Hivi ndivyo Tehama itakavyopunguza uhaba wa walimu nchini

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa akizungumza wakati wa kuzindua kituo cha ufundishaji mbadala katika Shule ya Sekondari Dodoma leo Februari 7, 2024. Picha na Rachel Chibwete

Muktasari:

  • Waziri wa Tamisemi, Mohammed Mchengerwa amezindua kituo cha ufundishaji mbadala kilichopo katika Shule ya Sekondari Dodoma, kikiwa sehemu ya juhudi za Serikali kupunguza uhaba wa walimu.

Dodoma. Serikali imesema kuanzishwa vituo vinavyofundisha kwa kutumia njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kutasaidia kupunguza uhaba wa walimu nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Jumatano Februari 7, 2024 alipozindua kituo cha ufundishaji mbadala kilichopo katika Shule ya Sekondari Dodoma.

Ufundishaji wa majaribio kupitia Tehama pia umeshafanyika katika Shule ya Sekondari Kibaha mkoani Pwani.

Kituo hicho kitafungwa kamera mbili nyuma na mbele ya darasa husika, pia kitakuwa na vinasa sauti, na vipaza sauti ambavyo vitamwezesha mwalimu aliye kituo kimoja kuwasiliana na wanafunzi waliopo darasa lingine lililofungwa vifaa hivyo kwa kutumia sauti na video.

Kupitia vifaa hivyo, watakuwa wanaonana na kusikilizana kama vile wapo pamoja.

Pia kutakuwa na skrini kubwa itakayomwezesha mwalimu kufundisha kwa kutumia vitabu na michoro iliyopo kwenye mtandao wa Google na Youtube, hivyo kumwezesha mwanafunzi kuelewa zaidi kwa kutumia picha na video zinazohusu somo husika.

Kutokana na mwalimu kuwaona wanafunzi anaowafundisha mahali walipo kwa kupitia skrini iliyopo darasani, anaweza kuuliza maswali na kupata majibu kutoka kwa wanafunzi anaowafundisha kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Waziri Mchengerwa amesema bado kuna uhaba mkubwa wa walimu 271,028 kuanzia ngazi ya awali, msingi hadi sekondari, hivyo kupitia vituo hivyo walimu wa masomo husika watakuwa wanafundisha wanafunzi kwenye shule ambazo zina upungufu wa walimu wa masomo hayo.

Amesema kuna wakati alianza kuwatoa walimu kwenye maeneo yenye idadi kubwa na kuwahamishia yenye idadi ndogo, lakini pamoja na hilo bado kumeonekana kuna uhaba mkubwa wa walimu, hivyo kupitia vituo hivyo wataweza kupuunguza.

“Mwalimu mmoja ataweza kufundisha wanafunzi wengi zaidi kutoka kwenye maeneo yenye uhaba wa walimu,” amesema Mchengerwa.

Ameagiza mikoa yote nchini kuwa na kituo kimoja cha kufundishia wanafunzi kwa kutumia Tehama.

Pia ameagiza wakurugenzi wa halmashauri kutenga fedha kununua vifaa vya Tehama kwenye bajeti za mwaka wa fedha 2024/25 ili kufanikisha ufundishaji mbadala kwa nchi nzima ifikapo Desemba 2025.

Mbali ya hayo, Mchengewa amewataka walimu wote wanaosoma shahada na astashahada katika elimu kujifunza namna ya kutumia teknolojia hiyo ili kuendesha vituo hivyo kwa umahiri na kuleta mafanikio chanya.

Naibu Katibu Mkuu Tamisemi, Dk Charles Msonde amesema teknolojia hiyo haitaondoa ajira za walimu kwani Serikali bado inaendelea kuwaajiri na kuwapeleka kwenye shule mbalimbali zenye uhaba wa walimu nchini.

Dk Msonde amesema uhaba wa walimu unachangiwa na ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na shule baada ya Serikali kuanza kutoa elimu bila ada.

