Jaji Kiongozi ataka maofisa wa Mahakama kuchukuliwa hatua

Jaji Kiongozi, Mustafa Siyani akizungumza na majaji wafawidhi wa Mahakama Kuu

Muktasari:

Mafunzo ya majaji wafawidhi wa Mahakama Kuu yamehitimishwa,  huku Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mustafa Siyani akiwataka kwenda kusimamia nidhamu kwa maofisa wa Mahakama ikiwemo kuwachukulia hatua wanaobainika kukiuka.

Arusha. Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mustafa Siyani amesema upo umuhimu mkubwa wa maofisa wa Mahakama kuchukuliwa hatua za kinidhamu wanapokiuka maadili ya kazi zao.

Amesema lengo ni kuongeza na kudumisha uwajibikaji katika mnyororo wa utoaji haki kwa wananchi unaozingatia maadili, lakini pia kujenga imani kwa umma juu ya chombo hicho kilichokasimiwa majukumu ya utoaji haki.

Kufuatia hili, amewataka majaji wafawidhi wa Mahakama Kuu,  kusimamia suala la maadili na uadilifu kwa watendaji walioko chini yao pindi wanapotekeleza majukumu yao ya kazi.

Jaji Siyani ameyasema hayo jana, Machi 1,2024  jijini Arusha wakati akifunga mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo majaji wafawidhi wa Mahakama Kuu nchini, kwa ajili ya kwenda kuwa wakufunzi wa kamati za maadili za maofisa wa mahakama za mikoa na wilaya.

Mbali na kuwajibishwa, Jaji Siyani amesema upo umuhimu pia wa umma kusikia juu ya hatua hizo za kinidhamu zinazochukuliwa, ili kupunguza malalamiko ya ukosefu wa maadili kwa maofisa hao wa Mahakama wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

“Mara kadhaa kumekuwa na malalamiko ya ukosefu wa maadili mahakamani bila kujali ukweli ama usahihi wa malalamiko hayo, lakini yanaondoa imani kwa jamii juu ya chombo hicho kilichokasimiwa majukumu ya utoaji haki,” amesema Jaji Siyani.

Amesema ili chombo hicho kiheshimike na kuaminiwa, ni lazima maofisa wake wawe na viwango vinavyokubalika vya uadilifu.

“Kwa sababu ya umuhimu huu, kamati za maadili zilianzishwa ili kuhakikisha maofisa wa Mahakama wanatimiza majukumu yao kwa uadilifu na kutengeneza mazingira ya kuaminika na jamii, hivyo basi majaji wafawidhi nendeni mkayasimamie haya yatekelezeke,” amesema Jaji Siyani


Awali, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, Joachim Tiganga amesema mafunzo hayo yamekuja wakati mwafaka kwao na kuahidi kwenda kuyasimamia utekelezaji wake ulete tija katika chombo hicho.

“Tunaahidi kwenda kusimamia kamati hizi na watendaji wetu pia kuhakikisha suala la maadili na uadilifu linachukua nafasi yake katika utekelezaji wa majukumu yetu yote,” amesema

Awali, akizungumza na waandishi wa habari, Mtendaji Mkuu wa Mahakama nchini, Profesa Elisante Ole Gabriel amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo majaji wafawidhi ili wakatoe mafunzo hayo kwa vingozi na wajumbe wa kamati za maadili za maofisa wa mahakama wa wilaya na mikoa nchini.