Trump aukaribia ushindi Marekani
Muktasari:
- Trump, mgombea urais wa Republican, ameshinda majimbo muhimu ya North Carolina na Georgia, akipata kura za majimbo 248 dhidi ya Kamala mwenye 214.
Washington D.C. Mgombea urais wa Marekani kupitia chama cha Republican, Donald Trump ameshinda katika majimbo mawili muhimu ya North Carolina na Georgia, hivyo kujiweka katika nafasi nzuri ya ushindi.
Hadi sasa, Trump amepata kura za majimbo (electoral college) 248 huku mpinzani wake, Kamala Harris akipata kura 214. Ili kutangazwa mshindi, lazima mgombea apate kura 270 za majimbo, hivyo Trump ameikaribia nafasi hiyo kwa mara nyingine.
Rais huyo wa zamani, anaongoza kwa kura 67,341,630 (sawa na asilimia 51.2), wakati Kamala akiwa na kura 62,080,264 (sawa na asilimia 47.4) ya kura zilizohesabiwa hadi sasa.
Katika baadhi ya maeneo, picha zinaonyesha wafuasi wa Trump wakiwa furaha, wakisherehekea katika baadhi ya sehemu za Marekani, huku mgombea wao wa urais akisonga mbele katika matokeo yaliyotarajiwa.
Wengine wamevalia kofia zilizoandikwa ‘Make America Great Again’, kaulimbiu ya kampeni ya Trump, huku wengine wakiwa wamejifunika bendera ya Marekani.
Kwa mujibu wa BBC, takriban dakika 30 zilizopita, uwanja ulio katikati ya Chuo Kikuu cha Howard ulikuwa umejaa wafuasi wa Kamala tayari kusherehekea.
Kwa kupoteza katika majimbo ya North Carolina na Georgia, ukumbi wa karamu ya usiku wa uchaguzi wa Kamala ghafla umesalia mahame.
Mamia ya wafuasi wake wanaondoka katika ukumbi huo, wengi sasa wanakataa kuzungumza na vyombo vya habari, kwani uwezekano wa ushindi wa Kamala unaonekana kupotea. Kamala pia hatarajiwi kuzungumza kwenye hafla hiyo kama ilivyokuwa imepangwa.
Endapo Trump ambaye ni Rais wa 45, atashinda uchaguzi huo, atatangazwa kuwa Rais wa 47 wa Marekani, taifa lililoongozwa na marais 46 tangu lilipopata uhuru mwaka 1776.