Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KESI YA MAUAJI YA MUUZA MADINI MTWARA: Kutoka mipango, mauaji mpaka askari kunyongwa- 10

Muktasari:

  •  Juni 23, 2025, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Mtwara iliwahukumu kunyongwa hadi kufa askari wawili kati ya saba kwa kosa la mauaji ya muuza madini, Mussa Hamis

Dar es Salaam. Katika sehemu hii ya mfululizo wa mapitio ya hukumu ya kesi ya mauaji iliyokuwa ikiwakabili polisi saba mkoani Mtwara, Mahakama inachambua ushahidi wa pande zote na kuamua kiini cha kwanza cha hatia ya kosa la mauaji.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Gilbert Sostenes Kalanje aliyekuwa Mrakibu wa Polisi na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara, Charles Onyango (Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Mkuu wa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara) na Nicholous Kisinza, Mrakibu Msaidizi wa Polisi na Ofisa wa Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara.

Wengine ni Marco Chigingozi, Mkaguzi Msaidizi, John Msuya (Mkaguzi na Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara), Shirazi Mkupa (Mkaguzi Msaidizi) na Salim Mbalu alikuwa Koplo.

Wote walishtakiwa kwa kosa la kumuua kwa kukusudia, mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis, mkazi wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi Januari 5, 2022, ndani ya Kituo cha Polisi Mitengo  wilayani  Mtwara.

Jaji Hamidu Mwanga kutoka Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, baada ya kujibu hoja za washtakiwa na mawakili wao kuhusu uhalali wa hati ya mashtaka, katika sehemu iliyopita, sasa anaendelea na simulizi ya hukumu hii.


Je ni kweli Mussa ni marehemu?

Jaji Mwanga alianza kwa kueleza kuwa, katika kesi ya aina hii ya mauaji, vipengele vitatu lazima vithibitishwe na upande wa mashtaka ili kumtia hatiani mshtakiwa.

“Kwanza, mtu anayedaiwa kuuawa amefariki, na kifo chake si cha kawaida.  Pili, watuhumiwa ndio waliohusika na kifo hicho, na tatu mauaji hayo yalifanywa kwa nia ovu au kwa kudhamiria,”alisema Jaji Mwanga.

“Kwa kuzingatia vipengele hivyo vitatu, nitachambua ushahidi uliowasilishwa kwa kila kipengele cha kosa hilo kwa kina, ili kubaini kama upande wa mashtaka umetimiza wajibu wake wa kuthibitisha kosa,”alieleza Jaji.

“Nikianza na kipengele cha kwanza, swali ni je, Mussa Hamis Hamis amefariki na ikiwa ndio, je alikufa kwa kifo kisicho cha kawaida?

“Katika hoja zao, mawakili wa mshtakiwa wa kwanza, Kalanje na wa pili, Onyango walidai kuwa, hakuna ushahidi madhubuti unaothibitisha kuwa Mussa Hamis Hamis amefariki, kwa kuwa chanzo cha kifo hakikubainika,”alisema.


Msimamo ushahidi wa mazingira

Jajia akaendelea: “Kwa mujibu wa msimamo wa sasa wa kisheria, mauaji yanaweza kuthibitishwa kwa ushahidi wa kimazingira hata bila ripoti ya uchunguzi wa daktari (postmortem) au kuwasilishwa kwa mwili wa marehemu.

“Kanuni hii ilielezwa katika kesi ya Mathias Bundala dhidi ya Jamhuri, rufaa ya jinai namba 62 ya mwaka 2004, Mahakama ya Rufaa, Mahakama ilisema, ...si sharti la kisheria kuwa chanzo cha kifo lazima kibainishwe katika kila kesi ya mauaji.

“Tunafahamu kuwa kuna utaratibu, kifo kinaweza kuthibitishwa kwa ushahidi wa kimazingira hata bila kuwasilishwa kwa mwili wa mtu anayedaiwa kufariki.

“Hivyo, ni wazi kisheria kuwa kosa la mauaji linaweza kuthibitishwa ipasavyo hata bila kubaini chanzo cha kifo,”alisisitiza Jaji Mwanga katika hukumu hiyo.

Jaji alisema katika kesi ya Said Bakari dhidi ya Jamhuri, rufaa ya jinai namba 422 ya 2013, iliyonukuliwa na Mahakama ya Rufaa katika kesi ya Sikujua Idd dhidi ya Jamhuri, rufaa ya jinai namba 484 ya 2019, ilielezwa kuwa:

“Ni sheria iliyo thabiti kwamba, kosa la mauaji linaweza kuthibitishwa kikamilifu kwa ushahidi wa kimazingira. Katika kuamua kesi inayojikita kwenye ushahidi wa kimazingira, njia sahihi kwa Mahakama ya kwanza na ile ya rufaa ni kuchambua na kupima kwa kina mazingira yote yaliyothibitishwa na ushahidi kwa jumla wake na siyo kuyachambua kwa vipande au kuyazingatia kwa kutenganisha vipande vya ushahidi au mazingira.

