
Ilielezwa kuwa alipomaliza kitendo hicho alimuamuru wakala huyo aondoke, ambapo aliokolewa na mtu mmoja ambaye jina lake na utambulisho wake haukuelezwa mahakamani.
Tukio hilo liliripotiwa katika kituo cha polisi, usiku wa siku hiyo na shahidi wa kwanza Pendo Ndiu, alifanya uchunguzi wa kimatibabu kwa mwathirika wa tukio hilo na kufanikisha kukamatwa kwa mrufani.
Mwishoni mwa kesi yake iliyojumuisha mashahidi saba wa upande wa mashitaka na shahidi mmoja kutoka upande wa utetezi, mahakama hio ilimtia hatiani na kumuhukumu adhabu hiyo.
Rufaa
Hii ni rufaa yake ya pili ambapo rufaa ya kwanza aligonga mwamba, Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.
Katika rufaa hii ya pili Kenedy alikuwa na sababu sita za rufaa ikiwemo, kesi ilikiuka kifungu cha 214 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya. 20 (CPA), kesi dhidi yake haikuthibitisha bila kuacha shaka yoyote.
Nyingine ni Hakimu alikosea kisheria kwa kutogundua kwamba mrufani alishtakiwa kwa ubakaji wa kisheria wakati mwathirika alikuwa mtu mzima, ambapo katika rufaa huyo Kenedy hakuwa na uwakilishi wa wakili.
Wakili wa Jamhuri katika rufaa hiyo aliieleza mahakama kuwa kumbukumbu ya rufaa inaonyesha kesi hiyo ilisikilizwa na mahakimu wawili ambapo hakimu wa kwanza alirekodi ushahidi wa shahidi wa kwanza hadi wa sita.
Alieleza kuwa hakimu wa pili alirekodi ushahidi wa shahidi wa saba na utetezi wa mrufani na ndiye aliyetoa hukumu hiyo na kuwa rekodi ya mahakama ilikuwa kimya kuhusu sababu za kesi hiyo kuhamishiwa kwa hakimu wa pili.
Aliendelea kueleza kuwa, upungufu huo unakinzana na kifungu cha 214 cha CPA, hivyo kudhoofisha mwenendo wa kesi na hukumu nzima hivyo kuiomba mahakama kubatilisha mwenendo wa kesi kuanzia hatua ya kurekodi ushahidi wa shahidi wa saba na kuendelea, na kurudishwa mahakama hiyo ya chini na hukumu mpya iandaliwe.
Kuhusu kosa la ubakaji alieleza kuwa mwathirika wa tukio hilo alikuwa na umri wa miaka 23 hivyo haikuwa sahihi kuandaa shitaka chini ya kifungu cha 130 (1) (2) (e) na 131 (1) cha Kanuni ya Adhabu.
Amesema kifungu hicho kinatumika kwa waathirika wa ubakaji ambao umri wao ni chini ya miaka 18 na kuongeza kuwa mahakama hiyo ya awali haikutoa uamuzi iwapo mrufani alikuwa na kesi ya kujibu katika shitaka la kwanza la wizi wa kutumia silaha. Badala yake ulikuwa kuhusiana na shitaka la pili la ubakaji pekee na kuwa mrufani hakujitetea kuhusu kosa la kwanza na wakili huyo kuhitimisha kuwa makosa hayo hayawezi kutibika kwani mrufani hakujitetea.
Wakili huyo wa Serikali alieleza kutokana na mazingira hayo, kesi dhidi ya mrufani haikuwa ya haki hivyo kuiomba mahakama hiyo kuruhusu rufaa hiyo.
Uamuzi majaji
Jaji Mdemu amesema katika kushughulikia rufaa hii, wameangalia masuala matatu ambayo yanaonekana kujitokeza wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo.
Ametaja masuala hayo ni kuhusiana na kasoro katika shitaka la kwanza la ubakaji ambapo kifungu cha 214 cha CPA kuhusu mabadiliko ya mahakimu wa kesi na tatu, namna ambavyo matokeo ya kesi ya msingi yalifikiwa na hakimu mfawidhi kwa mujibu wa kifungu cha 231 cha CPA hakikufuatwa.
Jaji Mdemu amesema katika hukumu kuna makosa matatu ya kiutaratibu ambayo mahakama hiyo ilifanya ambayo ni kufanya uamuzi wa kesi ya msingi kuhusiana na shitaka la pili la ubakaji pekee, hakuna kilichosemwa kuhusu kosa la kwanza.
Amesema hiyo ilikuwa ni kinyume na kifungu cha 231 cha CPA ambacho kinaitaka mahakama kutoa uamuzi wa kesi ya kujibu au la kuhusu mashitaka yanayomkabili mshtakiwa.
“Hakuna sehemu yoyote katika rekodi ya rufaa iliyoonyeshwa kwamba mrufani alijitetea mwenyewe kwa shitaka la wizi wa kutumia silaha. Hata hivyo, mahakama iliendelea kumtia hatiani mrufani kwa makosa yote mawili, yaani, wizi wa kutumia silaha na ubakaji,” amesema.
Jaji Mdemu amesema kutokana na dosari hizo imebaini kuwa Mahakama mbili zilikosea kushikilia kuwa kesi ya mashitaka ilithibitishwa kama inavyotakiwa kisheria.
Alihitimisha kwa kueleza kuwa wanaruhusu rufaa hiyo na kufuta hukumu katika makosa yote mawili na kuamuru mrufani kuachiliwa kutoka gerezani.