Kibarua cha gavana mpya wa BoT

Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba akifurahia jambo na mtangulizi wake Prof Florens Luoga alipowasili kwa mara ya kwanza Makao Makuu ya Benki Kuu ya Tanzania Dodoma. Picha na BOT

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza mabadiliko ya gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wadau wameeleza matarajio yao huku udhibiti wa mfumuko wa bei na ustawi wa sekta ya fedha vikitiliwa mkazo zaidi ili kutoa unafuu wa maisha kutokana na ugumu uliopo.

Juzi usiku, Rais Samia alimteua aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba kuwa gavana mpya wa BoT kuchukua nafasi ya Profesa Florens Luoga aliyestaafu.

Akizungumza na gazeti hili, Tutuba alisema BoT ni taasisi kubwa iliyojengwa kwa mifumo imara ambayo hakuna anayeweza kuipindisha kirahisi.

“Hakuna jipya zaidi ya kwenda kuangalia wenzangu wameishia wapi ili nami niendeleze mazuri waliyoyafanya. BoT inasimamia sera ya fedha pia nafahamu mwezi ujao itapitiwa kwa kushirikiana na IMF (Shirika la Fedha Duniani), tutashirikiana,” alisema Tutuba.

Vilevile, gavana huyo mpya alisema anafahamu BoT inalo jukumu la kusimamia utekelezaji wa ‘Tanzania Financial Sector Masterplan’ (Mkakati Kabambe wa Sekta ya Fedha Tanzania) unaogusa benki za biashara, taasisi za fedha, kampuni za bima na mifuko ya hifadhi za jamii.

“Hakuna gavana anayeenda BoT na jambo jipya. Kila kitu kinafahamika iwe kiasi cha ukwasi unaotakiwa au kingine chochote,” alisisitiza Tutuba.

Wakati Tutuba akisema hayo, mtaani kuna masuala kadhaa ambayo wadau wanasubiri kuona yanafanyiwa kazi haraka ili kurudisha mambo kwenye mstari ikiwamo kilio cha wamiliki wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni yaliyofungwa miaka minne iliyopita, kuongezeka kwa udanganyifu wa miamala ya fedha pamoja na mfumuko wa bei kwa bidhaa mbalimbali hasa vyakula na mafuta.

Mkurugenzi wa Shahada za Juu wa Chuo cha Usimamizi wa Biashara (CBE), Dk Dickson Pastory alisema miongoni mwa masuala ambayo gavana mpya anapaswa kuyaangalia kwa makini ni mfumuko wa bei.

“Kati ya masuala anayopaswa kuyasimamia kwa nguvu zote ni sera ya fedha ili kupunguza mfumuko wa bei, aangalie fedha zilizopo kwenye mzunguko ikibidi zipunguzwe kwa kuwa zikiwa nyingi husasababisha mfumuko kuongezeka,” alishauri Dk Pastory.

Alisema hatua hiyo ni muhimu ikaangalia iwapo ongezeko hilo ni jambo la muda mrefu au mfupi na kama litakuwa limetokana na Serikali kuwa na matumizi makubwa basi iyapunguze kwa namna ambayo haitoathiri ustawi wake.

Vilevile, Dk Pastory alisema gavana anapaswa kuja na mbinu za kuhakikisha benki za biashara zinapunguza riba ya mikopo kwa kuwa ni sehemu ya gharama za uendeshaji hivyo mzigo wote anatwishwa mkopaji.

Mwenyekiti wa Chama cha Wakurugenzi wa Benki Tanzania (TBA), Theobald Sabi alisema wana imani kubwa na utendaji wa Tutuba kwani wamekuwa wakishirikiana naye kwa ukaribu akiwa Katibu Mkuu wa Wizara.

“Kwa niaba ya wajumbe wa bodi ya TBA, tunampongeza Tutuba kwa kuteuliwa, uzoefu wake katika masuala ya sera za kiuchumi na usimamizi wa fedha za umma ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa majukumu yake mapya,” alisema Sabi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC.

Sabi alisema TBA inajivunia uongozi mzuri wa Tutuba tangu akiwa Katibu Mkuu na wana imani wataendelea kushirikiana kwa karibu kwa maslahi ya maendeleo ya uchumi wa nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Taasisi Ndogo za Fedha Tanzania (Tamfi), Winnie Terry alisema wana matarajio makubwa kwa Tutuba kwa kuwa wanamfahamu, ni mdau mwenzao wa huduma ndogo za fedha.

“Tuna matamanio na matarajio makubwa kwa kuwa tumekuwa na mijadala naye mara kadhaa juu ya ustawi wa huduma ndogo za fedha, tunajua namna gani anaguswa na maendeleo ya sekta hii hivyo tunatarajia makubwa kutoka kwake,” alisema Winnie.


