Mfumo wa ununuzi luku wapata hitilafu

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  •  Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) latoa ufafanuzi, huduma kurejea leo Desemba 14, 2023

Dar es Salaam. Wakati wateja wakikosa huduma ya mfumo wa ununuzi wa umeme (Luku), kutokana na hitilafu iliyotokea, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema matengenezo yanatarajiwa kukamilika baadaye leo Desemba 14,2023.

Matengenezo yanafanyika kutokana na kuwapo hitilafu katika mfumo huo tangu saa moja asubuhi ya leo, Desemba 14, 2023.

Akizungumza na Mwananchi Digital, msemaji wa shirika hilo, Kenneth Byamonda amesema hitilafu iliyotokea imesababisha wateja kushindwa kununua umeme.

“Timu ya wataalamu wetu tayari wanaendelea na jitihada za utatuzi wa hitilafu iliyojitokeza. Wataalamu walipofanya tathimini ya hitilafu iliyojitokeza walitueleza hadi jioni ya leo mfumo utakuwa umerejea katika hali yake ya kawaida,” amesema Byamonda.

Tanesco kupitia taarifa kwa umma imewaomba radhi wateja kwa usumbufu unaojitokeza.

Shirika limeahidi kuendelea kutoa taarifa ya maendeleo ya upatikanaji wa mfumo yatakavyoendelea.

Kabla ya taarifa hiyo kutolewa, baadhi ya watu mitandaoni walikuwa wakilalamika kukosa huduma ya Luku kila walipotaka kununua umeme.

Tatizo kama hili liliwahi kutokea Mei, 2021, kwa siku takribani tatu wananchi walishindwa kununua umeme kupitia njia tofauti, hali iliyosababisha baadhi ya wateja kupata hasara katika biashara zao.

Mei 18, 2021, Tanesco ilitoa taarifa kwa umma ikieleza kukosekana huduma ya ununuzi wa Luku kulitokana na hitilafu katika mfumo wa ununuzi Jumatatu ya Mei 17, 2021.

“Jambo hilo lilisababisha baadhi ya wateja kushindwa kununua umeme, tunaomba uvumilivu wakati wataalamu wetu wanafanya kazi kuhakikisha tatizo hilo linatatuliwa haraka,” inaeleza taarifa ya Mei 18, 2021.