Awamu ya kwanza waliopata mikopo ya elimu ya juu yatangazwa

Muktasari:

  • Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) nchini Tanzania imetangaza orodha ya awamu ya kwanza ya wanafunzi wa elimu ya juu waliopata mikopo huku awamu nyingine ikitarajiwa kutangazwa Alhamisi Oktoba 21, 2021.

Dodoma. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha ya awamu ya kwanza yenye wanafunzi 37,731 wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo yenye thamani ya Sh99.9 bilioni kwa mwaka wa masomo 2021/2022 unaotarajiwa kuanzia wiki ijayo.


Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema hayo leo Jumapili Oktoba 17, 2021 ambapo amesema kuwa kati ya wanafunzi hao, wanaume ni 23,379 sawa na asilimia 62 na wanawake ni 14,352 sawa na asilimia 38.


Badru ameongeza kuwa HESLB imeanza kupeleka fedha za wanafunzi waliopangiwa mikopo katika vyuo mbalimbali.


Amewataka wanafunzi kupata taarifa za kina katika akaunti walizotumia kuomba mkopo maarufu kama SIPA (Student’s Individual Permanent Account) na kujiandaa kwenda vyuoni kwa ajili ya kujisajili.


“Serikali imeshatupatia fedha na tumeanza kuzipeleka vyuoni … Lengo letu ni kuhakikisha wanafunzi wanaopangiwa wanazikuta fedha vyuoni ambako watajisajili na kupokea ili watimize ndoto zao,” amesema Badru.


Amesema orodha ya awamu ya pili imepangwa kutolewa Alhamisi, Oktoba 21, 2021 baada ya kukamilisha uchambuzi wa maombi unaoendelea na kuwataka waombaji mikopo kutembelea akaunti zao ya SIPA kupata taarifa kuhusu maombi yao.


“Orodha hii ya kwanza inajumuisha wanafunzi wenye sifa zikiwemo kuwa wahitaji, wameomba kwa usahihi na wana udahili wa chuo kimoja … tunakamilisha uchambuzi wa maombi mengine na tutaoa orodha ya pili Alhamis, Oktoba 21, 2021,” amesema Badru.


Sh570 bilioni zimetengwa kwa mikopo ya elimu ya juu 2021/2022 kwa ajili ya mikopo ya jumla ya wanafunzi 160,000. Kati yao, wanafunzi 70,000 watakuwa ni wanufaika wapya na wanafunzi zaidi ya 90,000 ni wale wanaoendelea na masomo baada ya kufaulu mitihani yao ya mwaka.  


Badru amesema HESLB imeshapokea fedha kwa ajili ya malipo ya wanafunzi na taratibu za malipo zimeanza ili fedha hizo ziwe zimefika vyuoni kuanzia Jumanne, Oktoba 19, 2021.