Askofu Shoo akemea dhuluma, ataka masilahi ya walimu, madaktari kuangaliwa upya

Muktasari:

  • Asema wenye mamlaka na madaraka wanapochukua mishahara na masilahi yao wawakumbuke watumishi hao.

Moshi. Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo ametumia sikukuu ya Pasaka kuwakumbusha wenye mamlaka na madaraka nchini, kujitoa kwa ajili ya wengine na kuepuka dhuluma na ubinafsi.

 Dk Shoo amesema hayo leo, Jumapili Machi 31, 2024, alipohubiri kwenye Usharika wa Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro, akigusia masilahi ya wabunge, walimu, madaktari na wauguzi.

Amesema kumekuwapo habari za rushwa, dhuluma na ubinafsi hasa miongoni mwa waliopewa mamlaka na madaraka na kutoa wito kwa wote wenye nafasi kujitoa kwa ajili ya watu ambao Mungu amewapa kuwaongoza na kuwatawala.

“Tunasikia habari za rushwa, habari za dhuluma na habari za ubinafsi, hasa miongoni mwa waliopewa mamlaka na madaraka; viongozi wa kanisa wanaojiita watumishi, vyama vya siasa, wabunge na hata viongozi wa Serikali, habari hizi zinasikika,” amesema na kuongeza:

“Leo tunapewa wito, tuwe na roho ya kuwajali watu, tusitazame mambo yetu wenyewe, tujifunze kwa Yesu, tujitoe kwa ajili ya watu ambao Mungu ametupa kuwaongoza au kuwatawala.”

DK Shoo amesema, “Si jambo la kufurahisha hata kidogo, inafika mahali hata Rais mwenyewe anazungumza kwamba kuna upigaji wa kutisha, tena anasema kuna mfumo ndani ya Serikali, watu wameweka mitandao yao ya kupiga maana yake kuiba mali ya Watanzania ambayo ingetumika kwa ajili ya maendeleo ya umma.

“Msiwe wabinafsi kupindukia, msitumie nafasi zenu kujilimbikizia mali nyingi kwa gharama ya Taifa zima na mahali pengine hata kwa gharama ya maisha ya watu walio wanyonge wa nchi hii,” amesema.

Dk Shoo amesema, “Ndugu zangu utii huu wa Yesu, kujinyenyekesha kwake, upendo wake wa kujitoa kwa ajili ya wengine, iwe funzo kwetu, tukaige mfano huu wa Yesu, tuwe wanyenyekevu, watiifu na wenye upendo kwa wengine.” 

Masilahi ya walimu, madaktari na wauguzi

Dk Shoo ambaye ni Mkuu wa KKKT mstaafu, amesema katika kuiga mfano wa Yesu wa kujitoa kwa ajili ya wengine, ni vyema wale wenye mamlaka na madaraka wanapochukua mishahara na masilahi yao kuwakumbuka walimu, madaktari na wauguzi ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.

Amesema wanatambua jitihada za Serikali katika kujenga shule, hospitali na hata vituo vya afya na kumekuwa na hatua kubwa, lakini amesema hiyo haitatosha kama hayataangaliwa masilahi ya walimu, madaktari na wauguzi.

 “Sijasikia sana wabunge wetu wakitetea mambo ya walimu, kwamba walimu jamani waongezewe mishahara na nini, hawa wanatoa mchango mkubwa kwa ujenzi wa Taifa letu, wanawaangalia watoto wetu ndugu zangu,” amesema.

“Sijui kama wabunge hawajisikii vibaya wakati wao mishahara yao ni Sh13 milioni kwa mwezi, sina neno nao wanaweza kupata hata Sh20 milioni. Mawaziri ndiyo usiseme ilihali mwalimu mwenye digrii amesota shuleni, chuoni anakwenda nyumbani na Sh650,000, mwalimu wa diploma Sh430,000 ndiyo anakwenda nayo nyumbani wewe mshahara wa Sh13 milioni na bado unaona hautoshi. Daktari wa digrii Sh1 milioni kijana anaanza maisha,” amesema.

