Vifo vitokanavyo na tetemeko la ardhi Uturuki, Syria vyafikia 4,300
Muktasari:
- Watu zaidi ya 4,300 wamefariki dunia kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea nchini Uturuki huku idada ikitajwa kuongezeka kwa kasi.
Dar es Salaam. Vikosi mbalimbali vya uokoaji nchini Uturuki vinaendelea kutoa msaada kwa manusura walioangukiwa na majengo kutokana na tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.8 lililotokea mashariki mwa nchi hiyo na nchi jirani ya Syria, ambapo takriban watu 4,300 wamefariki dunia huku idadi ikitarajiwa kuongezeka kwa kasi.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo vimesema nchi mbalimbali duniani zimetuma timu zao ili kusaidia katika juhudi za uokoaji kutokana na idadi ndogo ya wafanyakazi wa dharura waliokuwepo.
Katika jimbo lote la Hatay, kusini-magharibi mwa kitovu cha tetemeko la ardhi, maafisa wanasema kwamba majengo 1,500 yaliharibiwa na watu wengi waliripoti jamaa zao kukwama chini ya vifusi bila msaada au timu za uokoaji kuwasili.
Maelfu ya wananchi katika mji wa Gaziantep ulio umbali wa kilomita 33 (maili 20) kutoka eneo la lililoathirika watu walikimbilia katika maduka makubwa, viwanja vya michezo, misikiti na vituo vya jamii kutokana na hofu.
Katika ahadi za hivi punde za usaidizi wa kimataifa, Rais wa Korea Kusini Yoon Suk-yeol amesema anajiandaa kutuma kwa haraka timu ya watu 60 ya utafutaji na uokoaji pamoja na vifaa vya matibabu.
Serikali ya Pakistan ilituma ndege iliyobeba vifaa vya usaidizi na timu ya watu 50 ya utafutaji na uokoaji mapema leo Februari 7, na kusema kutakuwa na safari za ndege za kila siku kuelekea Syria na Uturuki kuanzia Jumatano.
India ilisema itatuma timu mbili za utafutaji na uokoaji, ikiwa ni pamoja na mbwa wenye mafunzo maalum na wafanyikazi wa matibabu.