ILO yatoa wito kwa wafanyakazi kutumia fursa ya uchumi Tanzania
Muktasari:
Shirika la Kazi Duniani (ILO) limevitaka vyama vya wafanyakazi na waajiri kutumia fursa ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania kama sehemu ya kuimarisha ulimwengu wa kazi wenye usawa.
Dar es Salaam. Shirika la Kazi Duniani (ILO) limevitaka vyama vya wafanyakazi na waajiri kutumia fursa ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania kama sehemu ya kuimarisha ulimwengu wa kazi wenye usawa.
ILO imesema ni miaka mitatu tangu dunia ikumbwe na janga la Uviko-19 lililosababisha madhara mbalimbali, ikiwemo mdodoro wa uchumi kwa baadhi ya mataifa lakini Serikali ya Tanzania, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imehakikisha uchumi unakuwa imara.
Kwa mujibu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), uchumi wa Tanzania kwa mwaka 2022 ulikuwa kwa asilimia 4.7, lakini makadirio ni kufikia asilimia kati ya 5.2 hadi 6.2 ndani ya mwaka huu.
“Tunatoa wito kwa Serikali, vyama vya wafanyakazi na wadau wengine kuchukua ukuaji wa uchumi, kama fursa ya kuimarisha ulimwengu wa kazi ulio imara zaidi utakaoipa kipaumbele zaidi jamii.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa utawala unaotoa fursa za kijamii, kama afya na elimu zinazopelekwa karibu na wananchi. Lakini njia mwafaka ni kutengeneza na kukuza nafasi za ajira na kazi zenye staha kwa wote,” amesema Jealous Chirove ambaye ni mwakilishi wa ILO Kanda ya Mashariki.
Chirove ameeleza hayo leo Jumatatu Mei Mosi, 2023 katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani inayoadhimishwa kitaifa katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro. Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Rais Samia pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Serikali.
Chirove amesema ni wajibu kuimarisha taasisi na masharika ya wafanyakazi kwa kuzipitia na kurekebisha sheria na kanuni zinazohusu kazi na ajira ili kukidhi mahitaji ya sasa na kukuza biashara.