Hausigeli, mama mahabusu kwa kujeruhi mtoto

Muktasari:
Mfanyakazi huyo ambaye ni mkazi wa Stakishari, Blanka Benjamin (15) kwa pamoja na mfanyabiashara Christine Thomas (28) wanadaiwa kutenda kosa hilo
Dar es Salaam. Mfanyakazi wa ndani (hausigeli) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kujibu mashtaka, likiwamo la kumpiga mtoto hadi kupoteza fahamu.
Mfanyakazi huyo ambaye ni mkazi wa Stakishari, Blanka Benjamin (15) kwa pamoja na mfanyabiashara Christine Thomas (28) wanadaiwa kutenda kosa hilo.
Christine anadaiwa kumpiga mtoto wake wa miaka miwili hadi akapoteza fahamu na kushindwa kumpeleka hospitali kwa matibabu na badala yake alimtelekeza huku akidaiwa kuwa na hali mbaya.
Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali, Hilda Kato mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ritha Tarimo amedai katika shtaka la kwanza linalomkabili Christine, alimpiga mtoto wake na kumsababishia maumivu makali yaliyosababisha apoteze fahamu.
Katika shtaka la pili linalowakabiliwa washtakiwa wote, wanadaiwa walifanya uzembe baada ya kumtekelekeza mtoto huyo kwa kushindwa kumpeleka hospitali kutibiwa.
Washtakiwa wamekana mashtaka na Hakimu Tarimo alitoa masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili kutoka taasisi inayotambuliwa kisheria watakaosaini dhamana ya Sh800,000.
Wamerudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana na Hakimu Tarimo aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 23 itakapotajwa.