Ajali pasua kichwa

Dar es Salaam. Ni mwezi wa ajali. Kauli hii inatosha kuelezea namna ajali za barabarani zilivyoshamiri nchini Desemba 2022, ambapo gazeti hili limeripoti ajali nane ndani ya mwezi huu.
Licha ya kutolewa kwa tahadhari mbalimbali kuhusu umakini kwenye matumizi ya barabara, hususan wakati huu wa likizo, bado ‘mzimu’ wa ajali umeendelea kuliandama Taifa na kuendelea kuwa kero.
Pazia la ajali mwezi huu lilifunguliwa Desemba mosi, watu watatu walifariki na wengine 18 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari manne yaliyogongwa kwa nyuma na lori aina ya tipa eneo la Mataa Nyakato jijini Mwanza, baada ya lori hilo kufeli breki. Desemba 7, basi la kampuni ya AN Classic lililokuwa likisafiri kutoka Tabora kuelekea Mbeya lilipata ajali eneo la Makongorosi wilayani Chunya, Mbeya na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine wanne wakijeruhiwa.
Siku sita baadaye, Desemba 13 eneo la Mkata wilayani Handeni mkoani Tanga ajali nyingine ilitokea iliyomhusisha Balozi wa Tanzania nchini Austria, Celestine Mushy ambaye alifariki dunia.
Taarifa ya awali iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Siriel Mchembe ilisema balozi huyo aliyekuwa peke yake kwenye gari aliendesha mwenyewe gari akitokea Dar es Salaam kwenda Moshi, Kilimanjaro, na baada ya ajali gari liliwaka moto akiwa ndani na kuteketea.
Wakati nchi ikiwa kwenye majonzi ya kumpoteza Balozi Mushy, ajali nyingine mbili zilitokea Desemba 19, moja ilihusisha basi la kampuni ya Happy Nation na abiria zaidi ya 50 walinusurika kufa, baada ya basi hilo kuteketea kwa moto mkoani Pwani.
Tukio hilo lilitokea saa nne asubuhi maeneo ya Bonde la Wami ambapo basi hilo lilikuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Arusha.
Ajali nyingine iliyotokea tarehe hiyo ilihusisha basi la kampuni ya Majinja likitokea mkoani Kigoma kwenda Dar es Salaam, ambapo abiria 30 walinusurika kufa baada ya basi hilo kuacha njia na kuanguka eneo la Mbezi Luguruni, Dar es Salaam.
Siku moja baadaye, Desemba 20, watu watatu, wakiwamo wanandoa ambao ni askari polisi Mkoa wa Arusha, Noah Semfukwe (30) na Agnes Kiyeyeu (27) waliripotiwa kufariki katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Tanangozi, nje kidogo ya Manispaa ya Iringa.
Chanzo cha ajali hiyo kilitajwa kuwa ni gari dogo aina ya Vits kugongana na basi la kampuni ya Luwinzo majira ya saa 3.05 asubuhi.
Desemba 28, watu watano walifariki kwa ajali ya gari mkoani Morogoro wakiwamo mume na mke, Grayson Ngogo (50) na Janet Ruvanda (42) ambao walikuwa wanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT). Pia, Grayson, alikuwa Makamu Mkuu wa Chuo cha Ualimu St Agrey na mke wake Janeth akiwa mwalimu wa Shule ya Sekondari Lejiko ya jijini Mbeya.
Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslim alisema ilitokea usiku wa Desemba 26, eneo la Iyovi, wilayani Kilosa, ikihusisha gari dogo aina ya Toyota Allion lililogongana uso kwa uso na gari kubwa la mafuta.
Zikiwa zimesalia siku tatu kabla ya kuumaliza mwaka 2022, ajali nyingine ilitokea mkoani Morogoro ambapo abiria 57 walinusurika kufa baada ya basi la kampuni ya Al Saedy kupinduka wakati dereva wa basi hilo akikwepa kugongana uso kwa uso na basi la kampuni ya Allys, katika eneo la Kitungwa Kingolwira Manispaa ya Morogoro.
Ajali hiyo ilitokea saa 2:40 asubuhi katika barabara kuu ya Pwani-Morogoro na kusababisha abiria 16 kupata majeraha madogo huku kondakta wa basi hilo akipelekwa hospitali ya rufaa ya mkoa huo kwa matibabu zaidi.
Akieleza sababu za kutokea kwa ajali hizo, hususan Desemba, Kamanda Kikosi cha Usalama Barabarani, Ramadhani Ng’anzi alisema madereva wengi hawana uzoefu wa kuendesha magari kwa umbali mrefu, ili kuepuka kadhia hiyo ni vyema wanaosafiri wawakodi madereva wenye uzoefu.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mohammed Kiongozi alisema mwaka huu wamechukua tahadhari kwa kuzungumza na wamiliki pamoja na chama cha madereva.
Kwa upande wa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), Salum Pazi alisema ili kuepukana na ajali, wamekuwa wakitoa elimu pamoja na kuwafanyia usaili madereva kabla ya kujiridhisha kuwa wanaimudu vilivyo kazi hiyo.