Kiini mitifuano ya Ma-RC, wabunge chatajwa

Dar/Mikoani. Nini kiini cha wateule wa Rais na wabunge kutunishiana misuli?

Hili ndilo swali linalogonga vichwa vya Watanzania kila mara na eneo ambako makundi hayo hayaachi kugongana huku wanasiasa, wasomi na wachambuzi wa siasa wakitaja sababu sita, ikiwamo masilahi binafsi, kuwa ndiyo chanzo.

Mifano wa hivi karibuni wa hali hiyo ni mvutano baina ya Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara na uongozi wa Mkoa wa Mara kuhusu uwekaji alama za mipaka, unaongeza msururu wa migongano hiyo.

Kazi ya uwekaji vigingi vya mipaka kutenganisha vijiji sita vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa), imezua sintofahamu iliyopelekea mbunge huyo kuangua kilio mbele ya wanahabari.

Wakati uzinduzi wa mpango huo Machi 27, Mkuu wa Mkoa wa Mara (RC), Meja Jenerali Suleiman Mzee aliwaonya wanasiasa, akiwemo Waitara, akisema amepata taarifa wanapinga uwekaji wa vigingi na hivyo kuwaonya wanataka kukwamisha kazi hiyo yenye masilahi ya umma.

Onyo hilo lilimwibua Waitara mbele ya wanahabari na kuangua kilio mbele ya kamera akidai programu hiyo inafanyika bila “wananchi wake” kushirikishwa licha ya kupewa ahadi kuwa hilo lingefanyika.

Dhana ya kila upande kupigania masilahi ya wananchi mara nyingine imewekwa mbele ya kila mgogoro unaojitokeza, huku masilahi ya kisiasa ambayo wakati mwingine ndiyo chanzo, yakiwekwa kando.


Baadhi ya mivutano

Mbali na suala la Waitara hali kama hiyo iliwahi kutokea mara kadhaa baina ya aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema na aliyekuwa RC wa Arusha, Mrisho Gambo mfano ilivyotokea wakati wa ujenzi wa hospitali ya mama na mtoto.

Katika ujenzi huo, Lema alisema ameleta wafadhili, Gambo akatumia nafasi yake kuwa juu ya mradi husika.

Mgogoro mwingine ulikuwa ya RC Manyara, Makongoro Nyerere na Naibu Waziri Pauline Gekul baada ya mkuu huyo wa mkoa kumtuhumu Gekul ambaye ni mbunge wa Babati mjini kuchochea mgogoro wa ardhi.

Halikadhalika mwaka jana, Gambo ambaye sasa ni mbunge wa Arusha Mjini (CCM) alipishana kauli na mkuu wa sawa wa mkoa Arusha, John Mongella kuhusu ujenzi wa kituo kipya cha mabasi eneo la Bondeni City jijini Arusha.

Migogoro mingine iliyowahi kusikika ni baina na aliyekuwa RC Dar es Salaam, Paul Makonda na baadhi ya wabunge wa upinzaji jijini Dar es Salaam kama Saed Kubenea (Ubungo) na Halima Mdee (Kawe); pia ile ya aliyekuwa RC Iringa, Ally Hapi na mchungaji Peter Msigwa, aliyekuwa mbunge wa Iringa Mjini.Pia ipo ya aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti na aliyekuwa Mbunge wa Simanjiro (CCM), James Ole Milya kutuhumiana kwa rushwa, mbunge wa zamani wa Hai na mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe na waliokuwa wakuu wa wilaya ya Hai kwa nyakati tofauti, Lengai Ole Sabaya na Gelasius Byakanwa.


Ilitengenezwa kisiasa

Kumekuwa na maoni tofauti kuhusu migogoro hiyo ambayo Dk Faraja Kristomus, mchambuzi wa siasa na masuala ya jamii alisema mingi ilitengenezwa kisiasa.