Mabadiliko BoT

Wakati Tutuba akitoka wizarani kwenda BoT, nafasi yake imejazwa na Dk Natu Mwamba aliyewahi kuwa naibu gavana miaka ya nyuma kisha akarudi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuendelea kufundisha huku akiwa mwenyekiti wa Bodi ya Uendeshaji wa Kiwanja cha Ndege Kilimanjaro (Kadco).

Kubadilishana kwa watendaji hao waandamizi, meneja mmoja wa benki alisema kutaongeza ushirikiano wa taasisi hizo muhimu za fedha na kuimarisha uwajibikaji.

“Aliyeteuliwa kuwa katibu mkuu alikuwa naibu gavana. Ukiangalia utaona mama (Rais Samia) anatengeneza muunganiko wa wizara na BoT. Watu wa BoT walikuwa wanajiona wao ni superior (bora) kuliko wizara. Walikuwa wanafanya wachotaka, huu uteuzi sio wa bahati mbaya, mama ameimulika BoT), alisema meneja huyo.

Tutuba anakwenda BoT, taasisi inayozisimamia benki za biashara na taasisi zote za fedha nchini, inayoandaa na kutekeleza sera ya fedha na kujenga mfumo wa fedha imara na unaofaa kwa ukuaji endelevu wa uchumi wa Taifa.

Kati ya mambo muhimu ambayo BoT imeyafanya siku za hivi karibuni ni kudhibiti thamani ya shilingi pamoja na mfumuko wa bei ambao umefika asilimia 4.9.

Mfumuko huo ingawa ni mkubwa zaidi kutokea ndani ya miaka mitano iliyopita, bado uko ndani ya malengo ya Tanzania ya kuwa ndani ya tarakimu moja.

Udhibiti huo umetokea BoT ikiwa chini ya Profesa Luoga aliyeuliwa Januari 2018 na kumaliza muda wake hivi sasa.

Licha ya changamoto zilizosababishwa na kuibuka kwa janga la Uviko-19 pamoja na vita vya Ukraine ambazo zimepunguza kasi ya kukua kwa uchumi kutokana na kupungua kwa biashara, hatua zilizochukuliwa na BoT zimeiwezesha Tanzania kutoathirika sana.

Tutuba anaenda kuchukua mikoba huku kilio cha wananchi wengi kikiwa ni ugumu wa kupata mikopo ambayo riba yake ni kubwa pia kwa wengi, hasa wajasiriamali wadogo kuimudu.

“Naomba akaishauri Serikali kuangalia makundi mahsusi ya uchumi wetu. Ni wakati sasa wa kuwa na benki zitakazowahudumia wananchi wa kawaida na wajasiriamali wadogo. Aishauri Serikali kuona namna nzuri ya kuwa na benki za wananchi zitakazowahudumia bila masharti makubwa,” alisema Joseph Haule, mfanyabiashara wa Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Haule alisema wajasiriamali wengi ni watu wenye elimu ndogo kuelewa kwa urahisi lugha ya benki hivyo ukipatikana utaratibu rahisi kwao wengi watatumia huduma za fedha.

Rais wa Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA), Godvictor Lyimo alisema Tutuba ametoka kuwa mtendaji mwenye majukumu mengi na sasa atawajibika kusimamia eneo moja kwa umakini mkubwa.

“Kati ya vitu ninavyotamani aende kuvisimamia ni kuhakikisha usalama wa amana za wateja wa benki. Miaka ya hivi karibuni tumeona benki kadhaa zikifilisika, hili si jambo jema. Adhibiti thamani ya shilingi na kuhakikisha Taifa linakuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni,” alishauri.

Pamoja na kufanikisha hayo yote, Lyimo alisema ni muhimu kuhakikisha mfumuko wa bei unaendelea kuwa wa sarafu moja na deni la Taifa kuhimilika. “Naamini ataishauri vyema Serikali kuhusu ukopaji,” alisema.

Mhamasishaji na muelimishaji wa sarafu mtandao nchini, Sandra Chogo alisema Tutuba bado ni kijana hivyo anaelewa vyema mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea kwenye sekta ya fedha duniani kote.

“Tanzania inatajwa kuwa miongoni mwa mataifa 20 yenye matumizi makubwa ya sarafu mtandao zinazoathiri uchumi wa mtu mmojammoja. Tunahitaji elimu na ujuzi wa sarafu hizi, naamini Tutuba atawashirikisha vijana wenzake wenye ufahamu wa kutosha ili kutoa uelekeo wa Taifa,” alisema Sandra ambaye ni mkaguzi wa hesabu za fedha pia.