Kaka adaiwa kumuua dada yake kwa jembe

Muktasari:
Imedaiwa kuwa ndugu hao walikuwa na mzozo kwa muda mrefu kutokana na mtuhumiwa kukataa kumsaidia mama yake
Rombo. Mkazi wa Kijiji cha Kingachi wilayani Rombo, Avelin Arobogast (48) ameuawa kwa madai ya kupigwa na jembe kichwani na mdogo wake wa kiume baada ya kumwambia aache ulevi ili amsaidie mama yake ambaye ni mgonjwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Emmanuel Lukula alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 25 na kumtaja mtuhumiwa wa mauaji hayo kuwa ni Simon Arobogast (36).
Alisema Avelin alipigwa na jembe kichwani upande wa kisogoni na kusababisha kutokwa na damu nyingi.
Kamanda Lukula alisema Jeshi la polisi linaendelea kumsaka mtuhumiwa huyo baada ya kutoroka.
Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kingachi Prosper Msana alisema ndugu hao wamekuwa na mzozo kwa muda mrefu kutokana na mtuhumiwa kukataa kumsaidia mama yake ambaye ni mgonjwa wa kiharusi badala yake fedha anazopata kibaruani hutumia kulewa na kuisumbua familia.
“Hawa watu ni jirani zangu, wamekuwa na mzozano kuhusu kumhudumia mama yao mgonjwa, huyu marehemu(dada mkubwa) alimuuliza mdogo wake kwanini anaenda kibaruani akipata fedha analewa na wakati mama yao ni mgonjwa?,” alisema mwenyekiti huyo.
“Basi walianza mzozano, ndipo akaamua kuchukua jembe akampiga kichwani kisha akadondoka, alivuja damu nyingi na alipokuwa anapelekwa Hospitali ya Karume alifariki dunia kabla ya kupewa huduma.”
Hata hivyo, Kamanda Lukula alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Karume wilayani hapa unasubiri kufanyiwa uchunguzi zaidi wa kutabibu.