Fisi aliyeripotiwa kuua, kujeruhi saba Lindi auawa

Muktasari:

  • Askari wa Tawa wamefanikiwa kumuua fisi aloyesababisha vifo vya watu wawili na kujeruhi watano mkoani Lindi baada ya kuwavamia.

Morogoro. Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imefanikiwa kumuua fisi aliyeua watu wawili na kujeruhi watano katika Wilaya ya Lindi Mkoani Lindi.

 Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kusini Mashariki, Abraham Jullu amesema hayo Leo Jumamosi Mei 13,2023 alipozungumzia na Mwananchi Digital ambapo ameeleza kuwa Mei 11,2023 Saa 12.00 asubuhi ofisi yake ilipokea simu kutoka kwa Mtendaji Kata ya Milola akitoa taarifa kuwa fisi amejeruhi watu watatu katika Kijiji cha Rutamba, watu wawili Kijiji Cha Ng'apa na kusababisha vifo vya watu wawili.

Jullu amesema baada ya kupokea taarifa hiyo mara moja alituma kikosi cha Askari wapatao watano kwa ajili ya kumsaka fisi huyo ambapo baada ya msako mkali majira ya mchana askari hao walifanikiwa kumuona na kumuua.

Amewataja waliofariki na  wametambulika kuwa ni Abilahi Pokosoi (50), na Saidi Makolela (75) huku waliojeruhiwa na fisi huyo kuwa ni Suleman Mtambo, Hadija Said, Alpha Ibrahimu, Maria Sabuni na mwingine aliyetambulika Kwa jina moja la Steven ambao wote walipelekwa katika Hospitali ya Sokoine Mkoani Lindi.


Aidha, Kamanda Jullu amesema taratibu za kuwasaka fisi wengine katika maeneo mbalimbali ikiwemo Milola na Vijiji vya Wilaya ya Ruangwa zinaendelea na kuona namna bora ya kuwahamisha na kuwapeleka maeneo ya hifadhi.

"Kama Mamlaka tunatoa pole kwa majeruhi na familia za waliofariki kuhusiana na tukio hili na niwatake wananchi wote kutoa taarifa mapema pale wanapoona wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo yao ili kuwawezesha askari kuchukua hatua za kuwadhibiti mapema kabla hawajasababisha madhara kwa maisha ya watu na mali zao." amesema.

Aidha wananchi wanasisitizwa kuchukua tahadhari ikiwemo kuepuka kutembea nyakati za alfajiri na usiku, na kutofanya shughuli za kibinadamu kama vile kilimo na ufugaji pembezoni mwa hifadhi na maeneo ya mapito (Shoroba) ya wanyamapori.

Afisa Habari Kitengo cha Uhusiano kwa Umma Tawa, Beatus Maganja amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi ya namna ya kuchukua tahafhali wakati wote  hususani wale wanaoishi pembezoni mwa hifadhi