Kesi inayomkabili ofisa kilimo Moshi Aprili 30

Erimina Clement Marandu(40), ambaye ni mmoja wa maofisa kilimo Wilaya ya Moshi akitoka mahakamani
Muktasari:
Kesi ya jinai inayomkabili mmoja wa maofisa kilimo, Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro, Ermina Clement Marandu(40) jina maarufu Pendo ya kumjeruhi na kushindwa kutoa huduma muhimu kwa msaidizi wake wa kazi za ndani, imepangwa kusikilizwa April 30, mwaka huu katika mahakama ya Wilaya ya Moshi baada ya kusomewa maelezo ya awali.
Moshi. Kesi ya jinai inayomkabili mmoja wa maofisa kilimo wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, Ermina Marandu (40) maarufu Pendo ya kumjeruhi na kushindwa kutoa huduma muhimu kwa msaidizi wake wa kazi za ndani itaanza kusikilizwa Aprili 30, mwaka huu katika mahakama ya Wilaya ya Moshi baada ya kusomewa maelezo ya awali.
Mshitakiwa huyo ambaye yupo nje kwa dhamana, leo Jumatano Aprili 3, 2024 amefikishwa mahakamani hapo na kusomewa maelezo ya awali mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama hiyo, Ruth Mkisi.
Hata hivyo, Hakimu Mkisi alisema kesi hiyo imepangwa kuanza kusikilizwa mahakamani hapo Aprili 30, mwaka huu.
"Baada ya mshitakiwa kusomewa maelezo ya awali ya kosa, tumepanga kusikiliza kesi hii Aprili 30, mwaka huu," amesema hakimu Mkisi.
Kwa mara ya kwanza mshitakiwa alifikishwa mahakamani Machi 13, mwaka huu akikabiliwa na kosa la kumjeruhi na kushindwa kutoa huduma na mahitaji muhimu kwa msaidizi huyo wa kazi za ndani.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 38/2024, mshitakiwa ambaye ni mwenyeji wa Wilaya ya Rombo na mkazi wa Kilototoni, kata ya Njia panda, Mji mdogo wa Himo, anadaiwa kumshambulia mfanyakazi huyo aitwaye Meresiana Nestory (16) kwa kumpiga na mti wa fagio na mateke na kumsababishia majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kesi hiyo itaongozwa na mawakili watatu wa upande wa Jamhuri ambao ni Kambarage Samson, Emelda Mushi na Amina Mkayale.
Msichana huyo ambaye ni mwenyeji wa Nyakanazi, Wilaya ya Biharamulo Kagera, kwa sasa anaendelea na matibabu aliyoyapata.
Kwa sasa anaishi wilayani Mwanga baada ya kuchukuliwa na ndugu yake.
Imeandikwa na Janeth Joseph na Florah Temba