“Nasema haya ndugu zangu ili tuone jinsi ambavyo ubinafsi uliokithiri unavyoweza kudidimiza sekta muhimu ya afya, elimu kwa kutokuwajali wale wanaohenyeka usiku na mchana. Biblia inatuambia kila mtu asiangalie mambo yake binafsi tu, bali ayaangalie na ya wengine,” amesema Askofu Shoo.

Amesema, “Tutoke hapa na ujumbe huu, kwa kuwa Yesu Kristo amejitoa kwa ajili yetu, ametushindia, basi hata ule ubinafsi unaokufanya ukatae kuwapa wengine haki yao na usiwathamini ile roho iondoke.”

Amesema wenye mamlaka wanapaswa kukumbuka kujitoa kwa ajili ya ambao wanatumika na kutumikia Taifa, hatua itakayosaidia kuleta maendeleo ya kweli, akieleza walimu wakikata tamaa ni hatari kwa Taifa.

“Kwa kweli niwasifu walimu wengi wanajitolea sana, juzi nimepokea taarifa shule moja huku Kilimanjaro ina watoto 450, walimu watano, sasa walimu wakiigia darasa la kwanza hadi la saba, madarasa mawili yatabaki na bado kuna la awali, halafu tunatarajia kujenga elimu bora,” amehoji.

“Naomba wahusika waangalie hili, kwani wapo wengine wanazunguka wamemaliza vyuo hawajapata kazi, yapo maeneo mengine wazazi wanaamua kujichanga kulipa walimu wa ziada, kwa maeneo ya vijijini hali ni mbaya,” amesema.

Askofu Shoo amesema, “Tujiulize shule za binafsi zinaongezeka inaashiria nini, ni kwamba wazazi wana hela wanataka kupeleka watoto wao private (shule binafsi). Tutafakari ni kiasi gani tunajitoa na ni kiasi gani viongozi wetu wanaonyesha upendo na kujitoa kwa wale wanaotoa elimu kwa watu wetu na wale wanaotibu.”


Ukandamizaji, mauaji

Dk Shoo pia ameitaka jamii kukataa roho za kikatili, mauaji ya watu wasio na hatia, mifumo ya ukandamizaji na mamlaka zisizotenda haki.

“Kaburi tupu ni alama ya matumaini na kuwa na tumaini haina maana kuwa kimya, alikubali mateso na kifo ili tumaini tulilonalo liwe uvuvio unaotufanya tuheshimu sana na kuulinda uhai wa kila kiumbe, tulinde uhai wa binadamu wenzetu lakini pia viumbe wengine wote.”

Amesema, “Kristo mfufuka anatupa nguvu na sababu ya kukataa na kupinga mauaji, ukatili, mifumo yote kandamizi na mamaka zozote zisizotenda haki.”

“Kuna mifumo duniani inaleta vifo. Kusababisha vifo, maumivu na ukatili, unaleta uharibifu na uonevu kama tunavyoshuhudia sasa, ni kama mifumo hii imekataa uhai, inakataa uzima kwa wengine,” amesema na kuongeza:

“Mungu wa uhai, Mungu wa uzima anayetaka haki na amani za dunia hii amesema kifo hakitanishinda yeye anataka haki na amani kwa dunia, sisi sote tuwe na uzima.”

Katika ibada hiyo iliyoongozwa na Mchungaji James Nkya, baadhi ya waumini waliohudhuria wamesema Pasaka ina maana kubwa kwa Wakristo na wanapaswa kuitumia kutenda mema na haki kwenye jamii.

"Hii ni sikukuu kubwa kwetu Wakristo, tunakumbuka kufufuka kwa Yesu Kristo, mkombozi wetu, siku hii tunakumbushwa kutenda mema, haki na kuwajali wengine, hata katika kusherehekea kwenye familia zetu, tuwatazame wenzetu ambao hawajajaliwa chochote," amesema Esther Hiza.