Waziri Mkuu Peru ajiuzulu kwa madai ya rushwa

Waziri Mkuu wa Peru, Alberto Otárola

Lima. Waziri Mkuu wa Peru, Alberto Otárola (57) amejiuzulu kwa madai ya kujaribu kutumia ushawishi wa wadhifa wake, kumsaidia mwanamke kupata zabuni za serikali zenye faida kubwa.

Otarola aliwaambia waandishi wa habari mjini Lima jana kwamba; "Katika mazungumzo na Rais wa Jamhuri (Rais Dina Boluarte), nimetangaza uamuzi wa kuwasilisha barua ya kujiuzulu kwangu."

Wiki iliyopita baadhi ya vyombo vya habari nchini Peru vilitoa sauti iliyorekodia, ikidaiwa ya Otarola akisikika akizungumza na mwanamke, ambaye baadaye alianza kufanya kazi katika majukumu mbalimbali ya serikali.

Hata hivyo, Otarola alivieleza vyombo vya habari sauti hiyo ni ya mwaka 2021, wakati huo hakuwa ofisa wa serikali, na ilibadilishwa na kuhaririwa kama sehemu ya njama ya wapinzani wake wa kisiasa. Awali alikana kutenda uhalifu wowote.

Kuvuja kwa sauti hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje, Javier Gonzalez-Olaechea jana Jumanne alisema kwamba Rais wa Peru, Dina Boluarte atafanya mabadiliko kwenye baraza lake la mawaziri, akibainisha kuwa mabadiliko hayo ya baraza yatakuwa sehemu ya kuzindua upya sera ya jumla ya serikali.

Kuondoka kwa Otarola, maana yake baraza la mawaziri nalo halipo na Rais Boluarte ana jukumu la kuunda upya baraza lake.

Sauti iliyorushwa na vyombo vya habari inadaiwa sauti ya mwanamke iliyosikika ikizungumza na Otarola ni ya Yaziré Pinedo mwenye umri wa miaka 25.

Pinedo aliripotiwa kupewa kandarasi mbili za kazi katika Wizara ya Ulinzi mwaka 2023 ambazo zilimfanya apate jumla ya Dola 14,000 za Marekani.

Otarola alikuwa Waziri wa Ulinzi wa Peru hadi mwisho wa 2022, wakati Rais Dina Boluarte alipoingia madarakani na alimpandisha cheo kuwa Waziri Mkuu.

Ndani ya sauti hizo Otarola anasikika akitangaza mapenzi yake kwa mwanamke huyo na kumtaka amtumie wasifu wake.

Matamshi hayo yanaonekana kupingana na kauli aliyotoa awali kwamba alikutana na Pinedo mara moja kwenye mkutano na kwamba alikuwa na uhusiano mfupi na mwanamke huyo.

Wakati kashfa hiyo inatolewa kwenye vyombo vya habari, Otarola alikuwa ziarani nchini Canada na Rais Boluarte alimtaka arejee nchini kulikofuatia na tangazo lake la kujizulu.

"Wale ambao wamekuwa wakinitaka nitoke serikalini...hawajasita hata kuhariri sauti iliyofichwa kwa nia ya kuniharibia jina," alisema Otárola katika hotuba yake ya kujiuzulu.

Miongoni mwa aliowashutumu kuwa sehemu ya njama ya kumdhalilisha ni Waziri Mkuu wa zamani, Martín Vizcarra.

Serikali ya Peru sio ngeni kwa misukosuko, Rais Boluarte tangu aingie madarakani amekwishafanya mabadiliko kadhaa ya baraza lake la mawaziri.


Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mashirika.