Amesema mpaka sasa kuna ongezeko la wanafunzi milioni 3.4.

Kutokana na ongezeko hilo, amesema ni lazima uhaba wa walimu ujitokeze na ndiyo maana Serikali inaendelea kubuni njia za kupunguza uhaba huo kwa kuweka teknolojia za kufundishia wanafunzi wengi kwa wakati mmoja.

Mwalimu wa jiografia kutoka Shule ya Sekondari ya Dodoma, Pendo Kaijage amesema teknolojia hiyo ni nzuri kwa kuwa itamwezesha mwalimu kufundisha bila kuchoka kwani atafundisha wanafunzi wa mikondo yote kwa wakati mmoja.

Pendo amesema kuna wakati walimu huwa wanachoka kufundisha kutokana na mikondo kuwa mingi, lakini kwa kutumia teknolojia atafundisha wote kwa wakati mmoja, hivyo itawapunguzia uchovu.

Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Dodoma, Jesca Lauden amesema teknolojia hiyo ni nzuri kwani leo wamejifunza jiografia kupitia mwalimu wa somo hilo aliye Shule ya Sekondari Kibaha na wamemwelewa kwani walikuwa wanaonana na kuwasiliana vizuri.

Amesema wamevutiwa na ufundishaji wa aina hiyo, hivyo kama utaratibu huo wa kufundisha ukiendelea utasaidia kupunguza utoro shuleni kwa sababu njia wanayotumia kusoma inawavutia wanafunzi wengi.


Ilivyokuwa Kibaha

Majaribio ya ufundishaji huo Jumatatu wiki hii yalifanyika katika Shule ya Sekondari Kibaha mkoani Pwani, ambako wanafunzi wamesema utawasaidia kupata uelewa kwa wepesi na kufanya vizuri kwenye mitihani ya kitaifa.

Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wamesema ufundishaji kwa kutumia Tehama unawawezeha kuokoa muda, hivyo kukamilisha mada kwa wakati.

"Ni teknolojia nzuri na huenda ukawa mwarobaini wa kukabiliana na uhaba wa walimu hasa wa masomo ya sayansi, maana mwalimu anatumia muda mfupi kuwafikia wanafunzi wengi kwa wakati mmoja, anaweza akawa Pwani akafundisha wanafunzi kutoka alipo na mikoa zaidi ya miwili hivyo utakuwa mkombozi," amesema mwanafunzi wa kidato cha nne shuleni hapo, Elihuruma Thomas.

Kwa upande wake, Zaharuki Hamisi amesema utaratibu huo utakapoanza kikamiifu, utaleta faraja kwa wanafunzi kwa kuwa watakuwa wanakamilisha mada za masomo mapema na kuanza marudio, hivyo kuwawezesha kufanya vizuri kwenye mitihani ya Taifa.

"Maana kama shule ina mikondo mitatu ya darasa moja, mwalimu hatalazimika kuingia kila chumba, anachofanya ni kukaaa chumba kimoja cha darasa anapofundisha wanafunzi wote wanafikiwa kwa muda uleule na masomo yaleyale," amesema.

Mkufunzi wa ujuzi wa namna ya kutumia mfumo huo kwa walimu, Jackson Mhoro ambaye ni mtaalamu wa Tehama kutoka Shirika la Elimu Kibaha, amesema mpaka sasa walimu wanne kutoka shule hiyo wameshapata ujuzi huo, huku wengine wakiendelea kunolewa, lengo likiwa kuwafikia wote.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Kibaha, George Kazi amesema ili kwenda na wakati juu ya matumizi ya mfumo huo wameandaa maudhui ya masomo ambayo hivi sasa yako kwenye hatua ya kufanyiwa maboresho.

Ofisa elimu mkoa wa Pwani, Sara Mlaki amesema matumizi ya mfumo huo yatarahisisha ufundishaji na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.

Amesema hatua inayofuata ni kuboresha miundombinu ya madarasa ili iendane na ufundishaji kwa njia ya Tehama.