Kikwete azitaja kero za umeme, maji na sukari

Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, akizungumza wakati wa utiaji saini mikataba sita ya ujenzi wa majengo 21, ikiwa ni upanuzi na ujenzi wa kampasi mpya za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika mikoa ya Lindi, Kagera, Zanzibar na Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Kikwete amesema Rais Samia amedhihirisha ushupavu katika uongozi katika kushughulikia changamoto.

Dar es Salaam. Wakati kilio cha mgawo wa maji na umeme, na uhaba wa sukari kikiendelea nchini, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, amemtaka Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kuwa imara anapoendelea kutafuta suluhisho la changamoto hizo kwa kuwa ni mambo ya kawaida kwenye uongozi.

Kikwete amesema anachoonyesha Rais Samia katika kipindi hiki,  kinadhihirisha ushupavu wake katika uongozi, akieleza changamoto ni sehemu ya uongozi na utulivu wake unawafanya wananchi pia kuwa watulivu.

Kauli ya Kikwete ameitoa katika kipindi ambacho kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa umeme, maji na sukari, ambayo bei yake imepanda maradufu.

Kikwete ambaye ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), amesema hayo leo Februari 22, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa utiaji saini mikataba sita ya ujenzi wa majengo 21, ikiwa ni upanuzi na ujenzi wa kampasi mpya katika mikoa ya Lindi, Kagera, Zanzibar na Dar es Salaam.

Akitoa shukrani kwa Serikali mbele ya Naibu Waziri wa Elimu, Omari Kipanga, Kikwete amesema chuo hicho kinapata ushirikiano mkubwa kutoka serikalini katika kufanikisha utekelezaji wa mradi huo.

Amepongeza jitihada zinazofanywa na Rais Samia katika kuiletea nchi maendeleo.

“Tunamshukuru Rais Samia kwa uongozi wake tunaona mambo yanaenda vizuri, changamoto ni sehemu ya maisha, kungekuwa hakuna changamoto isingekuwapo haja ya kuwa na viongozi. Changamoto hazitaisha, hata katika mataifa makubwa kama Marekani walipata uhuru 1774 hadi leo hawajamaliza changamoto,” amesema.

“Sasa kweli tunatarajia Tanzania hii kutakuwa hakuna changamoto kabisa? Mara umeme, mara sukari wote tumepitia hayo utasikia kuna hiki mara kile mara kuna EPA hizo zote ni changamoto za uongozi. Uongozi haupoi kama ugali. Uzuri ni kwamba changamoto zinatokea lakini Rais anaonyesha uongozi wenye utulivu katika kukabiliana nazo. Zikitokea changamoto halafu kiongozi ana-panic, wananchi wana-panic zaidi,” amesema Kikwete.

Upanuzi wa chuo

Akizungumzia upanuzi na ujenzi wa kampasi mpya za Udsm amesema ni utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ambao chuo hicho kimepata Dola za Marekani 47 milioni (Sh110 bilioni).

“Nimekuwa nikiufuatilia mradi huu kwa ukaribu na maeneo yote tunayotakiwa kujenga nimeshafika, imechukua muda kidogo kuanza ujenzi kwa sababu kulikuwa na changamoto ambazo tumeshazitatua sasa tunaenda kuanza, hivyo niwasihi makandarasi kuzingatia muda na ubora,” amesema.

Kikwete amesema: “Huu ucheleweshaji ukasababisha maneno kidogo, mfano siku moja nikiwa kule Lindi na mashemeji zangu wakasema wanasikia unafanyika mpango chuo kisijengwe hapa nikawaambia acheni uongo, maana maradhi ya  Watanzania ni uongo. Sijui hiki kirusi tumekipata wapi. Yaani wanaweza kutunga habari ya uongo halafu wakaieneza na wakati mwingine wakataka kuwahukumu watu kwa uongo waliouanzisha ‘which is unfair’ kwa hiyo jamani acheni uongo,” amesema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa William Anangisye amesema  utekelezaji wa mradi wa HEET unafanyika sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025, na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (2020-2025).

Profesa Anangisye amesema kwa pamoja vinalenga kuimarisha uchumi wa viwanda ili kuendana na uchumi wa kati, na kuongeza fursa za ajira kwa makundi mbalimbali, hususan vijana.

“Sisi tunajiona kuwa na bahati kubwa kufikiwa na mradi huu kwani unarandana na dira yetu ya Udsm ‘Vision 2061’ na mpango mkakati wa chuo 2020/21-2024/25 vinavyolenga kufanya mageuzi ya kitaasisi yanayoendana na vipaumbele na mahitaji ya Taifa ya sasa na baadaye,” amesema.

Amesema: “Hivyo utekelezaji wa mradi wa HEET umejikita kuimarisha na kuboresha miundombinu, ikiwemo ukarabati mkubwa na ujenzi wa majengo mapya, na kufunga vifaa vipya kwenye majengo haya. Ni katika muktadha huo, chuo kinajipanua na kuwafikia Watanzania zaidi.”

Mmoja wa makandarasi walioshinda zabuni ya kujenga majengo hayo, Taher Jafferji, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mohammedi Builders Ltd, aliahidi kuikamilisha kazi hiyo ndani ya muda uliopangwa.

Amesema suala la ubora ni kipaumbele chake.