Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Apiga magoti kumshukuru JPM, wabunge wa CCM, upinzani wachuana vikali

Muktasari:

  • Ayepiga magoti wakati akichangia hoja hiyo ni Mbunge wa Ileje (CCM), Janeth Mbene kama shukrani zake kwa Rais John Magufuli kwa kupeleka maendeleo katika jimbo lake.

Dodoma. Mbunge kupiga magoti, baadhi yao kuzuiwa kuendelea kuchangia ni miongoni mwa mambo yaliyojitokeza jana katika mjadala wa bajeti ya ofisi ya Rais - Tamisemi na Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora kwa mwaka wa fedha 2018/19.

Ayepiga magoti wakati akichangia hoja hiyo ni Mbunge wa Ileje (CCM), Janeth Mbene kama shukrani zake kwa Rais John Magufuli kwa kupeleka maendeleo katika jimbo lake.

Ili aweze kupiga magoti vizuri, ilimlazimu mbunge huyo kusogea kwenye njia ya kuingilia ya lango kuu la Bunge.

“Napenda kumshukuru Rais Magufuli kwa ahadi zake ambazo anazitekeleza, napenda kumshukuru pia kwa sababu, Ileje ambayo ni wilaya kongwe, imekuwa nyuma kwa miaka mingi sana,” alisema.

“Mimi naomba kwa heshima na taadhima nipige magoti hapa.”

Mbene alisema kuwa anafanya hivyo ingawa magoti yake ni mabovu kama shukrani kwa Rais Magufuli ambaye aliahidi ujenzi wa barabara ya lami ambayo ilipiganiwa kwa zaidi ya miaka miwili.

Mbunge azuiwa kuchangia

Katika tukio jingine, Mwenyekiti wa Bunge, Azzan Zungu alimzuia kuendelea kuchangia Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Upendo Peneza baada ya kuendelea kulitaja jina la Rais wakati wa kuchangia licha ya kukatazwa kufanya hivyo.

Upendo alikuwa akimhusisha Rais na kuzuiwa kwa maandamano nchini na Bunge kuonyeshwa ‘live’.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama aliomba kutoa taarifa ya kukiukwa kwa kanuni akisema Rais anawakilishwa na mawaziri ndani ya Bunge kwa mujibu wa Katiba.

Akitoa majibu ya mwongozo huo, Zungu alisema kuwa jina la Rais halipaswi kutajwa kwa dhihaka, halaumiwi wala hatakiwi kusemwa kama alivyosema mbunge huyo.

Zungu alimtaka mbunge huyo kuuliza utendaji wa mawaziri kwa sababu kanuni inawataka wabunge kutohoji utendaji wa Rais ndani ya Bunge.

“Natumia kanuni ya 73 ukae chini hutazungumza tena,” alisema kisha kumtaja mchangiaji mwingine.

Mjadala ulivyokuwa

Awali, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Martha Mlata aliomba kupelekewa salamu kwa Rais John Magufuli awasaidie kupata upinzani utakaowaletea maendeleo nchini.

“Upinzani unaojitambua, ulio bora, msajili wa vyama vya siasa uwapeleke wapinzani kwenye nchi zenye upinzani wenye mfano ambao mataifa yao yameweza kusimama imara kwa sababu hapa Tanzania bado hatujawa na upinzani ulio imara utakaosaidia Taifa,” alisema.

Mlata alisema nchi haijawa na upinzani imara utakaolisaidia Taifa wa kuwasaidia wanyonge.

Hata hivyo, Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini alimpa taarifa Mlata kuwa Tanzania ina upinzani imara na ndio maana CCM ikawakataza kwenda kwa wananchi kueleza sera zao kwa sababu ya hofu.

Akiendelea kuzungumza, Mlata aliikataa taarifa hiyo akisema kuna upinzani ambao unaenda kuwahadaa wananchi wasifanye kazi za maendeleo.

“Upinzani unaoandamana barabarani, unaomkataa Rais...” alisema na kukatizwa na taarifa kutoka kwa Mbunge wa Tanga Mjini (CUF), Mussa Mbarouk ambaye alisema upinzani ni vyama vya mageuzi na si upinzani. “Upinzani ni huyu anajenga nyumba na huyu anavunja. Sisi ni kioo cha Serikali usitusababishie tukasema mambo mengine huku hali ichafuke,” alisema Mbarouk.

Akiendelea, Mlata alihoji ni upinzani gani ambao hata mambo mazuri unayakataa.

Aliombewa taarifa na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe akitumia kanuni ya 64 inayowaelekeza wabunge kutozungumzia jambo ambalo halipo kwenye mjadala.

Alisema bajeti wanayoijadili ni ya Tamisemi na Menejimenti ya Utumishi wa Umma na kwamba, mahali sahihi kwa hoja za Mlata ilikuwa ni bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na kuomba Mwenyekiti wa Bunge, Zungu kumwelekeza mbunge huyo ajielekeza katika hoja.

Akijibu, Zungu alisema hakuna kanuni yoyote iliyovunjwa na mbunge huyo (Mlata) na kumtaka asibweteke na kutoka kwenye hoja.

Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde aliwataka wabunge wanaohoji utaratibu wa kurejesha mali za CCM warudi katika chama hicho ili waweze kufaidi mali ambazo walichangia wakiwa wanachama.

“Hata katika michango ya harusi huingii chumbani kwa sababu umechangia, unaishia mlangoni tu,” alisema.

Lusinde aliwataka wabunge wa upinzani kutoa boriti katika jicho lao kabla ya kutoa kibanzi kilichopo kwenye Serikali ya CCM akimaanisha kabla ya kuikosoa Serikali wajisahihishe wao kwanza.

Alisema katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Chadema imechukua mkopo wa Sh2 bilioni kutoka kwa mwanachama lakini hakuna uthibitisho wa kupokewa ndani ya chama.

Alisema pia kuna Sh866 milioni zililipwa kwa mwanachama kwa ajili ya mabango ya matangazo nje ya deni bila nyaraka .

“Wajinga ndio waliwao, mnang’ang’ania maandamano huku mnapigwa,” alisema na kuendelea kutaja upungufu mwingine uliotajwa na CAG katika ripoti yake.

Maneno hayo yaliwafanya baadhi ya wabunge wa upinzani kutaka kuomba kutoa taarifa, lakini Zungu aliwakatalia.