Mabadiliko yawa chachu ongezeko la wawekezaji katika miezi miwili

Friday June 11 2021
wawekezaji pic
By Ephrahim Bahemu
By Tuzo Mapunda

Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa uwekezaji mpya hapa nchini umeongezeka katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, sababu ikitajwa ni kubadilika kwa mtazamo wa Serikali kuhusu uwekezaji na sekta binafsi kwa jumla.

 Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Profesa Godius Kahyarara aliliambia gazeti hili juzi kuwa licha ya uwepo wa changamoto ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona, kuna wawekezaji wapya kwa wastani wameongezeka hapa nchini.

“Katika kipindi cha miezi miwili kati ya Machi na Mei, Kituo cha Uwekezaji cha Taifa (TIC) kimeweza kuandikisha miradi mipya 59, jambo ambalo ni ongezeko karibu mara mbili ya mwaka jana kwa muda kama huo,” alisema Kahyarara.

Alisema thamani ya miradi iliyoandikishwa katika kituo hicho imeongezeka kwa asilimia 500 kutoka Dola milioni 189 za Marekani (Sh437.5 bilioni) kwa kipindi kama hiki mwaka jana hadi Dola milioni 965 za Marekani (Sh 2.23 trilioni) kipindi hiki.

“Maombi ni mengi katika sekta kuu za ‘Special Economic Zones’ (maeneo maalumu ya kiuchumi), viwanda, kilimo, teknolojia na usafirishaji (Industrial Parks Agricultural Parks and Technology Parks),” alisema.

Profesa Kahyarara alisema mazungumzo na uhakiki yanaendelea katika maeneo hayo kwa kuwa ni miradi ya mitaji mikubwa na inayotumia mabilioni ya dola na inahitaji ardhi yenye sifa fulani.

Advertisement

Pia, alisema Serikali imepokea malalamiko ya wawekezaji 26 ambao wengine walikuwa wanasubiri mchakato na alitafsiri hatua hiyo kama mwitikio wa wawekezaji kutokana na wito wa Rais.

Profesa Kahyarara alisema siri ya mafanikio ni imani waliyojengewa wawekezaji na kama mambo yataendelea kwenda vizuri miaka mitano ijayo Tanzania itakuwa nchi yenye uchumi mkubwa kupitia uwekezaji, akisema Pwani na Dar es Salaam itajaa.

Hivi karibuni katika moja ya mikutano na wawekezaji, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dk Godwill Wanga alisema uwekezaji unategemea zaidi mazingira na hivi sasa kuna utashi wa kisiasa wa kuweka mazingira mazuri.

“Wawekezaji hufuatilia na kusikiliza kauli za wakuu wa nchi, kauli iliyotolewa na mkuu wetu wa nchi juu ya uwekezaji na inatoa imani ya kufanya uamuzi na kuwa Tanzania ni eneo zuri la kuwekeza,” alisema Dk Wanga.

Pia, aliongeza suala la Serikali ya Rais Samia kupigia chapuo uwekezaji katika ukanda maalumu wa kiuchumi nalo limekuwa kivutio cha wawekezaji, kwa kuwa wanajua huko hakuna kutozwa kodi mara mbilimbili.

“Kauli yake kuwa anafungua nchi katika uwekezaji imeongeza imani kwa watu, lakini pia suala la kutoa vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi,” alisema Dk Wanga.

Tangu aingie madarakani, Rais Samia Suluhu ameonyesha kuwa muumini wa biashara na uwekezaji na katika hotuba zake kadhaa amekuwa akitoa hakikisho kwa wafanyabiashara kuhusu mazingira ya kikodi na yasiyo ya kikodi.

Mwelekeo huo wa Rais Samia ulianza kuonekana Machi 31 wakati wa kuapishwa kwa Makamu wa Rais, Dk Philipo Mpango ambapo alitoa mwelekeo wa Serikali yake katika masuala ya kodi, jambo ambalo jumuiya ya wafanyabiashara walilitafsiri kama zawadi kwao.

“Sasa wale mnaowakamua na kuchukua vifaa vyao vya kazi na kufungia akaunti zao, mkachukua pesa kwa nguvu kwenye akaunti kisa sheria inakuruhusu kufanya hivyo, akitoka hapo anakwenda kufunga biashara anahamia nchi ya pili mnapunguza walipa kodi,” alisema Rais Samia.

Mbali na hatua hiyo, katika hotuba yake ya kwanza bungeni Aprili 22, Rais Samia aliweka wazi dhamira yake ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kuchukua hatua mahususi katika sera na sheria kwa kutoa vifungu vinavyosababisha vikwazo vya kukuza uwekezaji.

Advertisement