Alisema baada ya uchaguzi mkuu wa 2015 aliyekuwa Rais wa wakati huo, Hayati John Magufuli alilenga kudhoofisha upinzani kwa kupunguza nguvu za kisiasa za baadhi ya watu mashuhuri wa upinzani.

Alisema kutokana na hali hiyo, ndiyo maana Taifa likashuhudia anguko la wabunge maarufu Joseph Haule (Mikumi), Joseph Mbilinyi (Mbeya) Mbowe (Hai), Lema (Arusha), John Mnyika Kibamba na Halima Mdee (Kawe).

“Hata hivyo baadaye hali ya kisiasa nchini ilibadilika baada ya kifo cha Magufuli Machi 19 mwaka 2021, mwanzoni mambo yalikuwa magumu kwa upande wa upinzani kwani bado mazingira ya kufanya siasa hayakuwa rafiki.

“Mazingira hayakutengeneza ushiriki sawia kwa viongozi wa upinzani na walipojaribu kulazimisha siasa za majukwaani waliingia matatani.

“Hata hivyo, wakati majadiliano ya kuleta mwafaka wa kisiasa yakiendelea, ndani ya CCM mambo hayajawa mepesi,” alisema Dk Kristomus.

Alisema kauli ya Rais Samia aliyotoa siku ya wanawake iliyoandaliwa na Baraza la Wanawake la Chadema(Bawacha) ya kuwa kutakuwepo na wahafidhina kwa pande zote mbili, yaani CCM na Chadema, inadhihirisha kuwa mazingira ya kisiasa nchini yamebadilika sana.

“Sasa hivi tunashuhudia vigogo wa CCM na ndani ya Serikali kutengeneza makundi au kambi kwa ajili ya kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za mitaa mwakani utakaotengeneza mazingira ya kufanikisha uchaguzi wa 2025.

“Kutokana na hali hii, tutegemee vita zaidi kwa makada wa CCM. Wabunge watavurugana sana na wakuu wa mikoa na wilaya huku mawaziri nao wakivurugana na wakuu wa mikoa na viongozi wa CCM mikoa na wilaya,” alisema.

Hata hivyo, wasomi, wanasiasa na wachambuzi wengine waliohojiwa na gazeti hili kuhusu migogoro hiyo na nini kifanyike, walitaja masilahi binafsi kama sababu kubwa ikifuatiwa na katiba na Sheria za nchi kutoweka mipaka kati ya viongozi hao.

Mengine ni kutafuta umaarufu kisiasa, rushwa, mwingiliano wa majukumu majimboni na itifaki ya kimamlaka.

Mtaalamu wa masuala ya uongozi na Utawala, Sekela Kasebele alisema migogoro mingi katika jamii, ikiwemo inayohusisha viongozi wa kisiasa, Serikali na wananchi ni matokeo ya hulka ya binadamu kutafuta kinachomfurahisha na kumnufaisha badala ya uhalisia.

“Kwa mfano, viongozi wa kisiasa na Kiserikali huunga mkono upande ule unaolinda masilahi yao bila kujali ukweli halisi. Kwa ajili ya kura, mbunge hasa nyakati zinazokaribiana na uchaguzi, kama sasa, atakuwa upande wa wananchi,” alisema.

“Atafanya hivyo hata kama kiuhalisia anafahamu kuna makosa, ilimradi apate uungwaji mkono kisiasa. Tabia ya kulinda masilahi ndiyo pia huwasukuma RC na DC kutekeleza lolote linaloamuliwa na Serikali, hata kama ndani ya mioyo yao wanajua si sahihi,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mtandao wa watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema kiini cha tatizo ni uongozi kuteuliwa na uongozi wa wananchi wakati mwingine wanakuwa na masilahi tofauti katika maeneo yao.

