‘Karibu nyumbani’ Rugemalira baada ya siku 1,550

Muktasari:

  •  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana imemwachia huru mfanyabiashara James Rugemarila baada ya kukaa mahabusu kwa siku 1,550 tangu aliposhikiliwa Juni 19, 2017.


Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana imemwachia huru mfanyabiashara James Rugemarila baada ya kukaa mahabusu kwa siku 1,550 tangu aliposhikiliwa Juni 19, 2017.

Hatua hiyo ni baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuieleza mahakamani hiyo kuwa hana tena nia kuendelea na mashtaka dhidi yake.

Baada ya kuachiwa, nje ya mahakama, Rugemalira alilakiwa na wanafamilia pamoja na ndugu na marafiki ambao waliongozana naye hadi Kanisa Katoliki, Makongo Juu alikokwenda kumshukuru Mungu na baadaye nyumbani kwake.

Rugemalira ambaye ni mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), alikuwa anakabiliwa na mashtaka 12 ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Mshtakiwa huyo amefutiwa mashtaka chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), sura ya 20, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Hadi jana, Rugemalira aliendelea kukaa mahabusu zaidi ya miaka minne baada ya kushtakiwa kwa makosa hayo yasiyodhaminika.

Kila mara kesi hiyo ilipotajwa, upande wa mashitaka uliomba iahirishwa kwa kuwa upelelezi ulikuwa haujakamilika.

Uamuzi wa kumfutia mashtaka hayo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yake.

Wakili wa Serikali, Grace Mwanga aliieleza mahakama hiyo kuwa kesi hiyo ilikuwa imeitwa kwa ajili ya kutajwa lakini DPP alikuwa amewasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea nayo.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu alisema kupitia kifungu hicho, mahakama imemfutia mashtaka mshtakiwa huyo na kumwachia huru.

‘Karibu nyumbani’ Rugemalira baada ya siku 1,550

Hata hivyo, Hakimu Shaidi alisema kupitia kifungu hicho, DPP anao uwezo wa kumkamata na kumfungulia tena mashtaka, mshtakiwa huyo.

Wakati Rugemalira akifutiwa kesi na kuachiwa huru, mshtakiwa wa tatu ambaye ni mwanasheria wa IPTL, Joseph Makandege, ameendelea kushikiliwa.

Kesi dhidi ya Makandege imeahirishwa hadi Septemba 23, itakapotajwa huku upande wa mashtaka ukiieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wake haujakamilika.

Ndugu wapiga vigelegele

Baada ya Hakimu Shaidi kumwambia mshtakiwa amefutiwa kesi na anaweza kuondoka ndani ya chumba cha Mahakama, Rugemalira alionyesha furaha kubwa.

Ndugu na jamaa wa mfanyabiashara huyo waliofika mahakamani walipiga vigelegele vya shangwe baada ya hakimu kutamka kuwa ndugu yao yuko huru.

Rugemalira aliyekuwa amevalia kanzu nyeupe na kuning’iniza rozari shingoni huku akionekana kujawa na furaha alitumia muda wake kuagana na maofisa wa magereza na polisi waliokuwepo mahakamani hapo.

Aaanzia kanisani

Mara tu baada ya kutoka Kisutu, Rugemarila alikwenda moja kwa moja katika Parokia ya Bikira Maria Mama wa Rozari Takatifu, Makongo Juu kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kutoka gerezani.

Akiwa kanisani hapo alifanya sala fupi ndani ya kanisa hilo, na alipotoka nje hakuwa tayari kuzungumza na mwandishi wa Mwananchi kwa kirefu akisema “kwa leo sitaweza kuongea kwa sababu ya corona na ndio kwanza nimetoka gerezani, hivyo naomba muda niongee siku nyingine.”

Kutoka Kisutu hadi kanisani na hatimaye nyumbani, alikuwa ameambatana na mke wake, Benedicta, mtoto wao wa kiume na mmoja wa wanasheria wake.

Harakati kujikwamua

Februari 13, 2020, Rugemalira alimuomba DPP amuondoe katika kesi hiyo akidai alikuwa ameshawasilisha nyaraka za watu wanaotakiwa kushtakiwa katika kesi hiyo.

Alidai kuwa kelele alizopiga zitasaida kukamatwa kwa wezi halisi waliohusika katika kesi.

Pia, mshtakiwa huyo alidai kuwa aliwasilisha notisi (taarifa) kwa taasisi kubwa tisa, akimtaka DPP amuondoe kwenye kesi hiyo na asipofanya hivyo atawasilisha maombi rasmi ya kuiomba mahakama imwondoe katika kesi.

Aomba afutiwe kesi

Desemba 19, 2020 Rugemalira aliiomba mahakama imfutie kesi ifikapo Desemba 31, 2020 endapo upande wa mashtaka ungekuwa haujakamilisha upelelezi.

Rugemalira alipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka sita na mwenzake Harbinder Singh Seth ambaye ni mmiliki wa IPTL wakidaiwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu na kuisababisha Serikali hasara ya jumla ya takriban Sh358 bilioni.

Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi alidai washtakiwa hao walitenda makosa hayo kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam na katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India.

Wakili Kadushi alidai washtakiwa hao, wakiwa si watumishi wa umma, waliunda mtandao wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Mara kwa mara Rugemalira alisisitiza hana hatia katika kesi na hata yalipoanzishwa majadiliano ya DPP kuhusu kufutiwa mashtaka hayapiga hatua za maana, isipokuwa kwa mwenzake Seth ambaye aliachiwa Juni 16, 2021 baada ya kukiri kosa na kupigwa faini na fidia ya Sh26.9 bilioni.