Wanajeshi wanne wa Israel wauawa kwa mlipuko

Wanajeshi wa IDF waliouawa kwenye mlipuko huko Rafah jana Juni 10, 2024. Picha na Times of Israel

Muktasari:

  • Wanajeshi¬† wawili walipoingia ndani ya jengo la ghorofa tatu, lililipuka na kusababisha sehemu yake kuwaangukia baadhi ya askari ndani ya nyumba hiyo.

Rafah.  Jeshi la Israel (IDF) limethibitisha vifo vya wanajeshi wanne vilivyotokana na mlipuko uliotokea Juni 10, 2024 wakati wa mapigano kati yao na Hamas, eneo la Rafah Kusini mwa Gaza.

IDF imewataja wanajeshi hao kuwa ni Sajenti Eitan Karlsbrun (20), Meja Tal Pshebilski Shaulov (24), Sajenti Yair Levin (19) na Sajenti Almog Shalom (19) waliokuwa wakifanya kazi kitengo cha upelelezi cha Givati Brigade, huku Shalom na Levin wakiwa bado mafunzoni.

Kwa mujibu Tovuti ya Times of Israel awali wanajeshi hao walilipua nyumba waliyoitilia shaka katika eneo la Rafah cha Shaboura.

Baada ya muda askari wawili waliingia kwenye jengo hilo la ghorofa tatu, ndipo lililipuka na kusababisha sehemu ya kuta kuanguka baadhi ya askari wakiwa ndani.

Taarifa inaeleza wanajeshi wegine saba wamejeruhiwa.

IDF imesema ndani ya jengo hilo kuligunduliwa handaki ikielezwa lilikuwa likitumiwa na wapiganaji wa kundi la Hamas.

Vifo ya wanajeshi hao vinafanya idadi ya waliouawa tangu kuanza kwa operesheni ya ardhini eneo la Gaza, Oktoba 27, 2023 kufikia 299.

Kampeni ya kijeshi ya Israel huko Gaza imesababisha vifo vya takribani watu 37,124, wengi wao wakiwa raia.

Mapigano Gaza yamechochewa na shambulio la Hamas la Oktoba 7, 2023 dhidi ya Israel.

Usuluhishi wa Blinken

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken atafanya mazungumzo na viongozi wakuu wa upinzani wa Israel leo Jumanne Juni 11 ikiwa ni siku moja baada ya kuwasili nchini humo kushinikiza mpango wa kusitisha mapigano Gaza.

Ziara yake ni sehemu ya harakati za Marekani za kutaka kusitishwa kwa mapigano yaliyodumu kwa miezi minane kati ya Israel na kundi la Hamas.

Blinken atakutana na Benny Gantz, mkuu wa zamani wa jeshi aliyejiondoa katika Serikali ya Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu.

Wawili hao watakutana Tel Aviv, pamoja na kiongozi wa upinzani Yair Lapid.

Ziara ya Blinken ni ya nane tangu aanze harakati za kutafuta usuluhishi katika eneo hilo.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana Juni 10, 2024 lilipitisha azimio lililoandaliwa na Marekani linalounga mkono mpango wa wiki sita wa kusitisha mapigano.

Mpango huo unataka Israel kujiondoa katika makazi ya watu eneo la Gaza na Hamas kuwaachia huru mateka wanaoshikiliwa kutokana na mashambulizi ya Oktoba 7, 2023.


Imeandikwa na Sute Kamwelwe kwa msaada wa mtandao.