‘Jamii iwawezeshe kiuchumi wanawake’
Muktasari:
- Imeelezwa kuwa wanawake ndio wazalishaji wakuu hivyo jamii inatakiwa kuwezeshwa kiuchumi waepuke changamoto zinazowakabili.
Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa wanawake ndio wazalishaji wakuu hivyo jamii inatakiwa kuwezeshwa kiuchumi waepuke changamoto zinazowakabili.
Hayo yameelezwa na katibu mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Doto James wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake wajasiriamali nchini nzima ulioandaliwa na Mfuko wa Fursa kwa Wote (EOTF).
James amesema endapo wanawake hawatawezeshwa kiuchumi watakumbwa na changamoto za kukosa haki, unyanyasaji, kuwapunguzia ajira na kipato pamoja na kuwa na idadi kubwa ya wanawake wanaoishi katika umasikini.
“Jukumu la kuhakikisha kuwa wanawake wajasiriamali wanakuwa katika uchumi wa viwanda na kupata haki zao za msingi ni la jamii nzima hivyo kila mmoja wetu anapaswa kutimiza hilo kwa kuhakikisha wanawake wanashiriki katika michakato ya shughuli za maendeleo na kuleta maendeleo chanya,” amesema.
Amebainisha kuwa hatua hiyo italeta maendeleo chanya kwa wananchi katika sekta za kiuchumi na kijamii sambamba na kudumisha amani na haki ya usawa kwa kila binadamu bila kujali tofauti zao na hilo linawezekana kwa kila mmoja kutimiza wajibu.
Mwenyekiti wa EOTF, Anna Mkapa amesema wanawake ndio waliobeba uchumi wa viwanda katika nchi, ni wazalishaji wakubwa wa malighafi za aina zote za viwanda, watengenezaji ajira na wapiganaji wa umasikini, ujinga na maradhi katika taifa.
“Historia inatuambia mafanikio yoyote yale ya kiuchumi, kielimu na kijamii yanatokana na mwanamke, kwa Tanzania asilimia 53 ya wakazi ni wanawake na ndiyo tegemeo la uzalishaji wa mazao, uvuvi na ujasiriamali,” amesema Mama Mkapa.
Meneja mwandamizi wa bidhaa wa benki ya CRDB huduma za benki kwa wanawake, Rachel Senny amesema wanawake ndio wazalishaji wakubwa katika nchi lakini si wengi waliopo katika mfumo rasmi wa kifedha kwa ajili ya kuweka akiba na kupata mikopo.
“Sio kwamba wanawake hawapendi kuweka akiba hapana ndio maana wana vibubu na sio kwamba hawapendi kupata mikopo sio kweli wana mikopo huko mtaani tena mingine inawaumiza, hivyo ndiyo maana tunaona ni muhimu kuwaonyesha fursa zilizopo na kuwafungua macho,” amesema.