‘Kichuya chunga wewe Tambwe anakuja’

Mshambuliaji Amissi Tambwe

Muktasari:

Akiwa Vital’ O ya Burundi, Tambwe alifunga mabao 43 kabla ya kujiunga na Simba 2013

Dar es Salaam. Mechi ya Ligi Kuu baina ya Yanga na JKT Ruvu juzi ambayo mshambuliaji Amissi Tambwe alitokea benchi na kufunga mabao mawili imechochea vita kali ya ubora wa kufumania nyavu kati yake na kinara wa mabao, Shiza Kichuya wa Simba.

Baada ya Kichuya kukosa shabaha kwa dakika 180 alizocheza, Tambwe ana deni la bao moja pekee ili kumfikia kinara huyo wa mabao ambaye msimu huu amekuwa gumzo kila kona likiwamo bao lake la kona dhidi ya Yanga, Oktoba Mosi.

Tayari, Tambwe ambaye ni mshindi wa kiatu cha dhahabu msimu uliopita akiwa na mabao 21, ametamba kuwa kitaeleweka msimu huu tena kwani lazima Yanga itwae bingwa, naye atetee kiatu chake.

Mechi mbili zilizopita dhidi ya Mbao FC na Toto Africans, zote za Mwanza, Kichuya ambaye jina lake limekuwa kwenye chati za juu, hajafunga bao na hivyo kumwachia nafasi Tambwe kuibuka upya na kumkaribia.

Tambwe, aliyekosa michezo miwili za klabu yake, kutokana na kuwa majeruhi, juzi alirejea uwanjani kwenye mchezo dhidi ya JKT Ruvu kipindi cha pili akichukua nafasi ya Donald Ngoma na kufunga mabao mawili yaliyomwezesha kufikisha mabao sita kwenye ligi msimu huu.

Pia, amefikisha mabao 60 tangu aanze kibarua cha kucheza soka Ligi Kuu Tanzania Bara miaka mitatu iliyopita.

Tambwe alitua nchini 2013 na kujiunga na Simba na msimu huo, 2013/2014 aliibuka mfungaji bora kwa kufunga mabao 19, lakini msimu uliofuata, yaani 2014/2015 aliichezea Simba mzunguko wa kwanza pekee kabla ya kuachwa katika mazingira ya utatanishi.

Baadhi ya viongozi wa klabu hiyo (Simba) walidai alikuwa ameshuka kiwango, hivyo kwa hasira aliibukia kwa watani zao, Yanga alikomaliza msimu akiwa na mabao 14, matatu nyuma ya mfungaji bora wa wakati huo, Simon Msuva pia wa Yanga aliyefunga mabao 17.

Hali hiyo ilionyesha kuwa laiti Tambwe angeanza msimu huo akiwa Yanga, angefunga mabao mengi zaidi na pengine angeibuka tena mfungaji bora.

Mrundi huyo alionekana siyo mtu wa mzaha kwani msimu uliopita aliibuka mfungaji bora tena, akimaliza ligi na mabao 21 kibindoni, hivyo ndani ya misimu mitatu akiwa Tanzania kwa kufunga mabao 54 na akiongezewa sita aliyonayo hadi sasa, anafikisha mabao 60.

Tambwe wa ‘hat trick’

Mechi yake ya kwanza kwake kufunga mabao matatu hat trick ilikuwa Februari Mosi, 2014 dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha akiwa na Simba ambayo ilishinda mabao 4-0.

Mechi nyingine ambayo Mrundi huyo alifunga hat trick ilikuwa Septemba 19, 2014 dhidi ya Mgambo JKT, ambayo timu yake ya Simba ilipata ushindi mnono wa mabao 6-0.Mshambuliaji huyo alikamilisha rekodi yake ya kupiga hat-trick kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam msimu uliopita kwa kufunga mabao manne katika ushindi wa mabao 8-0 ya Yanga dhidi ya Coastal Union ya Tanga iliyoshuka daraja msimu huo.

Tambwe alisema mabao mawili aliyofunga katika mchezo dhidi ya JKT Ruvu juzi yamemwongezea kasi ya kufanya vizuri zaidi katika ufungaji ili kuhakikisha anatetea nafasi yake ya ufungaji bora msimu huu.

“Nimefurahi kufunga, nilikosa mechi kadhaa kutokana na kuumia, nimeingia uwanjani kipindi cha pili na kufunga mabao hayo mawili, ni jambo zuri kwangi limenifariji na kunitia moyo.

“Ushindani kwenye upande wa ufungaji msimu huu ni mkubwa zaidi kwani kila mmoja anajitahidi kufunga, ni tofauti na msimu uliopita, naamini nitaendelea kufunga mengi zaidi, malengo yangu ni kuwa mfungaji bora na kuisadia Yanga itwae ubingwa.“Nina imani tutachukua ubingwa tena kwani wapinzani wetu, Simba wametangulia, kuna mahali watakwama nasi tutachukua nafasi,” alisema.

Licha ya kutopenda kumzungumzia mpinzani wake, Kichuya, lakini kasi ya sasa ya Tambwe ni salamu tosha kwa Kichuya, mshambuliaji ambaye kesho ataiongoza timu yake, Simba kuikabili Mwadui FC ugenini kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.

Kocha na mchambuzi wa masuala ya soka nchini, Joseph Kanakafumu alisema Tambwe anayo nafasi kubwa ya kumpita Kichuya na hata kutwaa ufungaji bora kwa sababu ya nafasi yake uwanjani.

“Tambwe ni mshambuliaji halisi, hivyo ana nafasi kubwa ya kufunga mabao mengi tofauti na Kichuya ambaye anacheza kama winga, hivyo anakuwa na majukumu mawili, kufunga mabao lakini pia kutoa pasi kwa wenzake,” alisema Kanakamfumu.