Mamilioni yanavyochangwa fomu urais wa Samia

Rais Samia Suluhu Hassan, akihutubia katika mkutano mmojawapo wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Muktasari:

  • Zaidi ya Sh130 milioni zimekwisha changwa ili kugharamia fomu ya urais ndani ya chama ili hatimaye apitishwe. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amezungumzia hicho kinachoendelea.

Dar es Salaam. Wakati vuguvugu la uchaguzi mkuu mwakani likiendelea chini kwa chini, baadhi ya makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamemchangia Rais Samia Suluhu Hassan zaidi ya Sh130 milioni kwa ajili ya kuchukua fomu kugombea urais ndani ya chama chake.

Kwa nyakati tofauti tangu ameingia madarakani Machi 19, 2021, viongozi na makada wa chama hicho wamekuwa wakihamasisha kuwa na fomu moja ya mgombea urais ndani ya  CCM, wengine wakijitokeza kuchangisha fedha kwa ajili ya kulipia fomu hiyo.

Ikiwa CCM itampitisha mwakani kugombea urais, itakuwa mara yake ya kwanza kusimama kupeperusha bendera ya chama hicho tawala. Katika uchaguzi mkuu 2020 alikuwa mgombea mwenza wa Dk John Magufuli.

Dk Magufuli na Samia waliibuka washindi. Hata hivyo, Dk Magufuli hakuendelea  hadi mwisho wa awamu yake ya pili. Alifariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyama, Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu ya moyo.

Tangu awe Rais, makada na viongozi waandamizi wa chama hicho wamekuwa wakisema hakuna haja ya kujitokeza kuchukua fomu kuwania kupitishwa na CCM bali Rais Samia anatosha na hilo linaenda sambamba na uchangiaji fedha.

Tayari zaidi ya Sh135 milioni zimechangwa sababu ikielezwa wameridhishwa na utendaji wa Rais Samia.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamekuwa na mitazamo tofauti kuhusu uchangiaji huo.

Wapo wanaoeleza kitendo hicho ni sawa na kujipendekeza kwa kiongozi huyo ili kuonekana wema, huku wengine wakiona anafaa ndiyo maana wakajitosa kumchangia.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amesema anaendelea kuchungulia chungulia kwani kwa nafasi yake si muda mwafaka kuzungumzia jambo hilo.


Viongozi na fomu moja

Wakiwa kwenye mkutano mkuu wa CCM wilaya ya Ruangwa, Januari 2, 2024, mjumbe wa kamati kuu ya CCM na mbunge wa Ruangwa na  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM -Bara, Abdulrahman Kinana walisisitiza haja ya kuwa na fomu moja kwa ajili ya Rais Samia.

Majaliwa alisema Rais Samia amekuwa kielelezo cha mafanikio makubwa yanayofikiwa nchini, hivyo watawashauri wajumbe wengine wa kamati kuu na halmashauri kuu, watoe fomu moja kwa Rais Samia.

“Na mimi sikosei, mbele ya wajumbe wenzangu hawa kusema kuwa mheshimiwa makamu mwenyekiti, vyovyote itakavyokuwa, tunaomba tushauri kule kamati kuu na halmashauri kuu tutoe fomu moja tu ya (Rais) Samia Suluhu Hassan mwaka 2025 kama mgombea pekee wa CCM,” alisema Majaliwa.

Kwa upande wake, Kinana alisisitiza jambo hilo kwa kueleza chama hicho kina utamaduni wake ambao wangependa kuona ukiendelezwa. Ni utamaduni wa kiongozi aliye madarakani kuachwa aendelee kuongoza.

“Rais Samia yuko awamu ya kwanza. Kwa nini asiwe na awamu ya pili? Tuna sababu, hatuna? Kwa hiyo, kama kuna wengine watajitokeza kwa vyama vingine Katiba ya nchi inaruhusu, lakini kwa CCM tunazingatia utamaduni wetu wa CCM, hakuna anayeweza kumzuia. Yupo?  hakuna,” alisema.


Sh135.8 milioni zachangwa

Kazi ya uchangishaji fedha kwa ajili ya fomu ya Rais Samia ilifanyika Machi 10, 2024 kwenye Kongamano la Wanawake lililofanyika ukumbi wa Diamond Jubilee Dar es Salaam, Waziri Mkuu Majaliwa akiongoza uchangishaji huo uliowezesha Sh120 milioni kupatikana.

