Polisi wamuua fisi aliyejeruhi watu 10, wamo watano familia moja

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limefanikiwa kumuua fisi aliyewajeruhi watu 10 wakiwemo watano wa familia moja katika Kijiji cha Nyamarimbe, Wilaya ya Geita Machi 29, 2023.

Geita. Watu 10 wamenusurika kufa baada ya kujeruhiwa maeneo mbalimbali ya miili yao na fisi katika Kijiji cha Nyamarimbe, Tarafa ya Busanda wilayani Geita.

Tukio hilo lililotokea Machi 29, 2023 majira ya jioni kijijini hapo ambapo kati ya majeruhi watano ni wa familia moja ambao ni mama na watoto wake watatu pamoja na kaka yake.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Berthaneema Mlay amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema watu wanne walipata huduma ya kwanza na kuruhusiwa na wengine sita wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Geita kwa matibabu zaidi.

Amesema kabla fisi huyo hajawajeruhi aliwakimbiza watoto wawili waliokuwa wakichunga mifugo na alipowakosa aliua ng’ombe mmoja na baada ya taarifa za fisi kusambaa, wananchi walianza kukusanyika. Fisi huyo aliposikia kelele za sauti za watu, alitoka vichakani na kuwavamia na kila aliyefika kwa ajili ya kuokoa alijeruhiwa.

Alisema polisi walifanikiwa kumuua fisi kwa kumpiga risasi tatu na kusema eneo lile ni eneo la vichaka na kuwataka wananchi wanapokuwa shambani wawe zaidi ya mmoja ili kunusuru maisha pindi anapotokea mnyama mkali.

“Tunatoa wito kwa kwa wananchi waendelee kuchukua tahadhari wanapokuwa mashambani, na asiwe mmoja, kati yao angalau wawe wawili, watatu, ili kuweza kunusuru maisha yao anapotokea mnyama mkali,” amesema.

Akizungumzia hali ya majeruhi Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita, Dk Mfaume Kibwana amesema majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo walikuwa na majeraha madogomadogo kwenye mikono na miguu.

Mmoja wa majeruhi hao maneno Petro (35) amesema alishambuliwa na fisi huyo wakati wakimsaka kwa lengo la kumuua baada ya kuwakimbiza watoto na kuua ngombe mjamzito kisha kuondoka na ndama aliyekuwa bado hajazaliwa.