“Unakuta mbunge yupo kwa ajili ya kulinda masilahi ya wananchi lakini wakati huohuo RC au DC yeye yuko si tu kulinda masilahi ya wananchi, bali na masilahi mengine. Sasa hapo ndipo migogoro na mivutano hujitokeza baina yao,” alisema

Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut), Dk Kanaeli Kaale alisema wabunge na madiwani hupima upepo wa kisiasa kabla ya kuamua upande wa kuunga mkono pindi mgogoro unapoibuka kati ya wananchi na Serikali.

“Wale wa Serikali ambao ni wakuu wa wilaya na mikoa huangalia msimamo ama wa aliyewateua au maamuzi ya Serikali. Kila mmoja anaangalia na kulinda masilahi yake au kundi lake,” alisema.

Msomi huyo aliwashauri viongozi wote bila kujali mihimili wanayowakilisha, kujenga utamaduni wa kufanya mashauriano ili kupata muafaka wenye masilahi na faida endelevu kwa pande zote kuanzia wao wenyewe, mihimili na wananchi.


Wahusika wafunguka

Mmoja wa wabunge aliyewahi kujikuta katika mivutano kama hiyo ni Kubenea ambaye amesema kuna mambo mengi yanayochangia ikiwemo baadhi ya wateuliwa wa Rais kutofahamu majukumu yao na tabia ya baadhi ya wabunge kujikweza na kujiona wakubwa katika eneo wanaloliongoza.

“Muda mwingine wakuu wa mikoa hawana shida, lakini kikubwa ni tabia za watu binafsi kujikweza na kutoheshimu wenzao. Mfano Gambo kabla ya kuwa mbunge alikuwa mkuu wa mkoa wa Arusha je, alielewana na Lema? Alikuwa mkuu wa wilaya je, alielewana na watu?

“Ukimchukua mtu kama Mongella alikuwa Mwanza hatukusikia purukushani zozote kati ya wabunge wa mkoa ule, sasa huwezi kumlaumu mtu kama Mongella ukasema shida ni RC, bali ni Gambo kutokana na historia.”

Gambo alipotafutwa na Mwananchi simu yake haikupokewa wala ujumbe aliotumiwa kuomba kuzungumza naye haukujibiwa.

Kubenea pia alitoa mfano wa mvutano wa Makongoro na Gekul akisema “namfahamu Gekul vizuri tu, si mtu mwenye ustahimilivu fulani...Lakini mgogoro kati ya Waitara na Mzee shida ni mkuu wa mkoa kutomheshimu mbunge ambaye na yeye anajiona ana sauti kubwa kwa wananchi,” alisema Kubenea.

Kubenea ambaye pia ni mwanahabari alisema ili kuondoka na mivutano hiyo ya mara kwa mara ni vema mamlaka ya wakuu wa wilaya na mikoa yapunguzwe au ikiwezekana nafasi zao ziondolewe ili kuwepo kwa watu watakaochaguliwa.

“Wapunguziwe majukumu, huwezi ukamwambia mtu awe mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama, wakati hajui chochote, ndiyo maana baadhi yao wanatumia vibaya nafasi zao. Kingine kila mtu aheshimu mamlaka ya mwenzake kwa sababu wote sisi ni Watanzania, hakuna sababu ya kugombana,” alisema Kubenea.

Kwa upande wake, Waitara alisema wakuu wa mikoa ni wateule wa Rais hakuna sehemu ambayo wananchi wamependekeza kwamba wanamtaka mkuu wa mkoa fulani na akuwa ndiyo maana baadhi ya maeneo viongozi hao wamegeuka watendaji.

Waitara alisema baadhi yao wakipata maagizo bila ya kuyatafsiri vizuri au kukaa na timu ya watalaamu huyapeleka moja kwa moja kwenye kamati ya ulinzi na usalama ambayo yeye ni mwenyekiti na akizungumza jambo hakuna anayempinga.

