Waasi waua watu 114 nchini Mali

Muktasari:

  • Makumi ya raia wameuawa nchini Mali, kufuatia shambulio lililofanywa na wanamgambo wenye itikadi kali dhidi ya mashua moja iliyokua ikisafirisha watu kupitia mto Niger.

Mali. Wanamgambo wenye itikadi kali wameshambulia mashua moja katika mto ulioko kaskazini mashariki mwa Mali, na kuua takriban watu 49, Serikali ya mpito imesema.

Pia wanamgambo hao wameripotiwa kushambulia kambi ya jeshi na kuua wanajeshi 15, huku wapiganaji wapatao 50 wakisemekana kufariki na Serikali kutangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa.

Tishio la wanamgambo hao limekuwa likiongezeka licha ya madai ya jeshi kwamba wapiganaji mamluki wa kundi la Wagner, wangeweza kusaidia kukabiliana na makundi ya kigaidi ya nchini humo.

Kwa mujibu wa BBC, tangu mwishoni mwa mwezi uliopita, mji wa kaskazini wa Timbuktu umekuwa chini ya vizuizi na kumekuwa na mashambulizi mengine kadhaa hivi majuzi.

Wanamgambo wenye itikadi kali wameripotiwa kushambulia mashua hiyo ilipokuwa ikisafiri kwenye Mto Niger kutoka mji wa Gao kuelekea Mopti. Wanamgambo pia walishambulia kambi ya jeshi katika eneo la Gao.

Jeshi la Mali limesema kwenye mitandao ya kijamii kwamba mashua hiyo imeshambuliwa na makundi ya kigaidi yenye silaha.

Kiongozi wa mashua hiyo, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa mashua hiyo ilikuwa ikilengwa na angalau roketi tatu zilizolenga injini zake.

Mashua hiyo ilizimwa kwenye mto na jeshi liliingia kuwaondoa abiria, amesema kiongozi huyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Kulikuwa na uungwaji mkono mkubwa kwa jeshi la serikali wakati lilipotwaa mamlaka baada ya maandamano makubwa dhidi ya Rais wa wakati huo Ibrahim Keïta.

Tangu wakati huo, takwimu zinaonyesha kuwa serikali ya kijeshi ya Mali imepiga hatua ndogo katika mapambano yake dhidi ya makundi ya kigaidi yanayodhibiti baadhi ya sehemu za nchi.