Wazo la kuchanga fedha hizo lilianzia kwa mjasiriamali aliyeshiriki kongamano hilo lililokusanya wanawake kutoka maeneo mbalimbali nchini

“Naomba nitoe taarifa fedha ambayo imeratibiwa hapa na ile ambayo ilipatikana tangu mwanzo imefanya kuwa na Sh120 milioni, ndiyo mchango ambao kina mama mmeweza kuchangia mchana huu,” alisema Majaliwa.

Machi 26, 2024 Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT) chini ya Mwenyekiti wake, Mary Chatanda ulikabidhi Sh2 milioni kwa Katibu wa NEC, Idara ya Oganaizesheni ya CCM Taifa, Issa Gavu ukiwa ni mchango kwa ajili ya Rais Samia kuchukua fomu kuwania urais.

Februari, mwaka huu, kuelekea maadhimisho ya miaka 47 ya kuzaliwa kwa CCM, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana ya chama hicho (UVCCM), Mohammed Ali maarufu Kawaida, kwa niaba ya jumuiya hiyo, walimuunga mkono Rais Samia kwa kutoa Sh1 milioni kwa ajili ya fomu hiyo.

Fedha hizo zilikabidhiwa kwa Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango mkoani Kigoma ambako kulifanyika kongamano la kumpongeza Rais Samia kwa kazi anazozifanya.

Januari 20, 2024 wakati wa ziara ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda mkoani Tanga, mwenyekiti wa chama hicho mkoani humo, Rajab Abdulrahman alitangaza kwenye mkutano wa hadhara wa Makonda kutoa Sh1.7 milioni.

Katika ya hizo, Abdulrahman alichangia Sh1 milioni, huku mbunge wa Tanga, Ummy Mwalimu akichangia Sh600,000 na iliyobaki ikichangwa na viongozi wengine wa CCM mkoani humo.

Arusha nako, Januari 22, 2024 baadhi ya wadau wakiwemo wanaojiita ‘machalii wa Chuga’ na viongozi wa jamii ya Kimasai walichangia zaidi ya Sh2.4 milioni.

Machifu wa Mkoa wa Kilimanjaro pia walitoa fedha taslimu kwenye bahasha, kiasi walichochangia hakikuwekwa wazi.

Januari 10, mwaka huu mkoani Dar es Salaam, machifu walichangia Sh1.5 kwa ajili ya Rais Samia kuchua fomu, kiasi kilichopokewa na Waziri wa Michezo na Utamaduni, Dk Damas Ndumbaro.

Desemba 19, 2023 mkoani Mwanza, Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (Tahossa), walichangisha Sh3 milioni.

“Tumeamua kuvunja rekodi tangu kuumbwa kwa ulimwengu, kwa sisi wakuu wa shule kuamua kuchangisha fedha, kampeni hii inajulikana ‘Kapu la Mama’ lengo ni kumuunga mkono Rais Samia kwa kazi nzuri anayofanya,” alisema mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Muhange, Zamoyoni Uzale ambaye ni mhazini wa Tahossa.


Maelezo ya Dk Nchimbi

Alipotafutwa kuzungumzia kiasi kilichokusanywa, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amesema kwa nafasi yake, sasa si muda mwafaka kuzungumzia jambo hilo.

“Mimi ni mtu wa mwisho kujua, sasa hivi bado wako ngazi ya chini. Nakuwa wa mwisho kabisa mchakato rasmi wa kuchukua fomu utakapokuwa umeanza,” amesema.

Amesema kipindi cha mchakato wa kuchukua fomu kikianza kwa mujibu wa taratibu za chama hicho, ataliweka bayana kwa kulitangaza suala hilo hadharani baada ya kukabidhiwa kiasi hicho kama mtendaji wa chama.

“Sasa hivi na mimi nafanya kazi ya kuchungulia tu watu wanavyochangia, lakini naamini kutokana na mwamko ulivyo, michango itakuwa mingi tu,” amesema.


Maoni ya wachambuzi

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa waliozungumza na Mwananchi wamesema kitendo cha watu, wakiwemo viongozi wa CCM kutoa fedha kuwezesha Rais Samia kuchukua fomu,  ni sawa na kujipendekeza kwa kiongozi huyo ili kuonekana wema.

