‘Kutosajili ndoa chanzo cha migogoro ya mirathi’
Muktasari:
- Waziri wa Katiba na Sheria Dk Juma Homera amesema Serikali iko mbioni kufanya mapitio ya baadhi ya sheria ikiwemo sheria ya ndoa ili kutoa nafasi kwa Watanzania kupunguza changamoto zinazowakabili, hususani wanawake
Dodoma. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema moja ya changamoto kubwa inayojitokeza katika migogoro ya ndoa ni masuala ya mirathi, yanayotokana na watu wengi kutokuwa na uthibitisho halali wa ndoa zao.
LHRC imeeleza kuwa waathirika wakubwa wa hali hiyo ni wanawake.
Kwa mujibu wa taasisi hiyo, chanzo cha migogoro hiyo ni masharti ya Sheria ya Usajili wa Ndoa, ambayo yanawataka wanandoa kusajili ndoa zao ndani ya siku 30 baada ya kuzifunga.
Hata hivyo, utekelezaji wa sharti hilo umekuwa changamoto kwa wakazi wengi wa vijijini, ambao mara nyingi hukosa fursa ya kusajili ndoa zao kwa wakati.
Wakati hali hiyo ikiendelea, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Juma Homera amesema Serikali iko katika hatua za kufanya mapitio ya baadhi ya sheria, ikiwemo Sheria ya Ndoa, ili kupunguza changamoto zinazowakabili Watanzania, hususan wanawake.
Dk Homera ametoa kauli hiyo wakati akitangaza uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Awamu ya Pili kwa upande wa Zanzibar.
Amesema kampeni hiyo itajikita pia katika kutoa msaada wa kisheria kwenye masuala ya ndoa na mirathi.
Akizungumza jana jijini Dodoma katika kikao kilichowakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo mawakili wa Serikali, Meneja wa Uchechemuzi wa LHRC Mkoa wa Dodoma, Raymond Kanegene, amesema ukosefu wa elimu kuhusu sheria za ndoa na mirathi unaendelea kuwanyima wananchi haki zao na kusababisha familia nyingi kuishi katika mazingira magumu, hata pale wazazi wao walipokuwa na uwezo mzuri wa kiuchumi.
Kanegene alisema LHRC imekuwa ikipokea malalamiko mengi yanayotokana na wananchi kutofahamu taratibu za kisheria zinazohusu ndoa na urithi.
Alitolea mfano kesi ya mwanamke mmoja aliyekuwa ameishi katika ndoa ya kimila kwa miaka mingi na kupata watoto na mume wake, lakini alishindwa kupata haki zake za urithi baada ya mume huyo kufunga ndoa nyingine iliyokuwa imesajiliwa na kutambulika kisheria.
Kanegena alisema matukio ya aina hiyo yanaonesha umuhimu wa kuongeza elimu ya sheria kwa wananchi pamoja na kufanya maboresho ya sheria ili kulinda haki za wanawake na watoto.
“LHRC hupokea zaidi ya malalamiko 3,000 kila mwezi yanayohusu masuala mbalimbali ya kisheria na kati ya hayo, mengi yanatokana na migogoro ya ndoa na mirathi lakini ukiangalia chanzo ni wengi kutokuwa na uhalali katika usajili wa ndoa zao,” alisema Kanegene.
Hata hivyo, mwakilishi wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Emmanuela Mwingira amesema wanandoa wengi huamini kuwa kufunga ndoa kanisani, msikitini au kwa kufuata mila kunatosha bila kujua “hakuna ndoa kama hakuna usajili”.
Mwingira anasema watu wengi wanaamini wako ndani ya ndoa lakini ukweli unabaki kuwa wanaishi na vimada si ndoa, hivyo likitokea jambo lolote miongozi mwao, huweza kusababisha changamoto wanapohitaji huduma zinazohitaji uthibitisho wa ndoa.
“Hakuna namna kwamba mtu anaweza kujificha kwenye jambo lolote, bila usajili wa ndoa hiyo siyo ndoa kabisa, hili wananchi wanapaswa kulitambua na usajili wa ndoa sheria inataka iwe ndani ya siku 30, mtu akizidisha hapo anakuwa nje ya utaratibu,” anasema Mwingira.
Kanegene amesema changamoto kubwa zaidi hujitokeza kwenye ndoa za kimila, ambazo mara nyingi hazisajiliwi kwa mujibu wa sheria na hivyo kusababisha migogoro ya mirathi na haki za wanandoa pindi mmoja wao anapofariki dunia.
“Ili kuwa na ndoa inayotambulika sharti mhusika awe amefunga ndoa ya kanisani, Bakwata au hata ndoa ya bomani hizo zinakuwa zimesajiliwa moja kwa moja, kwani vyeti vyao vinatoka serikalini, cha msingi watoa huduma watoke Taasisi zilizosajiliwa.
Hata hivyo, ameeleza kuwa changamoto zinaweza kujitokeza pale ndoa zinapofungwa katika baadhi ya nyumba za ibada ambazo hazina usajili unaotambuliwa kisheria, hali inayoweza kuwaathiri wanandoa na warithi wao baadaye.
Amezitaja ndoa zinazopata changamoto ni zilizofungwa kimila au zile zilizopitia nyumba za ibada zisizo na usajili.
Hata hivyo, Mwingira anasema wanandoa waliofunga ndoa kimila miaka mingi iliyopita wanaweza kuzisajili kwa kufuata taratibu zinazotolewa na mamlaka husika, hasa kwa kuzingatia mazingira ya nyakati na maeneo wanayotoka.
Wakili Hidaya Haonga kutoka LHR, amesema pamoja na changamoto wanazokutana nazo, Serikali inapaswa kuzitazama baadhi ya sheria ili kuzifanyia marekebisho, huku akisisitiza utekelezaji wa hukumu mbalimbali za mahakama zinazolenga kulinda haki za wananchi.