Majaliwa, Kinana wataka CCM itoe fomu moja ya Urais kwa Samia

Muktasari:

  • Mkutano Mkuu Maalum wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Ruangwa, Mkoa wa Lindi umefanyika huku Mbunge wake ambaye pia ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara Abdulrahman Kinana wamezungumzia ubora wa Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan kuwa anatosha kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Ruangwa. Mbunge wa Ruangwa (CCM), Kassim Majaliwa amesema maendeleo yanayofanyika jimboni humo chini ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan yanawafanya kushawishi vikao vya juu ya chama hicho kutoa fomu moja tu ya urais ndani ya chama katika uchaguzi mkuu 2025.

Majaliwa ambaye pia ni Waziri Mkuu, amesema hayo leo Jumanne, Januari 2, 2025 kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM wa Wilaya ya Ruangwa uliofanyika Uwanja wa Likangara.

Lengo la mkutano huo ni kuelezea utekelezaji wa Ilani ya CCM ndani ya Jimbo hilo na mgeni rasmi alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara Abdulrahman Kinana.

Katika maelezo yake, Majaliwa amesema: “Na mimi sikosei, mbele ya wajumbe wenzangu hawa kusema kuwa mheshimiwa makamu mwenyekiti, vyovyote itakavyokuwa, tunaomba tushauri kule kamati kuu na halmashauri kuu tutoe fomu moja tu ya (Rais) Samia Suluhu Hassan mwaka 2025 kama mgombea pekee wa CCM.

Tukiwa na uhakika haya yanayofanyika leo, maajabu tunayaoyaona yataendelea na sisi Wanaruangwa tutanufaika.”

Majaliwa amesema Rais Samia amekuwa kielelezo cha mafanikio makubwa yanayofikiwa nchini, hivyo kuliwezesha Taifa kuendelea kupata utulivu, maelewano na kasi kubwa ya maendeleo kupitia maono, maelekezo na mipango mbalimbali.

“Sisi wana-Ruangwa tunatoa shukurani za dhati kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia na kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa wilayani na Kitaifa. 

Kwa hakika Rais amekuwa kielelezo cha misingi ya uongozi na utawala bora, hivyo sisi wana – CCM  tunaendelea kutembea kifua mbele na tunamuhakikishia mazingira aliyoyaweka yatatuwezesha kushinda chaguzi zote za serikali za mitaa mwaka huu na zile za Uchaguzi Mkuu za mwaka 2025,” amesema

Majaliwa ametaja baadhi ya masuala makubwa ya kitaifa yaliyofanywa na Rais Samia tangu alipoingia madarakani ni pamoja na kuendeleza miradi ya kielelezo na ya kimkakati ukiwemo ujenzi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere, ujenzi wa wa Reli ya Kisasa na madaraja makubwa likiwemo la Kigongo - Busisi ili kukuza uchumi, kuongeza fursa za ajira na kufikia malengo yaliyokusudiwa katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Amesema mafanikio mengine ni kurejesha taswira ya Tanzania katika medani za kimataifa na kuimarisha diplomasia ya uchumi:“Kwa kufanya hivi Rais, amefungua fursa mbalimbali ukiwemo uwekezaji, mitaji, masoko ya bidhaa, ongezeko la watalii, kubidhaisha lugha ya Kiswahili na utatuzi wa changamoto za kibiashara na nchi jirani.”

Pia, amesema Rais Samia, ameiwezesha nchi kuwa na mtangamano wa kisiasa unaojumuisha siasa safi, za kistaarabu na zinazoheshimu mawazo ya kila mmoja wetu.

Hatua ambayo imefanya hali ya siasa nchini kuwa tulivu chini ya sera ya upatanishi, ustahimilivu, mageuzi na ujenzi wa nchi aliyoipa jina la 4R (Reconciliation, Resilience, Reform and Rebuilding), kwa Kiswahili ni Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Ujenzi wa Taifa.

Katika hatua nyingine,  Majaliwa ametaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana wilayani Ruangwa tangu Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani ni pamoja na uboreshwaji wa huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za afya, elimu, maji, miundombinu ya barabara na kilimo na hivyo kuwawezesha wananchi kupata maendeleo.

Akizungumzia huduma za afya, Majaliwa amesema Serikali imewezesha ujenzi wa hospitali ya wilayaujenzi wa vituo vya afya vipya vinne katika Kata za Malolo, Nangurugai, Narungombe na NamichigaUjenzi wa zahanati mpya tisa za Namungo, Mbangara, Muhuru, Namkatila, Mkaranga, Mihewe, Lipande, Mkutingome na Mtakuja na hivyo kuwawezesha wananchi kupata huduma karibu na makazi yao na kwa wakati.

Mgeni rasmi katika mkutano huo Kinana pamoja na kuzungumza masuala mbalimbali aligusia Uchaguzi Mkuu 2025 akisema licha ya Rais Samia kuwa na sifa za utekelezaji wa Ilani na kukubalika kwa wananchi, utamaduni wa chama hicho utazingatiwa na kwamba sio dhambi wana CCM kuridhika naye.

“Utamaduni tulionao, Rais anapokuwa kwenye awamu ya kwanza, huwa tunapenda aendelee kwenye awamu inayofuata, kweli sio kweli.” amesema Kinana akitoa mfano kwa kutaja marais waliotangulia kutumia utamaduni huo tangu awamu ya tatu chini ya Hayati Rais Benjamini Mkapa.

“Rais Samia yuko awamu ya kwanza. Kwanini asiwe na awamu ya pili? Tuna sababu?, hatuna. Kwa hiyo, kama kuna wengine watajitokeza kwa vyama vingine Katiba ya nchi inaruhusu lakini kwa CCM tunazingatia utamaduni wetu wa CCM, hakuna anayeweza kumzuia. Yupo? , hakuna,” amesema