Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chanzo ajali zinazohusisha kemikali chatajwa

Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti GCLA, Daniel Ndiyo.

Muktasari:

 Ofisi ya Kanda ya Kati-Dodoma ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imetoa elimu usimamizi salama wa kemikali kwa wafanyabiashara 80 wa kemikali na kutaja nne za ajali zinazohusisha kemikali

Dodoma. Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), kupitia Ofisi ya Kanda ya Kati-Dodoma, imetaja sababu nne za ajali zinazohusisha kemikali nchini, ikiwamo kutozingatia matakwa ya sheria ya usimamizi na udhibiti wa bidhaa hiyo.

Sababu nyingine ni uelewa mdogo kuhusu kemikali, kutokuwa na mafunzo juu ya usimamizi na usafirishaji salama wa kemikali na baadhi ya wafanyabiashara wa kemikali kutosajiliwa na GCLA.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti GCLA, Daniel Ndiyo jijini Dodoma leo Januari 27, 2024 alipokuwa akifungua mafunzo kwa wasimamizi wa kemikali kwa lengo la kuhakikisha, wanasimamia vyema shughuli zinazohusisha kemikali kwenye maeneo yao ya kazi.

“Mafunzo haya yatawajengea uwezo wasimamizi wa kemikali kufahamu madhara na faida ya kemikali na wote wanatakiwa kufahamu  namna sahihi ya kutumia kemikali na kushughulikia kemikali-taka zinazozalishwa.

“Kwa sababu ajali za kemikali hutokana na sababu kadhaa, ikiwamo ya uelewa mdogo wa sheria za nchi na ufinyu wa rasilimali watu, hivyo kuchangia matumizi ya kemikali yasiyo sahihi na udhibiti hafifu wa kemikali taka,” amesema Ndiyo.


Amesema dhumuni la kutoa mafunzo hayo ni kutokana na matakwa ya Sheria ya Kemikali ya Viwandani na Majumbani Sura 182.

Ndiyo  amesema sheria hiyo inataka wadau wote wanaojishughulisha na kemikali kuwa na uelewa wa matumizi sahihi na salama ya kemikali.

"Matumizi ya kemikali huzalisha kemikali taka zinazoweza kuleta madhara kwa afya na mazingira zisipodhibitiwa, hivyo mafunzo haya ni muhimu katika kujenga uelewa wa kujihusisha na kemikali pamoja na kuzuia ajali zinazoweza kutokea kutokana na matumizi yasiyo sahihi na salama ya kemikali,” amesema Ndiyo.

Meneja wa Ofisi ya Kanda ya Kati – Dodoma, Gerald Meliyo, ametoa rai kwa wasimamizi wa kemikali kuhakikisha wanakuwa kwenye nafasi chanya ya kuwaelimisha wafanyakazi waliopo chini yao kuhusu matumizi sahihi ya kemikali.

Pia, amewasisitiza kuhamasisha wadau wengine kupata mafunzo na kueneza elimu ya matumizi salama ya kemikali kwenye maeneo yao ya kazi na nje ili kulinda afya za watu, wanyama na mazingira.

Mshiriki wa mafunzo hayo, Mhandisi Aron Mwaigaga ameishauri mamlaka hiyo kuendelea kutoa elimu kwa wadau na wananchi.

Mafunzo hayo ya usimamizi salama wa kemikali yanahusisha washiriki zaidi ya 80 kutoka mikoa ya Iringa, Tabora, Singida, Dodoma na Morogoro yakifanyika Dodoma.