Wamesema wanachopaswa kufanya makada wa chama hicho ni kumsaidia Rais Samia katika kuhakikisha wanakijenga chama hicho katika ngazi ya chini,  ili iwe rahisi kwa mwenyekiti wao kupata kura nyingi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Wakili Rainery Songea amesema hadhani kama Rais Samia atashindwa kulipia fomu hiyo, bali ni michezo ya kisiasa na wanaofanya hivyo wana malengo yao, ikiwemo kujipendekeza na kujiweka karibu na chama au Rais.

“Siamini kama Rais atashindwa kulipia au kukwama kuchukua fomu ya urais hata iwe bei gani, wanatumia huo mwanya kwa ajili ya kujiweka karibu na Mama (Rais Samia) au kujionyesha kama wapo. Si unajua katika siasa la muhimu ni kujulikana na kujionyesha itategemea na njia utakayoitumia,” amesema.

Mchambuzi mwingine, Ali Makame amesema wanaofanya hivyo wana lengo la kujipendekeza kwa Rais na ni ushawishi uliopitwa na wakati kwa wana-CCM kujionyesha wanamjali mwenyekiti wao.

“Anayempenda Mama afanye majukumu ya chama ili kila mmoja aone hawa kweli wanafanya kazi ya chama, si kusema tukamchukulie fomu. Kuna mashambulizi yanayotolewa na baadhi ya vyama vya upinzani, wanachotakiwa ni kuwajibu kwa vitendo, ili kumsaidia mwenyekiti wao wafanye yale yanayokera watu,” amesema.

“Wenyeviti wa mikoa wanatakiwa kuwaunganisha Wana-CCM na Watanzania, sambamba na kufichua maovu yanayofanywa ili wananchi wajenge imani na chama chao kuanzia ngazi ya chini hadi mkoa, lakini ukiangalia kila mkoa aliopita Makonda, watu wanashindwa kupeleka shida zao katika ofisi husika, wakihisi hazitafanyiwa kazi,” amesema Makame.


Alichokisema Wassira

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira amesema falsafa za 4r za Rais Samia (maridhiano, mageuzi, ustahimilivu na kujenga upya taifa) zimefanikiwa katika kuleta juhudi za pamoja.

Wasira ambaye ni waziri wa zamani katika utawala wa awamu ya kwanza, pili, tatu na nne alieleza hayo hivi karibuni katika kipindi cha twende pamoja kinachorushwa na televisheni ya Channel 10, kilichoangazia miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya sita na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na utoaji wa huduma za jamii.

Alisema moja ya maeneo yaliyokuwa yakilalamikiwa na vyama vya siasa ni kwamba mfumo wa uchaguzi hauna uhalali, lakini miswada mitatu iliyopelekwa bungeni na wabunge kujadili, kisha Rais Samia kusaini kama sheria imejibu malalamiko yao.

“Huko nyuma mikutano ya hadhara ilikataliwa, Rais akasema waache wafanye, wengine wakasema haitoshi wanataka kufanya maandamano, Rais akasema waache waandamane na polisi wawasindikize,” alisema Wasira ambaye ni mbunge wa zamani wa Bunda mkoani Mara.

Kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, Wasira alisema CCM inaelekea kushinda kwa sababu ya kazi kubwa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ya maji chini ya Rais Samia.

“Tuna hoja na jambo la kuwaambia Watanzania, sababu za kuendelea kuongoza tunazo, wenzetu wanaotaka kututoa wana zao, tutazipeleka kwa wananchi. Katika CCM hatuna tatizo kubwa nimesikia baadhi ya wenzangu wanasema mwaka tuchape fomu moja, tutaingia gharama tu ya nini kuchapa fomu wakati mgombea tunaye.

“Sio kwa hisia kwa utamaduni, utamaduni wa CCM ukiwa Rais ukimaliza awamu ya kwanza, unaelekea ya pili kwa mujibu wa Katiba na unakuwa mgombea, hakuna mwana-CCM anayesema anataka fomu, kama yupo tumwambie kwamba hakuna fomu, tunakwenda kamati kuu na mgombea wetu ambaye ni mwenyekiti,’’alisema.

Hata hivyo, Wasira alisema kwa vile katibu mkuu (Dk Emmanuel Nchimbi) yupo ataamua kama kuchapa fomu moja au la ushauri wangu kwake hakuna haja ya fomu kwa sababu wana-CCM hawana mpango wa kuichukua kwa sababu sio utamaduni wao.

“Unachapa fomu ya nini ili uingie gharama? Maana ni gharama kuliko kuchapa fomu nyingi,” alisisitiza.


Imeandikwa na Peter Elias, Tuzo Mapunda na Bakari Kiango.