Ndalichako asisitiza mahusiano mazuri mahala pa kazi

Muktasari:
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako amesema wizara hiyo itaendelea kuimarisha mahusiano mazuri mahala pa kazi, kwani Serikali inaamini huchangia kufanikisha malengo na kuchochea ufanisi.
Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako amesema wizara hiyo itaendelea kuimarisha mahusiano mazuri mahala pa kazi, kwani Serikali inaamini huchangia kufanikisha malengo na kuchochea ufanisi.
Ndalichako ameyasema hayo leo Jumatatu Mei Mosi, 2023 wakati akitoa hotuba mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi kitaifa (Mei Mosi) ambayo kitaifa inafanyika mjini Morogoro.
Ndalichako ambaye ni Mbunge wa Kasulu Mjini amemwahidi Rais kuwa wizara yake itaendelea kufanya kazi katika utatu kwa kushirikiana na Tucta, Shirika la Kazi Duniani (ILO) ili kuhakikisha hilo linafanikiwa.
“Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi na Ajira itaendelea kuimarisha utatu kuhakikisha tunafanya kazi kwa ukaribu na shirikisho la vyama vya wafanyakazi na tutaendelea kushirikiana na ILO ili kuimarisha mahusiano mazuri mahala pa kazi.
“Tunaamini kwamba kunapokuwa na mahusiano mazuri mahala pa kazi inaleta ari ya watumishi kujituma na hivyo kufanikisha malengo na kuchochea ufanisi,” amesema Waziri Ndalichako.
Aidha amemshukuru Rais kwa kuwathamini wafanyakazi na kuongeza ajira mpya, “Nikupongeze mambo makubwa uliyoyafanya tumeshuhudia wakipandishwa madaraja, wakipata nyongeza wa mshahara, ubadilishaji wa miundo umefanya mengi kwa kipindi chako bila kusahau kuongeza ajira mpya,” amesema.
Aprili 26 mwaka huu, Ndalichako amesema kupitia Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (Osha) Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji kazi nchini.
Ndalichako amesema Serikali inaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Sheria namba tano ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 miongoni mwa wadau na Watanzania wote kwa ujumla.