Kituo kilichojengwa hifadhi ya barabara chaundiwa kamati

Muktasari:

  • Wakati kukiwa na malalamiko ya kituo cha mafuta kujengwa kwenye hifadhi ya barabara eneo la Kimara Stop Over, Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), wamesema suala hilo limeenda ngazi za juu.

Dar es Salaam. Wakati kukiwa na malalamiko ya kituo cha mafuta kujengwa kwenye hifadhi ya barabara eneo la Kimara Stop Over, Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), wamesema suala hilo limeenda ngazi za juu.

Julai 2017, takriban nyumba 2,000 zilizokuwa ndani ya eneo la mita 121.5 la hifadhi ya barabara ya Morogoro kuanzia Kimara hadi Kiluvya zilibomolewa kupisha mradi wa ujenzi wa njia nane wenye urefu wa kilomita 19.2.

Hata hivyo, wakati mradi huo ukiwa umekamilika kwa zaidi ya asilimia 95, yameibuka malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi walioondolewa wakihoji kwanini wavunjiwe halafu baadaye kuendelezwe miradi mingine.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao, mwenyekiti wa waathirika wa Kimara - Stop over, Nassor Hamza alisema wanasikitishwa na ujenzi uliofanyika kwa kuwa eneo hilo walikuwa wakiishi wananchi. “Tulivunjiwa na kuambiwa tumevamia bila kulipwa chochote, lakini sisi tulikuwa walipa kodi na huduma zote za kijamii tulikuwa tunapewa. Hili tunaona si sawa,” alisema Hamza.

Alisema wanashangaa kuondolewa na eneo hilo kugeuzwa kuwa la biashara kwa kujenga vituo vya mafuta.

“Kwa kuwa tuliovunjiwa tuko wengi, tumegawanyika makundi. Wapo waliokwenda mahakamani, wapo wanaojipanga kufungua kesi na wengine tunapambana kwa njia nyingine kudai haki yetu,”alisema.

Desemba 24, mwaka huu, Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Kibamba, Earnest Mgawe alipozungumza na waandishi wa habari alisema si sawa Serikali kuwavunjia wananchi, kisha kugeuza maeneo hayo kuwa ya biashara. Alisema chakusikitisha zaidi kilichovunjwa si nyumba za wananchi pekee, bali hata nyumba za ibada, kwani ipo misikiti na makanisa yaliyovunjwa.

Tanroads wafunguka

Akitolea ufafafanuzi suala hilo Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Haruna Senkuku alisema baada ya Tanroads kuvunja nyumba hizo haina maana maeneo hayo yanatakiwa kubaki wazi, bali kuna mambo yanayotakiwa kufanyika lakini si ya kudumu.

“Hivi vituo vya mafuta vinavyowekwa ikiwemo hiki kimoja kinachoitwa Rupeez, viko kwenye dizaini ya barabara hiyo kwa maana baada ya ujenzi wa barabara na kuondoa nyumba kuna vitu ambavyo tutaruhusu viwepo.

“Suala ambalo mkuu wa mkoa amelikazania ni kufanya yale maeneo yasiwe vichaka, lakini limechukua mwelekeo ambao kidogo unahitaji mjadala na limefika ofisi za juu, nisingependa nilitolee uamuzi sasa hivi hadi pale kamati iliyoundwa itakapotoa majibu,” alisema Senkuku.

Alieleza kituo hicho hakijengwi kana kwamba pamevamiwa, vitajengwa vingi kwa kufuata mfumo wa Tanroads na katika mkataba utakaoingiwa kitakuwa ni kituo cha muda, ili siku Serikali itakapohitaji eneo lake iweze kulichukua.