“Pia, nchini India, katika kesi ya Mani Kumar Thapa dhidi ya Jimbo la Sikkim, AIR 2002 SC 2920, Mahakama iliamua kama ifuatavyo; katika kesi ya mauaji, si lazima kwa kiwango cha juu wala siyo kiambatanisho muhimu kuthibitisha ‘corpus delicti’ (yaani mwili wa marehemu). Ukweli wa kifo,  lazima uthibitishwe kama ilivyo kwa ukweli mwingine wowote. Mwili wa marehemu katika baadhi ya kesi, huenda usiweze kupatikana.”

“Kuna uwezekano mwingi mwili wa marehemu unaweza kuondolewa (usipatikane) bila kuacha dalili yoyote,”alisema Jaji Mwanga.

“Hivyo basi, kama upatikanaji wa mwili wa marehemu utakuwa wa lazima ili kumtia mtu hatiani, basi katika kesi nyingi, watuhumiwa wangefanikiwa kuhakikisha kuwa mwili wa marehemu unaharibiwa kiasi cha kumpa mshtakiwa kinga kamili dhidi ya kutiwa hatiani au kupewa adhabu.

“Kinachohitajika kisheria ili kutoa hukumu ya hatia ya kosa la mauaji ni kuwepo kwa ushahidi wa kuaminika na wa kueleweka kwamba kosa la mauaji, kama ilivyo kwa tukio jingine la kifo, lilitendeka, lazima lithibitishwe kwa ushahidi wa moja kwa moja au wa kimazingira, hata kama mwili wa marehemu haukupatikana.

“Kwa misingi hiyo ya kisheria, ni dhahiri kwamba mauaji yanaweza kuthibitishwa bila uwepo wa mwili wa marehemu,”alieleza Jaji Mwanga.


Ulazima wa sababu ya kifo

Jaji Mwanga alisema athari za kutaka sababu ya kifo ithibitishwe ili kuthibitisha kosa la mauaji ziliwahi kushughulikiwa na Mahakama hii katika kesi ya Jamhuri dhidi ya Hamisi Said Luwongo @ Meshack, kesi ya jinai namba 44 ya 2023, Mahakama ilionya kwamba:

“Inapaswa kusisitizwa kwamba, kushikilia msimamo wa kufanya uchunguzi wa maiti na kuwa na mwili wa marehemu kutakuwa na madhara mawili katika mfumo wa haki ya jina,”alisema Jaji Mwanga.

“Kwanza, kuua na kuharibu mwili kutakuwa ni kinga kamili kwa wauaji dhidi ya kutiwa hatiani au kupewa adhabu. Pili, mauaji mengi hayatatatuliwa kwa kuwa wauaji watajificha nyuma ya ukosefu wa maiti.

“Hivyo basi, madai ya wakili wa utetezi kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaothibitisha kuwa Musa Hamis Hamis amefariki dunia, kwa kuwa sababu ya kifo haikuthibitishwa, hayana msingi wowote wa kisheria,”alisisitiza Jaji.


Ushahidi wa Mussa kuitwa polisi

Jaji alisema ni ushahidi wa Hawa Bakari ambaye ni shahidi wa kwanza upande wa mashtaka, mama mzazi wa marehemu, kuwa mwanawe Mussa alitoweka tangu Januari 5, 2022, baada ya kuitwa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara na washtakiwa.

Ushahidi huu uliungwa mkono na ushahidi wa shahidi wa pili, Salumu Abdallah Ng'ombo, aliyempeleka Mussa Hamis Hamis katika Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara tarehe hiyo kumuacha hapo, na hakumuona tena tangu siku hiyo.

Pia, kuna ushahidi wa shahidi wa 20, Geofrey Simba, Januari 21, 2022, akiwa ameongozwa na Inspekta Msaidizi Greyson Mahembe eneo la msitu wa Hiari, alishuhudia mbavu na mifupa kadhaa ya binadamu, ambavyo ni vielelezo namba PE6 na PE7 vya upande wa mashtaka.

“Vielelezo hivyo vilifanyiwa vipimo vya vinasaba (DNA) na Fidelis Bugoye ambaye ni shahidi wa tisa ambaye pia ni Mkemia wa Serikali na kulinganishwa na sampuli za mate kutoka kwa mama wa marehemu,na kubainika kuwa mifupa hiyo ni ya binadamu na ilikuwa ya Musa Hamis Hamis,”alieleza Jaji.

“Hivyo basi, tukitumia misingi ya kisheria iliyoelezwa katika kesi za hapo juu kuhusu uthibitisho wa kifo kwa ushahidi wa kimazingira, kwa kuzingatia ukweli na mazingira ya kesi hii, hakuna shaka kwamba Musa Hamis Hamis amefariki dunia.

“Kwa mujibu wa ushahidi wa utetezi, aliuawa kwa ukatili na mwili wake kutupwa kinyama katika msitu wa Hiari. Hivyo, hoja ya kwanza inajibiwa kwa uthibitisho,”alisema Jaji Mwanga.

Usikose sehemu ijayo kuona Mahakama ilivyochambua ushahidi kuhusu kiini cha pili, kama washtakiwa ndio waliohusika na kifo hicho.