Waziri Mkuu UK atozwa faini kutofunga mkanda kwenye gari

Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak.

Muktasari:

  • Polisi wa Lancashire wamesema wamempa Sunak adhabu ya kulipa faini isiyobadilika masharti.

London. Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak amepigwa faini kwa kutofunga mkanda kwenye gari lililokuwa likitembea wakati akirekodi video kwa ajili ya mitandao ya kijamii.

Polisi wa Lancashire wamesema kuwa wamempa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 42, adhabu ya kulipa faini isiyobadilika masharti.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Ofisi ya Waziri Mkuu ilieleza kwamba Sunak amekubali kuwa hilo lilikuwa kosa na ameomba radhi na kuongeza kuwa atalipa faini hiyo.

Abiria wanaokutwa hawajafunga kufunga mkanda kwenye gari kwa ajili ya usalama, wanaweza kutozwa faini ya Pauni 100 (takribani Sh289,000).

Hii inaweza kuongezeka hadi Pauni 500 (Sh1.446 milioni) ikiwa kesi itaenda mahakamani.

Waziri Mkuu alikuwa Lancashire wakati video hiyo iliporekodiwa, wakati wa safari kaskazini mwa Uingereza.

Video hiyo ya kutangaza awamu nyingine ya serikali ya kupunguza matumizi, iliwekwa kwenye akaunti ya Instagram ya Sunak.

Ni mara ya pili kwa Sunak kupokea notisi ya adhabu isiyobadilika akiwa serikalini.

Aprili 2022, alitozwa faini pamoja na Boris Johnson na mkewe Carrie kwa kuvunja kanuni za kuzuia Uviko-19 kwa kuhudhuria mkusanyiko wa siku ya kuzaliwa kwa Waziri Mkuu wa wakati huo, huko Downing Street Juni 2020.

Notisi za adhabu zisizobadilika ni adhabu ya kukiuka sheria na inamaanisha faini ambayo inahitaji kulipwa ndani ya siku 28, au kupingwa.

Iwapo mtu atachagua kupinga faini hiyo, basi polisi watapitia kesi hiyo na kuamua kama wataiondoa faini hiyo au kupeleka suala hilo mahakamani.

Chama cha Liberal Democrats kilisema, kwa kuwa Waziri Mkuu wa pili kuwahi kuhudumu kwa kutozwa faini na polisi, “ameonyesha kutozingatia sheria sawa na Boris Johnson”.

Naibu kiongozi wa Lib-Dem, Daisy Cooper amesema: “Kutoka lango la sherehe hadi lango la mkanda wa kiti cha gari, wanasiasa hawa wa Conservative wanawachukulia watu wa Uingereza kama wajinga.

“Wakati wakiendelea kudhani kwamba ni sheria moja kwao na nyingine kwa kila mtu mwingine, faini hii ni ukumbusho kwamba Conservatives hatimaye kupata ujio wao.”

Lakini Mbunge wa chama cha Conservative wa Blackpool South, Scott Benton amemtetea Sunak akisema “kila mtu hufanya makossa.”

Benton amesema polisi wanapaswa kuzingatia “kukabiliana na uhalifu mkubwa katika jamii zetu”, na kuongeza: “Hebu tuweke hili katika uwiano hapa. Kila mwaka mamilioni ya Waingereza hupokea notisi sawa za adhabu zisizobadilika.”

Abiria walio na umri wa miaka 14 na zaidi wana jukumu la kuhakikisha kuwa wamefunga mkanda wa usalama katika magari, vani na magari mengine ya mizigo ikiwa moja itawekwa. Madereva wanawajibika kwa abiria chini ya miaka 14.

Msamaha ni pamoja na kuwa na cheti cha daktari kwa sababu za kimatibabu au kuwa kwenye gari linalotumika kwa polisi, zimamoto au huduma nyingine ya uokoaji.