Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kibano chaja waganga wakuu wa wilaya

New Content Item (4)

Waziri wa Tamisemi, Mohammed Mchengerwa (kushoto) akikabidhi funguo kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela (kulia) wakati wa kupokea magari 13 yaliyotolewa na Serikali kwa waganga wakuu wa wilaya za Arusha (5) na Manyara (8). Wengine wanaoshuhudia ni mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Thomas Sabaya, na Katibu wa CCM Mussa Matoroka. Picha na Bertha Ismail.

Muktasari:

  •  Serikali yafanya mapitio kuwachuja wasiowajibika, Waziri Mchengerwa agusia vifo vya wajawazito kwa uzembe

Arusha. Serikali imesema iko katika mchakato wa kufanya mapitio, kuwachuja waganga wakuu wa wilaya (DMO) kwa kuwaondoa walioshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amesema hayo leo Desemba 14, 2023 alipokabidhi magari 13 kwa sekta ya afya.

Mkoa wa Arusha umepatiwa magari matano na Manyara manane yatakayotumika kwenye wilaya za mikoa hiyo.

Mchengerwa amesema  kumekuwapo matukio mengi ya kihalifu yanayotokea ndani ya vituo vya afya, ikiwamo wajawazito kunyimwa huduma stahiki za kujifungua kwa  kukosa fedha.

Amesema wizara imekuwa ikitoa tamko kuhusu matukio hayo, wakati waganga wakuu wa wilaya wapo.

"Waganga wa wilaya niwaambie tu wazi, kutakuwa na zoezi la kufanya mapitio hivi karibuni ili kuona wale ambao wana sifa ndiyo watakaobaki kwenye nafasi zao, namaanisha wale ambao wako tayari kuwasikiliza wananchi na kufanya usimamizi mzuri katika maeneo yao, hivyo kuokoa maisha ya Watanzania," amesema Mchengerwa.

"Mfano, haiwezekani mjamzito anafika kituo cha afya anashindwa kuhudumiwa hadi anapata matatizo au kufariki dunia kwa sababu eti amekosa fedha labda Sh50,000 na wakati mwingine huduma hizo ni bure. Haiwezekani hata kidogo, unaweza kufanya kisingizio hujui lakini itabidi utupishe."

Kuhusu magari hayo, Mchengerwa amesema yakatumike kwenye usimamizi wa sekta ya afya na si vinginevyo.

"Naamini baada ya kukabidhiwa hakutakuwa na malalamiko wala kisingizio cha kwa nini mtendaji ameshindwa kwenda kusimamia kazi katika eneo lake, kwa sababu gari la usimamizi unalo, lakini pia hatutataka kusikia mganga wa wilaya huna taarifa ya matukio katika vituo vyako vya afya," amesema.

Mchengerwa amewataka waganga wakuu wa wilaya, wakuu wa wilaya na wakurugenzi kufanya mazungumzo na wataalamu wote katika maeneo yao na kuwahudumia Watanzania.

"Rais Samia (Suluhu Hassan) amemaliza kwa nafasi yake, ameleta fedha za ujenzi, vifaatiba, magari na ajira katoa; kazi iliyobaki ni sisi kwenda kusimamia utekelezaji wa azma yake ya kila Mtanzania akapate huduma bora za afya," amesema Mchengerwa.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Tamisemi anayeshughulikia sekta ya afya, Dk Wilson Mahera amesema hatasita kuwachukulia hatua kali watumishi wa afya wanaofanya uzembe, hasa kwa wajawazito wanaokwenda kujifungua katika vituo vya afya na zahanati.

"Ole wenu watumishi wa afya mnaofanya uzembe kwa wagonjwa, tutachukua hatua. Nanyi wahudumu wa afya, wenzenu wakichukuliwa hatua halafu mkalalamika kuwa hawakustahili adhabu husika, pia tutawachukulia hatua. Haiwezekani mgonjwa anataka huduma za afya halafu mnazembea na kusababisha vifo," amesema.

Moja kati ya wilaya ya mkoani Arusha iliyokabidhiwa gari ni Karatu, ambayo mkurugenzi mtendaji wa halmashauri, Juma Hokororo amesema changamoto kubwa kwa sekta ya afya ilikuwa usafiri kwa ajili ya utekelezaji wa kaguzi na taarifa za vituo vya afya.

"Tunashukuru Rais Samia kutuletea magari haya, yataenda kuongeza kasi kubwa ya utekelezaji wa majukumu ya sekta ya afya kwa Wilaya ya Karatu, tunaahidi kuyatunza ili yadumu na yafanye kazi iliyokusudiwa," amesema Hokororo.