Wadau washauri mbinu mashirika ya umma kuepuka hasara

Muktasari:

 Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) imeendesha mjadala X-Space uliokuwa na mada ya isemayo: “Kipi kinaweza kuwa suluhu ya kudumu kwa mashirika ya umma yanayojiendesha kwa hasara?”

Dar es Salaam. Wadau wa maendeleo nchini  wamependekeza njia zinazopaswa kuchukuliwa na Serikali,  ili mashirika ya umma yajiendeshe kwa weledi na kupata faida ikiwemo nafasi ya mkurugenzi kutangazwa hadharani na wenye sifa waombe.

Mapendekezo mengine, kazi zitolewe kwa mkataba, mashirika yapewe mitaji, mashirika yatengenezewe malengo, mashirika yajenge utararibu wa kubana matumizi,  kuboresha uwajibikaji na kujifunza kutoka mashirika binafsi.

Maoni hayo yametolewa na wadau leo Jumatano Aprili 3, 2024 katika mjadala wa Mwananchi X Space uliokuwa na mada ya isemayo: “Kipi kinaweza kuwa suluhu ya kudumu kwa mashirika ya umma yanayojiendesha kwa hasara?”

Machi 28, 2024 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu (CAG), Charles Kichere aliwasilisha ripoti ya mwaka 2022/23 kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ikionyesha baadhi ya mashirika ya umma yameendelea kujiendesha kibiashara likiwemo ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).

Akizungumza katika mjadala huo, Meneja wa fedha kutoka taasisi ya Wajibu, Jackon Mmali amesema ili mashirika yajiendeshe vizuri ni lazima nafasi ya mkurugenzi mkuu itangazwe na mamlaka zifikirie kuruhusu Watanzania au raia wa nje wenye uwezo wa kufanya biashara waruhusiwe kuomba.

“Kwa kuanzia tuanze hata na Watanzania wanaoshi nje ya nchi waruhusiwe kuomba, wafanyiwe usaili na wataalamu au timu iliyobobea katika maeneo hayo na majina matatu au mawili yatakayoonekana bora yachukuliwe na kupelekwa kupigiwa kura,” amesema.

Amesema wakati wa kuteuliwa ndani ya mkataba yao wawekewe malengo ya kibiashara mathalani kuboresha utendaji wa shirika na anatakiwa kutengeneza kiasi gani cha faida kwa kuzingatia muda aliopangiwa.

Mmali amesema ilivyo sasa watendaji wa mashirika mengi ya umma wanashindwa kufahamu kama yalianzishwa kwa lengo la kuleta ufanisi katika utendaji kazi na kutoa huduma za kijamii hasa katika maeneo ambayo sekta binafsi haziwezi.

“Hali hiyo inatokana na watumishi wengi wanaofanya kazi katika mashirika hayo hawakuomba kufanya kazi katika maeneo hayo,  isipokuwa wanahamishiwa kutoka mashirika mengine na inawasababishia kukosa kuwa na malengo,” amesema

Hoja hiyo iliungwa mkono na Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda aliyesema si kila kazi ya umma inapaswa kuwa ya kudumu bali kunatakiwa kuanzishwa utaratibu wa kuanza kutoa kazi kwa mkataba.

“Tunaweza kumpatia miaka minne tukiona anafanya vizuri tunarudia kumpatia mkataba mwingine baada ya kuona anafanya vizuri lakini akionekana hafanyi vizuri anapatiwa mwingine,” amesema.

Kwa upande wake, Mwandishi mwandamizi kutoka gazeti la Mwananchi, Elias Msuya amesema njia nyingine mashirika hayo yanapaswa  kujifunza kutoka kwa mashirika binafsi yanayozalisha kwa faida na Serikali iyawekee malengo na wakishindwa itafutwe namna yingine ya kuwa simamia.

“Mashirika mengi yanakufa kwa sababu bodi zake si imara kwa sababu zinaundwa watu ambao hawana uzoefu… ‘’ amesema.

Kwa upande wake, mtaalamu wa masuala ya uwekezaji na fedha, Ahobokile Mwaitenda  amesema changamoto kubwa kwa mashirika umma ni muundo wa utawala  wakurugenzi wanaokaa ndani ya muda mfupi na kuondolewa.

“Watu wanatakiwa kukaa kwa muda mrefu ili watekeleze mipango na malengo na kama mashirika ya kutengeneza faida wawe wanapatikana kwa kuzingatia uwezo wao kwa kufanyiwa mahojiano bila kuhusisha mamlaka za kisiasa,” amesema.

Amesema changamoto nyingine ni kukosa mitaji ya kujiendesha huku akitolea mfano Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), limepata hasara kwa sababu halikupewa na mtaji wakati linaanzisha biashara na badala yake lilikuwa linaazima ndege kutoka serikalini.

“Kwa hiyo ATCL ilikuwa inatakiwa kulipa kodi ya kukopa na walikuwa wanaingia gharama kuzifanyia matengenezo ndege hizo,” amesema.

Mwaitenda amebainisha changamoto nyingine ni matumizi ya ovyo ya fedha kwa sababu watu wanaokabidhiwa ofisi za mashirika hayo hawajali maendeleo ya taasisi ya husika.

“Tunapaswa kuboresha uwajibikaji pale mtu anapokosea hatakiwi kuhamishiwa kwenda  sehemu nyingine, tujifunze kama wanavyofanya Kenya watendaji wanapimwa kila baada ya muda fulani na kuachana na kufanya kazi kwa utamaduni wa kudumu,” amesema.