Kardinali Rugambwa: Nimeyapokea majukumu haya kwa unyeyekevu

Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa (katikati), akiwa na Askofu Mkuu Paul Ruzoka (kushoto) na Mkuu wa Mkoa  Tabora Dk Batilda Burian. Picha na Robert Kakwesi

Muktasari:

  • Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa awasili jimboni Tabora huku akiwashukuru watanzania na kusema ameyapokea majukumu ya ukardinali kwa unyenyekevu mkubwa kama alivyokuwa anayapokea mengine katika maisha yake.

Tabora. Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa awasili jimboni Tabora huku akiwashukuru watanzania na kusema ameyapokea majukumu ya ukardinali kwa unyenyekevu mkubwa kama alivyokuwa anayapokea mengine katika maisha yake.

Hayo amesayema leo kweye hafla ya kumpokea akitokea jijini Dar es Salaam alikowasili jana Ijumaa Oktoba 6, 2023; akitokea Vatican Roma, alikokuwa ameenda kwaajili ya ibada ya kusimikwa rasmi hadhi hiyo baada ya kuwa ametangazwa Julai 9, 2023 akiwa anatoka kwenye ibada ya Mama Maria wa Fatima.

“Nimeyapokea majukumu ya ukardinali kwa unyenyekevu mkubwa kama ambavy nimekuwa nikipokea majukumu mengine katika maisha yangu ya utume...nina ahidi kushirikiana na waumini, wananchi wote kwa ujumla lakini pia kushirikiana na Serikali,” amesema.

Hivyo kardinali huyo amewataka wote walipofika kumpokea kujisikia kuwa wapo nyumbani na kusisitiza kuu ya kuwa na mashirikiano pasipo kubaguana.

Amesema wamewekwa makardinali 21 na Papa huko Roma na kusindikizwa na wengi akiwemo Askofu Mkuu wa jimbo kuu la Tabora Paul Ruzoka na kuwashukuru wote kwa mapokezi mazuri kuanzia Dar es Salaam hadi leo Tabora na kwamba alishtuka kwani alitegemea kupokewa na watu wasiozidi thelathini.

“Ilibidi viongozi ndani ya ndege wawaeleza abiria kuwa wasubiri kwanza wao wateremke na kwamba ni upendo mkubwa sana waliouonesha ambao wanapaswa pia kumpa Mwenyezi Mungu,” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Barilda Burian amemweleza Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa kuwa atapata ushirikiano mkubwa kutoka Serikalini na kumuomba asiwe na wasiwasi.

Amemtaka adumishe ushiriano uliopo huku akilipongeza Kanisa kwa kutoa huduma za kijamii kwa kushirikiana na Serikali.