“Ifike mahali tuwe na vetting (uchunguzi) nzuri au kanuni fulani hivi unapataje mkuu wa mkoa, ukimkuta mtu ambaye hana busara sana, ndiyo hii mivutano inajitokeza. Mara nyingi wabunge ni wenyeji wa eneo husika, ikitokea mnakinzana kwenye mambo ambayo wananchi wanajua hiki, mbunge hili au mkuu wa mkoa anasema nimeagizwa inabidi mfanye hili, hapo lazima mgogoro uanze.

“Kwa sababu kile ambacho mkuu wa mkoa analazimisha kifanyike unakuta ni tofauti na kile mbunge na wananchi wanajua na walishakubaliana kwenye vikao.Lakini mkuu wa mkoa anakwamba nimetumwa ni maagizo ya Serikali kutoka juu na bahati mbaya ukimwambia tushauriane anakujibu ameshasema,” alisema Waitara.

“Namshauri Rais kwa namna ilivyo hata wabunge wa CCM wengi wanatengenezewa ajali za kushindwa uchaguzi na wakuu wa wilaya au wakuu wa mikoa kwa masilahi binafsi, ni vema akafuatilia kama mbunge analalamika basi aitwe pamoja na mkuu wa mkoa kwenye kikao, tujue nani anakosea na awajibishwe.

“Mbunge hawezi kulalamika hovyo...ukiona alalamika hadharani maana yake maji yamefika shingoni, hakuna namna lazima asema ili wananchi wajue. Ukikaa kimya utahukumiwa watakwambia uliona kuna shida ukakaa kimya, sikupenda kugombana na RC lakini haya mazingira aliyotengeneza hapa,” alisema.


Wanasiasa, wabunge wafunguka

Mkurugenzi wa Itifaki, Uenezi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema sababu kubwa ya migogoro hiyo ni itifaki inayomfanya mkuu wa wilaya kuwa na mamlaka makubwa kuliko mbunge aliyechaguliwa na wananchi.

“Mbunge akitaka kufurukuta anatulizwa na dola. Wabunge hawana sauti majimboni kwao na hawaheshimiwi katika utekelezaji wa programu mbalimbali kwenye majimbo yao lakini wakati uchaguzi ukifika wao ndio wanahojiwa na wananchi.”

“RC au DC yeye hata akiharibu anategemea uteuzi na si kura za wananchi. Wakati mwingine unamkuta RC au DC naye anataka kugombea ubunge, hivyo anamfanyia mbunge fujo makusudi kwa malengo ya kumharibia,” alisema

Mrema alisema suluhusho ni kuwa na viongozi wa kuchaguliwa kwenye ngazi zote kwa nafasi za RC na DC ziondolewe kikatiba, kwa kuwa hao ni makada na ni wajumbe wa kamati za siasa za mkoa au wilaya, hivyo Katiba mpya iwandoe rasmi.

Aliyewahi kuwa Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli alisema ukiona kuna misuguano baina ya wateule na wabunge, baadhi inachangiwa na mgongano katika masilahi binafsi na mara nyingi ikitokea hivyo kiini ni masuala ya rushwa.

“Kwa uzoefu wangu chanzo cha tatizo ni rushwa. Pale ambapo mmoja anahisi mwenzake anataka kumzibia riziki ndiyo tatizo linaanza,” alisema.

“Mimi wakati wangu si DC, DED hata RC sikuwahi kumpa nafasi ya kunisogelea kwani hao mwajiri wao ni Rais wakati mbuge anaajiriwa wananchi. Sikuwapa nafasi ya kuingilia majukumu yangu wala kuingilia utendaji wao,” alisisitiza.

Katibu mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alisema kiini cha misuguano hiyo ni wahusika kutojua mipaka ya nafasi zao na kwamba wateule wa Rais baadhi yao wanajiona bora kuliko waliochaguliwa na wananchi kwenye sanduku la kura..

Kwa upande wake, Mbunge wa Mtera (CCM), Livingston Lusinde alisema kupishana kwa wabunge na wakuu wa mikoa ni jambo la kawaida kwani kila mmoja anapohisi anakandamizwa na mwingine lazima akatae.