Mchango wa elimu Songea wafananishwa na kodi ya kichwa

What you need to know:

Juzi, manispaa hiyo ilibandika tangazo kueleza nia ya kutunga sheria ndogo kuanzisha Bodi ya Mfuko wa Elimu ambao kila mwananchi atachangia Sh10,000 kwa mwaka.

Songea. Wananchi wamepinga mchango wa Sh10,000 kwa ajili ya mfuko wa elimu wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wakiufananisha na kodi ya kichwa iliyofutwa miaka mingi na Serikali.

Juzi, manispaa hiyo ilibandika tangazo kueleza nia ya kutunga sheria ndogo kuanzisha Bodi ya Mfuko wa Elimu ambao kila mwananchi atachangia Sh10,000 kwa mwaka.

Katika tangazo kwa wananchi lililosainiwa na mkurugenzi mtendaji wa Manispaa ya Songea, Tina Sekambo, halmashauri imetangaza nia ya kutunga sheria ndogo sita za ada na ushuru; ushuru wa masoko na kodi ya vibanda vya biashara; ushuru wa maegesho ya magari; ushuru wa madini ya ujenzi; kilimo cha kahawa na uanzishwaji wa Bodi ya Mfuko wa Elimu.

Halmashauri imesema mtu yeyote mwenye maoni au pingamizi anatakiwa kuwasilisha kwa maandishi kwa mkurugenzi wa manispaa ndani ya siku 14 tangu siku ya tangazo hilo, ambayo ni juzi. Baadhi ya wananchi walijikusanya kwenye vikundi jana kusoma tangazo hilo lililobandikwa maeneo kadhaa wakilalamikia mchango kwa ajili ya elimu.

Akizungumza na Mwananchi, mkazi wa Majengo, Aidan Rwena baada ya kusoma tangazo lililobandikwa eneo la Soko Kuu alisema ushuru wa elimu iwapo utapitishwa utawafanya waishi kwa shaka kwa kuwa wengi wao hawana uwezo wa kulipa fedha hizo.

“Napinga ushuru huu, una lengo la kutukomesha wananchi. Tuna michango mingi na hali zetu ni ngumu ukisema kila mtu alipe Sh10,000 ni kuturudisha kwenye kodi ya kichwa, huu ni uonevu kwa wananchi wanyonge,” alisema.

Violeth Rungu, mkazi wa Namanyigu katika Manispaa ya Songea aliyesoma tangazo lililopo eneo la manispaa alisema limemsikitisha kwa kuwa kuna kodi nyingi za kulipa.

“Kuna kodi kibao, za majengo, ardhi, biashara bado tulipie na hii inayofanana na kodi ya kichwa, hapana! Watuonee huruma. Sina uhakika wa kupata fedha, familia ni kubwa Sh10,000 kwa watu kumi ni fedha nyingi,” alisema Violeth.

Diwani wa Ruhuwiko, Wilbroad Mahundi alisema hayatambui mapendekezo hayo kwa kuwa hakuna kikao kilichoyapendekeza.

“Siungi mkono kodi hiyo, kama mkurugenzi anadai ni kwa ajili ya mfuko wa kuchangia elimu tayari Serikali inatoa elimu bure. Waache kuwaumiza wananchi kwa kuwa hizo kodi ambazo ni kero tulishazikataza,” alisema. Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Ruvuma, Tito Mbilinyi maarufu Mwilamba alisema wanashangazwa na manispaa kuwarundikia kodi ambazo waliiomba Serikali Kuu kuwapunguzia zile ambazo zimekuwa kero.

Alipotafutwa na Mwananchi, mkurugenzi mtendaji wa Manispaa ya Songea, Tina Sekambo alisema elimu ni gharama hivyo iwapo wananchi wataridhia Sh10,000 zitaingizwa kwenye mfuko wa elimu.

Tina alisema hayo ni mapendekezo ya sheria ndogo za halmashauri na iwapo wananchi watayakataa hawatatozwa. “Naomba muwaelimishe wananchi wawe na amani, nawasiliana na mwanasheria ili kuondoa tangazo kwa kuwa naona limezua malalamiko mengi na linatukosesha amani,” alisema Tina.

This page might use cookies if your analytics vendor requires them.