Jinsi Chadema inavyosuka safu ya uongozi mikoani

Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema akizungumza katika uchaguzi wa kuwapata viongozi wapya wa Mkoa wa Geita. Wengine waliokaa ni viongozi wa kamati ya chama hicho waliokuwa wakisimamia mchakato huo.

Muktasari:

Aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba ashinda uenyekiti wa Chadema Kagera

Dar es Salaam. Mikoa sita inayounda kanda za Victoria na Serengeti za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imekamilisha safu za viongozi wa juu wa chama hicho katika mikoa.

Chaguzi za kuwapata viongozi hao wajuu wa mikoa wakiwamo pia wa mabaraza ya vijana, wazee na wanawake wa Chadema zilifanyika kuanzia Machi 24 hadi Machi 28 mwaka huu katika mikoa ya Mwanza, Kagera, Simiyu, Mara, Geita na Shinyanga.

Mchakato wa kuwapata viongozi wa Chadema wa mikoa unafanyika baada ya kukamilika kwa uchaguzi viongozi wa ngazi chini ikiwamo matawi, majimbo na wilaya.

Akizungumza na Mwananchi Digital,  leo Ijumaa Machi 29, 2024, Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zakaria Obadi amesema katika mkoa wa Kagera, aliyekuwa Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba ameshinda uenyekiti wa chama hicho, huku Daniel Damian akipendekezwa kuwa katibu wa mkoa huo.

Obadi amesema katika Mkoa wa Geita, nafasi ya uenyekiti wa mkoa imeenda kwa Makanji Kasandiko na Deogratius Shinyanga akipendekezwa kuwa katibu wa mkoa huo.

Kwa Mkoa wa Mwanza, Peter Matyoko ameibuka na ushindi nafasi ya uenyekiti, Boniphece Nkobe akipendekezwa nafasi ya katibu wa mkoa.

Katibu wa Chadema, Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami amesema Emmanuel Ntobi ameshinda uenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga, huku Agatha Mamuya akipendekezwa kuwa katibu wa mkoa.

Ntobi aliwahi kuwa mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Shinyanga kabla ya mwaka 2023 kuondolewa katika kiti hicho kwa madai ya vitendo vya utovu wa nidhamu.

Katika Mkoa wa Mara, aliyeshinda uenyekiti ni Chacha Heche, huku Donald Mwembe akipendekezwa kuwa katibu wa mkoa.

“Tunashukuru tumemaliza salama mchakato wa uchaguzi katika mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara, kinachofuata tunasubiri utaratibu kutoka ofisi ya katibu mkuu wa chama kuhusu hatua nyingine ya uchaguzi wa kanda,” amesema Mnyawami.

Kwa mujibu wa taratibu za Chadema, baada ya makatibu wa kanda kupendekezwa katika uchaguzi, watathibitishwa katika kikao cha kamati ya utendaji ya kanda husika.

Wakati kanda za Serengeti na Mara zikikamilisha mchakato, kanda ya Pwani yenye mikoa ya Pwani na Dar es Salaam inatarajiwa kufanya uchaguzi wa ngazi ya mikoa kuanzia Aprili 3 hadi 5, 2024.

Katibu wa kanda hiyo, Jerry Kerenge amesema wilaya za Dar es Salaam, wamezigawanya kimkoa akisema Mkoa wa Kinondoni waliopitishiwa kugombea uenyekiti ni Henry Kilewo (anayetetea) na Joel Mwakalebela.

Kerenge amesema Ubungo walioteuliwa kuwania uenyekiti ni Amos Maziku na Ernest Mgawe. Wakati Ilala waliopitishwa kuwania uenyekiti ni Jacob Kissi, Manase Mjema, Gabriel Moshi na Deogatius Kajula.

Katika Kanda ya Nyasa yenye mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, Rukwa na Songwe wanatarajia kuanza uchaguzi Aprili 2 hadi 3, 2024.