Mamia wajitokeza kumuaga Dk Kamala

New Content Item (1)

Mke wa marehemu Dk Kamala, Adelaida Kamala akiaga  mwili wa mumewe, baada ya kumalizika kwa Ibada ya kuaga mwili huo, iliyofanyika  katika kanisa la Mwenyeheri Isidori Bakanja, Boko jijini  Dar es Salaam. Picha na Nasra Abdallah

Muktasari:

  • Dk Kamala alifariki dunia Februari 12, 2024 katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu. 

Dar es Salaam. Mamia ya waombolezaji wamejitokeza jijini hapa katika ibada ya kuuaga mwili wa mbunge wa zamani wa Nkenge, na aliyewahi kuwa waziri wa Afrika Mashariki, Dk Diodorus Kamala.

Dk Kamala alifariki dunia Februari 12, 2024 katika Hospitali ya Mzena jijini hapa alikokuwa akipatiwa matibabu.

Maziko yanatarajiwa kufanyika Jumanne wiki ijayo kijiji kwao Bwanjai wilayani Nkenge mkoani Kagera.

Ibada hiyo iliyoanza saa tano asubuhi  hadi saa nane mchana, imefanyika leo Jumamosi Februari 17, 2024 katika Kanisa Katoliki la Mwenyeheri Isdori Bakanja, lililopo Boko, jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya waombolezaji waliojitokeza walipata nafasi ya kutoa salamu za rambirambi.

Akitoa salamu hizo  aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Francis Nanai, amesema alifahamiana na Dk Kamala miaka ya 1980 walipokuwa wanasoma Shule ya Sekondari Ikongi iliyopo wilayani Bukoba mkoani Kagera.

"Enzi hizo wakati tunasoma, Dk Kamala alikuwa ni mtu mwenye bidii kwa kila anachokifanya na hakupenda kushindwa kirahisi rahisi hivyo kuwa mfano kwa wanafunzi wengi waliotaka kupata mafanikio katika maisha yao," amesema.

Balozi Anthony Cheche, aliyewahi kuhudumu Ubelgiji, ambako Dk Kamala aliwahi kufanya kazi akiwa balozi amesema kwao hakuwa tu bosi bali mwalimu na rafiki.

Balozi Cheche amesema ni kutokana na hilo, hata alipoondoka yeye alijikuta akiteuliwa kurithi nafasi yake ya ubalozi wa Ubelgiji na ofisa mwingine aliyemtaja Balozi Agnes Kayota naye akachaguliwa kuwa Balozi wa Malawi, wote wakiwa wameiva chini ya mikono yake. 

"Balozi Kamala pia alikuwa mkarimu kwa watu wote kwani bila kujali wadhifa wake mara nyingi alitualika na kujumuika nasi  nyumbani kwake na hukuwa akionyesha kuwa yeye ni tofauti na anaowaongoza, hivyo kutufanya tujisikie tupo nyumbani," amesema Balozi Cheche ambaye kwa sasa ni mstaafu.

Makamu Mkuu wa Chuo cha Mzumbe, Profesa Willium Mwegoha, ambako Dk Kamala alikuwa akifanya kazi mpaka mauti yalipomfika, amesema kwao hakuwa tu mwalimu bali ni mwanafamilia.

Profesa Mwegoha ameeleza kabla ya Dk Kamala kuwa Mhadhiri Mwandamizi katika chuo hicho, alianza kufundisha akiwa na umri mdogo lakini pia alisoma hapo na alikuwa mmoja wa viongozi wa serikali ya wanafunzi.

"Hivyo suala la uongozi lipo ndani yake tangu akiwa mdogo na ndiyo maana aliweza kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani na nje ya nchi, kwetu sisi wana-Mzumbe tutaendelea kumuenzi kwa uchapakazi wake," amesema Makamu Mkuu huyo wa chuo.

Padri Richard Tiganya, aliyeongoza misa aliwataka waombolezaji kuhakikisha wanapoishi nyakati zote wanakuwa karibu na Mungu kwa kuwa kifo kaandikiwa kila mtu isipokuwa tofauti ipo kwenye siku na muda.

"Ukiacha ukaribu na Mungu, pia mpende kuwa watu wa kujitolea kwa kuwa mmoja wa waombolezaji waliofika hapa ametoa ushuhuda kuwa Dk Kamala aliwahi kuwapa ng'ombe, na wao leo wamerudisha ng'ombe itakayoliwa katika shughuli yake ya maziko," amesema.

Awali akisoma wasifu wa Dk Kamala, mtoto wake, Ketty Kamala amesema baba yake alizaliwa Novemba 26, 1968 Kijiji cha Nkenge, Mkoa wa Kagera na kupata elimu katika ngazi na fani mbalimbali.

Katika maisha yake aliwahi kuwa mbunge wa Nkenge kuanzia mwaka 2000 hadi 2010 na mwaka 2006 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Afrika Mashariki na baadaye Waziri kamili mwaka 2008 hadi 2010.

Mwaka 2011 aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Uholanzi ambako alitumikia nafasi hiyo hadi mwaka 2015 aliporejea kuwa mbunge hadi mwaka 2020 na baadaye kurudi kufundisha Chuo cha Mzumbe.

Mwili wabebwa na wahadhiri wenzake

Jeneza lenye mwili wa Dk Kamala lilibebwa na wahadhiri wenzake wakati wa kuingizwa na kutolewa kanisani.

Wahadhiri hao wapatao 20 waliokuwa wamevaa majoho wakati wa kutoka kanisani walisukuma jeneza taratibu mpaka lilipo gari maalumu wa kuubebea kuingiza kwenye gari.